ILIPOISHIA........
Nilizidi
kuchanganyikiwa nilipoanza kuwatambua baadhi yao, kilichokuwa kinanishangaza ni
kwamba kila niliyemtambua alikuwa kashatangulia mbele ya haki tukamzika, yaani
namaanisha alishakufa kitambo.
SASA ENDELEA.......
Mtu wa kwanza
kumtambua alikuwa ni mzee Mboma, alionekana akitembeatembea huku uso wake ukiwa
umeghubikwa na huzuni.
‘Ni mambo gani haya jamani?’ Nilibaki
nikijiuliza.
Ni mwaka mmoja sasa
tangu tumzike mzee Mboma. Kifo chake kiliwashtua watu wengi sana pale mtaani, na siyo mtaani kwetu peke
yake; bali nchi nzima ilisikitishwa na kifo cha mzee huyo kutokana na
umashuhuri wake.
Ukianza kuongelea
waasisi wa chama kilichotukomboa kutoka kwenye utawala wa kikoloni hutomuacha
mzee huyu. Alikuwa ni mwanasiasa mkongwe ambaye alionyesha uanaharakati wake
katika kupigania uhuru wa nchi yetu na Afrika kwa ujumla.
Mzee huyo alitegemewa
sana pale mtaani kwetu kwa ushauri na kusuluhisha migogoro kutokana na busara
zake. Kitendawili kilijitokeza kufuatia habari za kifo chake, mpaka waleo bado
hakijateguliwa.
Hakufa kwa ugonjwa
wala hakuuliwa na mtu yeyote. Kwa kweli kifo chake kilizua gumzo kwenye vyombo
vya habari; kujiua kwa kujinyonga bila kujulikana sababu ni fumbo tosha ambalo
halijafumbuliwa mpaka sasa.
Alijinyonga mishale
ya saa kumi jioni kwa kutumia kamba ya usumba palepale nyumbani kwake. Hakuacha
waraka wowote kuelezea sababu zilizopelekea kuchukua uamuzi wa kujinyonga. Hata
mkewe hakuwa na hili wala lile juu ya kifo chake. Watu wengi huwa hawaamini
kuwa alijinyonga, lakini ukweli ndiyo huo.
Basi kitendo cha
kumuona mzee Mboma katika kundi lile kilinifanya nizidi kutaharuki.
‘Kwani mtu akifa huwa anarudi tena duniani?’
Hili ndilo swali lililofuatia baada ya kuvuta kumbukumbu za mzee huyo aliyekuwa
na busara sambamba na hekima mithili ya hayati baba wa taifa, mwl. Julius
Kambarage Nyerere.
Sijakaa sawa nikamtambua
mtu mwingine, mtu aliyekuwa muhimu sana na mhimili katika maisha yangu. Nilitamani
kumkimbilia ili nikamsabahi kwa kumkumbatia. Nilijisahau kabisa kuwa awali
nilishindwa kujongea japo ile hatua moja. Nilikosa jinsi baada ya kubaini kuwa
hali yangu ilikuwa bado iko vilevile, viungo vya mwili wangu vyote vilikuwa
havina nguvu mfano wa mtu aliyepooza.
Nilitaka kumuita
lakini nikaishia kugugumia kwani sikuweza hata kukifumbua kinywa changu.
Nilimung’unya mung’unya maneno utadhani bubu anayelalamika.
Kushindwa kwenda
kumkumbatia ndugu yangu huyo wa damu kuliniumiza sana moyoni. Nilishindwa
kupata uhakika ya kwamba na yeye alikuwa kaniona au la! Tatizo hata kuongea
kwenyewe sikuweza, japo ningemuita kwa sauti natumai angenisikia.
ITAENDELEA..........
No comments:
Post a Comment