Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata
hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa
kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Masharti
hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia
kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika
ajali ya kutisha.
SASA ENDELEA..........
Habari
hii ndiyo iliyonitonesha majeraha yaliyokuwa yamejengeka ndani ya moyo wangu
mithili ya donda ndugu. Kuanzia hapo nilianza kumchukia James na kumuona ni
shetani mkubwa ambaye alikuwa anastahili kutupwa kwenye moto wa jehanamu.
Nilijikuta
nahukumu wakati maandiko ya Mungu yanatuambia tusikuhumu ili na sisi tusije
tukahukumiwa. Niliumia sana nilipoambiwa hiyo habari.
‘Ndiyo
maana mambo ya kaka James yalianza kuwa safi mara baada ya vifo vya wazazi
wetu.’ Niliwaza.
Wakati
huo huo nikakumbuka swali, nikaona nimuulize huyo huyo Sharifa kwani hata yeye
alikuwa ni mdau wa kafara hizo.
“Umesema kafara ya daraja la kwanza inahusisha
wazazi wote wawili na ndugu mmoja wa damu, mbona sasa baba yangu alikufa wakati
hakuwa baba wa kumzaa James?”
“Kwa kuwa alikuwa kamuoa mama mzazi wa James
na pia alikuwa na mapenzi ya baba kwake, basi kafara yake ilifana.” Alijibu
Sharifa.
Akaendelea
kunieleza kosa la James lilikuja kutokea baada ya kutakiwa kutoa kafara
nyingine ili kukamilisha kafara za kwenye daraja la kwanza. Hapo alitakiwa
ndugu yake wa karibu; mdogo mtu, kaka mtu, shangazi ama mjomba.
Kwa bahati mbaya sana
ndugu wa damu aliyekuwa yu ngali hai nilikuwa ni mimi peke yangu. Aliamua
kukaidi kunitoa kafara kutokana na mambo mawili.
Jambo la kwanza ni
upendo uliokuwepo baina yangu na yeye. Kusema kweli kaka James alikuwa
ananipenda kupita kiasi, na ndiyo maana hakuwa tayari kunitoa kafara.
Jambo lingine
lililomsababisha kaka James agome kunitoa kafara ni kwamba hapakuwa na ndungu
mwingine wa karibu zaidi yangu mimi. Kama angenitoa kafara basi angebaki bila
ndugu wa karibu katika dunia hii. Sasa kubaki bila ndugu wa karibu lilikuwa ni
jambo gumu sana kwake.
Nadhani hata wewe
mpenzi msomaji usingepata fursa ya kusimuliwa simulizi hii nzuri iliyojaa
vitisho vya lejaleja na yenye kusisimua kwani ningekuwa tayari nimeshalala
mauti.
Baada ya kuona
kunitoa kafara haiwezekani, James aliacha kabisa kwenda kwa mganga aliyekuwa
amemfanyia dawa ya kumpa utajiri huo wakati alitakiwa awe anaenda mara moja kwa
mwezi kufanya ibada. Muda wa kukamilisha kafara ya daraja la kwanza ulipita
huku akiwa hajakamilisha, akaongezwa muda wa ziada nao ukawa umepita.
Mganga alipoona James
kapuuzia agano hilo aliamua kumripoti kwa wataalamu wake ambao ndiyo waliokuwa
wanamwezesha kufanya uganga huo.
Wataalamu hao
walikasirishwa sana na kitendo chake cha
kujifanya mjanja na mwenye akili kuzidi wao waliokuwa wamempa maagizo yale.
Ndipo walipoamua kumtoa duniani kwa staili ya kujiua mwenyewe ili akaonekane
ana dhambi hata mbele za mwenyezi Mungu.
Japo kabla ya kutoa
adhabu hiyo walitoa muda wa kutosha kwake wakitegemea labda angejirudi na
kukamilisha agano lao, siku zilizidi kwenda bila ya mabadiliko yoyote ya kutaka
kujirudi kwa James.
Tena alipoona kakaa
muda mrefu bila kupatwa na matatizo yoyote ilhali alikuwa hajakamilisha kutoa
kafara alijua kuwa huenda zile zote zilikuwa ni danganya toto tu na vitisho
visivyokuwa na misingi yoyote. Baada ya muda wa nyongeza kuisha uhai wa James
ukawa ni halali ya wataalamu hao.
Hayo ndiyo mambo
yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa ya kaka yangu
kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha yake na ya
wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila Sharifa ndiye
aliyekuja kuning’amua.
NINI KITAFUATIA? USIKOSE TOLEO
LIJALO!!!
No comments:
Post a Comment