ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Yangu
macho na masikio siku hiyo, lakini mimi nimeshamnyanyulia mikono huyo ibilisi.
Nashangaa sijui kwa nini kaniandama sana na kunisababishia ndege mbaya katia
maisha yangu, kanipotezea dira ya maisha kabisa, isitoshe hata hatima yangu
haijulikani.” Nilijikuta nikiongea kwa uchungu huku nikionyesha kukata tamaa
kwa hali zote.
SASA ENDELEA.......
“Tatizo
lako wewe ni mwepesi mno wa kukata tamaa. Hebu hakikisha unapambana mpaka
dakika ya mwisho.”
“Nitapambana vipi kaka wakati hali ninavyoiona
inazidi kuelekea kubaya tu. Hebu jiulize hizo alama za vidole vyangu
zimeonekanaje kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu wakati sikuwahi hata
kugusa?”
“Huenda ulishika bila kijielewa kutokana na
kuchanganyikiwa na tukio.”
“Hakuna kitu kama hicho kaka, mimi hata
nichanganyikiwe vipi lakini huwa najielewa.”
“Basi yote hayo tumwachie Mungu, yeye ndiye
atakayeamua kuwa tushindwe au tushinde hii kesi.”
“Mimi nahisi hata Mungu kashanipa kisogo, haya
siyo matatizo ya kwanza kwangu, walianza wazazi wangu wakafariki, kipenzi
changu Ana naye akanitoka kimzahamzaha. Haikuishia hapo tu, kaka James ambaye
alikuwa ndiyo nguzo yangu ya pekee iliyokuwa imebakia, naye akafariki dunia,
tena kifo cha ghafla ghafla tu.” Nilijikuta nikimshtakia Mungu kwa wakili huku
machozi yakianza kunibubujika kwenye mifereji ya mashavu yangu.
Ndipo
mlango ulipofunguliwa kisha askari magereza akaingia na kumtaka wakili aondoke
kwani muda wa kuendelea kuongea na mimi ulikuwa umefikia kikomo.
Wakili
aliniaga na kuniambia atakuja kunipa taarifa pale tarehe ya kesi yangu
itakapopangwa. Aliondoka na kuniacha nikifutafuta machozi ambayo yalikuwa
yameshaanza kukolea kutokana na kuyaamsha machungu yaliyokuwa yamejilaza
moyoni; machungu ya kuondokewa na watu wangu muhimu katika hii dunia ambao ni
wazazi wangu, kaka James na kipenzi changu Anna.
Mawazo
juu ya msichana huyo ambaye nilikuwa nimembatiza jina la Ibilisi yalianza
kuzunguka kunako kichwa changu. Hata hivyo sikuweza kupata jibu ni kwa nini
msichana huyo alikuwa ameniandama kiasi kile.
Niliendelea
na maisha ya gerezani ingawa nilikuwa ni mahabusu. Mpaka muda huo nilikuwa bado
sijayazoea kabisa maisha ya huko, ilikuwa ni ngumu sana kwangu kuyazoea maisha
ya huko.
Siku moja kabla ya
kesi yangu kuendelea wakili alikuja kunipa taarifa. Hata hivyo alipokuja
aliniambia habari nyingine ambayo ilizidi kunichanganya zaidi.
Alisema kuwa siku
aliyotoka kuongea na mimi kwenye hospitali ya magereza alikutana na msichana
aliyekuwa akitusumbua katika kesi hiyo. Msichana aliyekuwa amenisingizika kuwa
nimeua wakati sijaua.
MH! HAYA SASA, WAKILI WA BRIGHTON
ANAKUTANA NA YULE MSICHANA HATARI. JE,
ATAAMBIWA NINI? USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment