ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Baada
ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga
siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.
SASA ENDELEA.......
Kwa namna moja au
nyingine nilifurahi kusikia hivyo kwani nilikuwa na shauku kubwa ya kujua hatma
ya hiyo kesi yangu. Japokuwa nilikuwa najua fika ya kwamba kuokoka kwangu
ilikuwa ni bahati nasibu, kitendo cha kupelekwa mahakamani na kupandishwa kizimbani
mara kwa mara kilikuwa kimeshanikifu.
Niliona ni heri
hukumu yangu ikitoka, hata kama nitahukumiwa kunyongwa basi nitakaa gerezani
bila bughudha siku zote za kungojea kunyongwa kwangu.
Niliteremka kizimbani
na kuchukuliwa na askari magereza kwa ulinzi mkali mpaka kwenye karandinga lao
kama ilivyo ada. Tulikaa kidogo kuwasubiri baadhi ya mahabusu ambao kesi zao
zilikuwa zinaendelea kusikilizwa. Baada ya kukamilika wote, tuliondoka
mahakamani na kuelekea magereza.
*****************************
Mwezi mmoja ulitimia
tangu siku ambayo kesi yangu ilisikiliza. Hayawi hayawi hatimaye sasa yakawa,
siku ya hukumu yangu iliwadia.
Mapigo ya moyo wangu
yalikuwa yakinidunda kasi kuliko kawaida. Pamoja na kwamba nilikuwa naiombea
siku ya hukumu ifike, siku hiyo nilikuwa nimenyong’onyea na kuwa mpole kama
shilingi mia.
Usiombe kuwekwa
kizimbani kwa mara ya mwisho ukisubiri hukumu, tena hukumu yenyewe ya kesi ya
mauaji! Hakika nilikuwa nipo maji siku hiyo.
Nilipandishwa
kizimbani huku nikiwa nimenywea pasipo mfano. Yaani ilikuwa ni tofauti kabisa
na siku zingine zote nilizofika mahakamani hapo.
Jaji alianza kusoma
hukumu yangu kwa kutaja kosa lililokuwa linanikabili na kutangulia kusema kuwa
adhabu ya kosa hilo ni kifo endapo mtuhumia atapatikana na hatia.
Niliposikia hivyo
moyo wangu ulilipuka pu kana kwamba ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kusikia hiyo
adhabu ya mtu mwenye hatia ya kuua.
Jaji huyo aliendelea
kwa kusema kuwa hakuna shaka yoyote kwa ushahidi ambao ulitolewa ya kuwa
nilimuua Kishoka Mpoto siku ya tukio hilo.
“Hata katika utetezi
wake mshtakiwa kashindwa kutoa maelezo sawasawa ambayo yanaweza yakailinda hoja
yake kuwa hajaua. Suala la kudai kuwa shahidi aliyetoa taarifa za tukio kituoni
ni mchawi au ni jini haliwezi likaaminiwa na mahakama hata siku moja kwani
hakuna uchawi juu ya sheria.” Aliendelea kutema maneno jaji Aneth Mwalukwa.
Aliendelea kusema
kuwa ushahidi wa picha, alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu
kilichokuwa kimetumika kumuulia Kishoka vilikuwa ni vielelezo tosha kabisa kunitia
hatiani.
“Japokuwa sababu au
chanzo cha mtuhumiwa kumuua marehemu hakijafahamika mpaka sasa kutokana na
mshtakiwa kuendelea kushikilia msimamo wa kwamba hajaua, bado haiondoi dhana ya
mtuhumia kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.” Alizidi kusema jaji huyo.
“Kazi yangu ilikuwa
ni kuchambua madai ya pande zote mbili, lakini upande wa utetezi umeonekana
kuwa na hoja ambazo hazina mantiki kabisa, hoja za kusingizia ushirikia. Katika
kusoma madai ya upande wa mshtakiwa sikuona shahidi yeyote ama ushahidi wowote
ulioonyesha kuwa ni kweli mtuhumiwa hajaua zaidi ya maneno matupu ya kudai kuwa
tukio liliambatana na ushirikina.” Aliunguruma mwanamama huyo.
Mpaka hapo matumaini
yalikuwa yameshaniishia kabisa. Nilijua fika kuwa mwisho wa hukumu yangu ni
adhabu ya kifo. Huku maelezo ya hakimu hayajafika mwisho nilianza kuhisi
machozi yakinilengalenga huku pua zangu zikionekana kuloa.
Jaji aliendelea
kusema kuwa jambo la shahidi aliyetoa taarifa polisi kutotokea kituoni haliwezi
likaleta shaka yoyote juu yake kwani jambo muhimu ambalo ni kutoa taarifa
alikuwa kashalifanya. Tena kwa kuongeza ushahidi aliamua kujitokeza mahakamani
na kutoa ushahidi wa picha ambao ulionyesha hali halisi ya tukio lilivyokuwa.
“Kutofika kituoni
huenda kulichangiwa na woga pamoja na kuchanganyikiwa kutokana na uzito wa
tukio jenyewe ulivyokuwa.” Aliendelea kufafanua jaji huyo.
Ulikuwa ni uchambuzi
ambao ulichukua karibu saa moja. Jaji Aneth Mwalukwa alihitimisha hukumu yake
iliyokuwa na kurasa kadhaa kwa kueleza kuwa anakubaliana na upande wa mashtaka
kuwa nilikuwa nimetenda kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya marehemu Kishoka
Mpoto.
“Kwa mujibu wa sheria
za nchi yetu mtu anayepatikana na kosa hilo, adhabu yake ni kifo. Kwa hiyo
natamka kwamba mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Brighton David kwa kosa
la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudi.
Jaji alinyamaza
kidogo kisha akanitazama na akuniambia,
“Mshtakiwa Brighton David nakuhukumu adhabu ya
kifo, utanyongwa kwa kitanza mpaka ufe.”
Jaji
alipomaliza kusoma hukumu yangu aligonga nyundo mezani kisha akainuka na
kuondoka.
Kwa
kweli sikuweza kujizuia. Nilijikuta nikiangua kilio cha haja huku simanzi na
huzuni zikitawala kwa watu wengi waliokuwa wamefika mahakamani hapo, wale
waliokuwa wananijua na hata wale ambao walikuwa hawanijui.
Wakati
jaji anaondoka mahakamani askari magereza walinishusha kizimbani na kuanza
kunipeleka kwenye karandinga la magereza bila hata kunipa nafasi ya kuagana na
baadhi ya watu niliokuwa najuana nao.
Kijana
niliyekuwa nimemuachia kuisimamia miradi yangu alikuja mbio akitaka kuongea
nami kwa mara ya mwisho, lakini bila huruma askari alinisukuma na kunitaka
niingie kwenye karandinga haraka.
Gari
lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani
**************************
HAYA SASA, HUKUMU IMESHATLEWA!
BRIGHTON ATANYONGWA KWELI AU ITAKUWAJE? ENDELEA KUFUATILIA!
No comments:
Post a Comment