Brighton anaota
ndoto ya ajabu akiwaona watu waliokufa siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee
Mboma, Patrick, James na Anna. Baada ya ndoto hiyo anazongwa na mwanadada
Sharifa anayemsababishia kesi ya mauaji ya mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi
inaunguruma mahakamani kisha anajikuta akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka
afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa
gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa
amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James, naye Mack anaanza kumhadithia kisa
kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. Hatimaye siku ya kunyongwa inafika kweli, hata
hivyo anajikuta anakolewa kimiujiza na msichana aliyemsingizia kuua, yaani
Sharifa, anatolewa gerezani na kuwa huru kabisa.
Anaporudi
kwake anakuta nyumba yake ishauzwa na mtu aliyekuwa amemwachia. Sasa endelea...................
Hata hivyo
nilijishauri mwenyewe kuwa kama ningeenda kwenye nyumba hiyo basi ningeonekana
kwa watu wengi, na hofu yangu ilikuwa ni kuvuja kwa siri ya kutoroka gerezani.
Nilijua
fika dunia haina siri na walimwengu hawana dogo. Kitendo cha kuniona tu basi
wangeanza kuhoji kutaka kujua kulikoni. Watu wengi walikuwa wanajua fika kuwa
mimi nilihukumiwa kifo, sasa kuonekana pale mtaani kungeweza kuzua gumzo na
kuniletea matatizo mengine tena, huenda ningejikuta nakamatwa na vyombo vya
dola.
Hata
wakati naenda kwenye nyumba yangu hiyo nilienda kwa kujificha ficha sana ili
nisionekane kwa watu wa mtaa ule. Lengo langu lilikuwa ni kwamba nifike kwa
Mapara na kumwambia tufanye mipango ya kuhama mji huo kinyemera na kuenda
katika mji mwingine ambao ingekuwa vigumu watu kunishtukia.
Akili
yangu ilikuwa imenituma kuuza kila kitu kisha kutimkia mji wa mbali ambako
ningeweza kuishi kwa raha zangu bila kushtukiwa mpango wangu wa kutoroka jela.
Sasa
kitendo cha kuambiwa Mapara hakuwa anaishi hapo tena kiliichokesha akili yangu
mara dufu. Nikawa nawaza cha kufanya bila kupata majibu.
Jamaa
baada ya kuniona nimekaa kimya kirefu nikiwaza kwa kina huku nikipiga miayo
mfululizo isiyo na idadi; aliamua kuzama ndani kisha akafunga geti ‘paa!’
Nilibaki pale nje peke yangu nikiwaza na kuwazua bila kupata muafaka wa mawazo
yangu.
Hatimaye
niliamua kuchukua maamuzi ya hatari kwani sikuwa na jinsi.
‘Potelea mbali kifo hakina breki, ngoja niende
hapo hapo alipokuwa kapanga Mapara ili nikajaribu kuulizia kama bado kapanga
hapo au la!’ Nilijishauri na kuanza kuondoka.
Kwa
jinsi nilivyokuwa nimekonda ilikuwa ni vigumu sana kwa mtu yeyote aliyekuwa
akinifahamu kugundua kwa haraka kuwa ndiyo mimi. Ukizingatia miaka mingi
sikuwepo mtaani hapo na pia watu walikuwa wameshanifuta hata katika fikra zao
kutokana na hukumu niliyokuwa nimepewa, yaani hukumu ya kunyongwa; basi
niliweza kupishana nao kama vile hatujuani.
Nilienda
moja kwa moja mpaka kwenye nyumba alimokuwa kapanga Mapara. Nikaingia mpaka
ndani ya nyumba hiyo. Moja kwa moja nilienda mpaka kwenye chumba alichokuwa
akikaa.
Nilipogonga
ilisikika sauti ya mwanamke ikiniitikia.
‘Huyu jamaa kashavuta jiko nini?’ yalikuwa ni
mawazo yangu baada ya kuisikia sauti ya mwanadada huyo.
Mara
mwanamke mrembo alifungua mlango na kutoka kidogo kisha akasimama mlangoni kwa
mtindo wa kuegemea mlango. Alikuwa ndani ya kanga tu lakini kanga hizo zilikuwa
ni mbili, ya kwanza ilikuwa imeanzia kifuani kuyafunika maziwa na ya pili
ilikuwa imeanzia kiunoni.
Nilimsabahi
naye akaitikia. Kilichofuata baada ya salamu ni kumuuliza habari za Mapara.
“Mh! Mapara, mbona simfahamu?” Alijibu
mwanamama huyo aliyekuwa na uzuri wa shani.
Baada
ya kujibiwa hivyo moyo wangu ulishtuka utadhani umepigwa shoti ya umeme. Tumbo
likawa joto kwani dalili za mambo kuzidi kuniwia ugumu zilikuwa
zinajidhihirisha waziwazi. Wahenga walisema dalili ya mvua ni mawingu, pia
mwanzo wa ngoma siku zote huwa ni lele.
“Kwani
wewe siyo mpangaji wa siku nyingi hapa?” Nilimhoji mama huyo.
“Ndiyo sina siku nyingi hapa, nina miezi kama
mitano hivi tangu kuhamia kwenye hiki chumba.”
“Ndiyo maana, kwa maana Mapara alikuwa kapanga
kwenye chumba hikihiki na ni muda mrefu
umepita tangu nifike kumsabahi.”
“Labda muulize kaka wa kwenye chumba kinachofuata kwani huwa nasikia yeye ndiyo
mkongwe zaidi hapa.”
“Sawa, asante kwa msaada wako.”
“Wala usijali, karibu tena.”
“Nimekaribia.” Nilijibu kisha nikaondoka kwa
hatua za taratibu kabisa mpaka kwenye chumba kilichofuata.
Kwa
adabu zote nilianza kuugonga mlango. Sikujibiwa chochote. Mle ndani kulikuwa na
mdundo wa redio uliokuwa ukikita kwa sauti utadhani ni ukumbi wa disko.
Niliamua
kugonga tena kwa kuamini kuwa labda nilipogonga kwa mara ya kwanza hawakusikia
kutokana na makelele ya redio. Tena safari hii nililazimika kuukaza mkono ili
kuwafanya waliokuwemo humo ndani wanisikie.
JE, HICHO CHUMBA ANAISHI NANI? NA
JE, BRIGHTON ATAPATA UFUMBUZI WA MASWALI YAKE? USIKOSE KUSOMA TOLEO LIJALO.
No comments:
Post a Comment