Sunday, January 12, 2014

Simulizi: Nimekosa nini? sehemu ya 1

                                                                 NIMEKOSA NINI?


Alfajiri na mapema niliamka. Sikuamka kwa bahati mbaya muda huo bali ilikuwa ndiyo kawaida yangu kila siku. Nilikuwa nikiamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kwenda katika mihangaiko yangu ya kila siku.
                Ingawa siku hiyo nilikuwa kwenye mtoka kisha nikachelewa sana kurudi nyumbani, sikuwa na budi ya kujidamka asubuhi na mapema ili niende kazini.
                Baada ya kupiga mswaki niliingia maliwatoni kujiswafi. Nilipomaliza nilirudi chumbani kwangu, nikauramba kama ilivyokuwa ada kila nilipokuwa naelekea kazini.
                Nilichukua suruali yangu niliyokuwa nimevaa jana yake nilipokuwa kazini ili nichukue pochi iliyokuwa kwenye mfuko wa suruali hiyo kwani humo ndiyo kulikuwa na nauli yangu ya kunipeleka kazini na kunirudisha nyumbani.
                “Umeiona pochi yangu mama Chris?” Nilimuuliza mke wangu aliyekuwa kajilaza kitandani kwa wakati huo.
“Hata sijaiona, kwani ulikuwa umeiweka wapi?” Aliuliza.
“Nakumbuka jana nimeenda nayo kazini, lakini nimeangalia kwenye suruali niliyokuwa nimevaa sijaiona.”
“Mh! Sasa itakuwa wapi?”
“Kama vipi achana nayo kwa sasa, acha niende kazini nikirudi nitakuja niitafute vizuri! Cha kufanya sasa hivi nipe shilingi elfu kumi kwa ajili ya nauli.” Niimwambia mke wangu naye akainuka na kunichukulia kwenye droo ya kitanda kisha akanipatia.
                Nilimuaga mke wangu kwa kumbusu kwenye paji la uso kisha nikamalizia kwa mwanangu kipenzi  aliyekuwa bado kalala.
“Kila la heri mume wangu, nakutakia kazi njema!” Yalikuwa ni maneno ya mke wangu kipenzi mama Chris, maneno  ambayo alikuwa akiniambia kila siku nikiwa naelekea kazini.
“Asante mama, na wewe nakutakia siku njema, utamsalimia mwanangu Chris atakapoamka.” Nilijibu huku nikichana chana nywele zangu huku nikijiangalia kwenye kioo kikubwa kilichokuwepo kwenye meza ya kujirembea iliyokuwemo humo chumbani.
                Nilipoanza  kuondoka mama Chris akanishika mkono,
“Ngoja kwanza baba wewe!”  Alitamka maneno yale wakati akiuvuta mkono wangu!
“Nini tena mama?” Nilihoji kwa lugha ya kubembeleza nikidhani kuwa labda mama Chris anataka mambo yetu yale ya mchezo wa kikubwa, maana katika kumbukumbu zangu usiku huo timu zote zilikuwa kambi kwani mwenzangu alikuwa katika sherehe zake za kila mwezi.
                “Hii tai haijakaa vizuri mume wangu, angalia na hii kola ya shati lako shingoni ilivyokaa shaghala baghala, utaenda unachekwa njia  nzima!” Aliongea wakati akinirekebisha huku tabasamu lake mwanana akilitoa.
“Nitachekwa mimi au utachekwa wewe mke wangu maana umeshindwa kunikagua wakati natoka!”
“Mimi sitachekwa  sababu sitakuwepo huko.” Aliongea mke wangu huku akihamia kwenye tai kuiweka sawa.
                Alipomaliza kuyaweka sawa mavazi yangu nilimkumbatia tena kwa mara nyingine na kumpiga mabusu motomoto kisha nikatoka zangu. Nilienda mpaka stendi kugombania daladala, si unajua tena usafiri wetu wa huku Bongo.
                Sikuchelewa kupata gari, nikapanda na kwenda kushukia posta mpya kisha nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea ofisi yetu ilipokuwa.
                Nilipofika ofisini nilipigwa na butwaa baada ya kuwakuta watu wamejazana. Kwa haraka haraka nikaanza kuhisi kuwa kuna tukio kubwa ambalo lilikuwa limetokea. Watu walikuwa wameuzunguka mlango huku polisi wakiwa wanarandaranda.
                Maswali mia mia yakaanza kuzunguka katika akili yangu bila kupata majibu. Kwa kuwa nilikuwa tayari nipo kwenye tukio lenyewe, nilipiga moyo konde na kujiambia kuwa muda si mrefu nitakijua kilichojili.
                “Halafu linaonekana ni tukio kubwa sana, yaani mpaka polisi wamekuja!” Nilijiwazia huku nikitembea kwa tahadhari kuelekea ofisini.

ITAENDELEA........

Wednesday, January 1, 2014

Tanzia. WAZIRI WA FEDHA NCHINI TANZANIA AFARIKI DUNIA!!!

Breaking news!!!
WAZIRI WA FEDHA NCHINI TANZANIA MH DR. WILLIAM MGIMWA AFARIKI DUNIA!






Waziri wa Fedha, Dk. William Augustao Mgimwa (63) amefariki dunia.

Taarifa za hivi punde zinasema Waziri huyo wa fedha katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete amefariki dunia hii leo baada ya kuugua na kulazwa nchini Afrika Kusini.

Mgimwa aliyezaliwa January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Binafsi ya Milpark ya nchini humo.

Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Hospitali hiyo ya Milpark ndiyo imekuwa ikitumiwa na Serikali ya Tanzania kupeleka watu wanaoumwa na mtu wa karibuni zaidi kuhudumiwa katika hospitali hiyo ni marehemu Dk. Sengondo Mvungi.

HIKI NDICHO ALICHOANDIKA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI ZITTO KABWE KWENYE UKURASA WAKE WA FACEBOOK MUDA MCHACHE ULIOPITA


Tanzia Waziri wa Fedha William Mgimwa, Mb

Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Waziri wetu wa Fedha ndg. William Mgimwa.

Kwa kipindi kifupi nilichofanya naye kazi kwa karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha (nikiwa mkaribishwa kama Waziri wa Fedha kivuli), kisha kwenye kamati ndogo niliyounda kuhusu miradi ya Umeme ya Mchuchuma na Liganga na Ngaka, na baadaye akiwa Waziri wa Fedha, jambo la msingi nilioona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa aliyonayo kwa watu wengine.

Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti za kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi kuliko wengine wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa Kamati za Mahesabu.


Uzalendo wake hauna mashaka na kujituma kwake katika kazi ni tabia ya kupigiwa mfano.

Mungu ameamua kumchukua mja wake na sisi wanadamu hatuna uwezo wa kupinga.


Nawapa pole sana familia yake kwa kumpoteza baba yao mpendwa. Naomba mola awape moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.

Nawapa pole wananchi wa Jimbo la Kalenga na Halmashauri ya Wilaya Iringa kwa kupoteza kiongozi wao.

Mola ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amina
Share this article :