KWA WASOMAJI WAPYA.....
Brighton anaota ndoto ya ajabu akiwaona watu waliokufa
siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick, James na Anna. Baada ya
ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa anayemsababishia kesi ya mauaji ya
mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi inaunguruma mahakamani kisha anajikuta
akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa
ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa
anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James,
naye Mack anaanza kumhadithia kisa kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. sasa
endelea...................
Alipopandishwa
kizimbani kwa mara ya kwanza alisomewa mashtaka kisha akatakiwa kutojibu
chochote kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kusikiliza kesi kama hiyo,
yaani kesi ya mauaji.
Aliendelea kukaa
rumande wakati taratibu za upelelezi wa kesi yake zikiwa bado hazijakamilika.
Jalada lake lilipokamilika kesi yake ilihamishiwa kwenye mahaka kuu.
Kesi iliendelea
kurindima. Kitu kilichomuacha hoi Mack ni yule shahidi namba moja wa kesi hiyo
ambaye alijitambulisha kuwa ni mume wake
na Sada, yaani mwanadada aliyekuwa ameuawa.
Mack alishangaa
kumuona shahidi huyo ndiye jamaa aliyekuwa ameuliwa na kaka James kwa kupigwa
risasi baada ya kumkuta na Neila ambaye alikuwa ni mpenzi wake (yaani kaka
James). Kijasho chembamba kilianza kumtoka.
Jamaa alitoa ushahidi
wake akidai kuwa siku ya tukio alikuwepo na alimshuhudia Mack wakati anafanya
mauaji.
Kilichozidi
kumchanganya Mack na ndiyo hicho hicho kilichokuwa kinazifanya kesi zetu ziwe
mapacha ni ushahidi wa ule mkanda uliorekodiwa na kamera maalum za nyumba hiyo
ukionyesha mwanzo mpaka mwisho wa tukio.
Mack hakuua. Tena
maskini wa Mungu alikuwa haijui hata hiyo nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke
huyo. Ni sawa kweli alikuwa na wenyeji kidogo kwenye mtaa wa Matopeni, lakini
alipokuwa akikaa Sada alikuwa hapajui na ndiyo maana alichemsha kumpata siku
alipoenda kumtafuta.
Yale yale kama
yaliyotokea kwangu, kuonekana alama za vidole vyangu kwenye mwili wa Kishoka na
kwenye kisu wakati sikuwahi hata kuvigusa. Tena hiyo ni tisa, kumi kuonekana
picha zangu kwenye kamera nikimchinja Kishoka wakati sikuhusika abadani!
Mwisho wa siku Mack
alihukumiwa kunyongwa mpaka afe kwa kosa la kumuua Sada kwa kukusudia. Hivyo
ndivyo stori ilivyoenda kwa mujibu wa maelezo yake.
Nilivuta pumzi ndeefu
kisha nikaishusha baada ya kumaliza kusimuliwa simulizi hiyo na Mack mwenyewe.
“Mbona kama kuna
zengwe fulani hivi kwenye mirathi ya kaka James? Maana mambo yanayotokea
siyaelewielewi!” Nilitamka maneno hayo nikimwambia Mack.
“Na hayo matatizo siyo kwetu sisi peke yetu
tu, takribani watu wote uliowauzia mali za huyo marehemu kaka yako wamepatwa na
matatizo!” Alisikika Mack na kuzidi kunipa mpasuko wa moyo.
Sasa
moyo wangu haukuwa na amani tena. Niliishiwa nguvu mithili ya mtu anapoletewa
msiba wa mtu ampendaye kwa dhati. Hata hivyo hamu ya kutaka kujua kilichojiri
kwa wateja wangu hao ilizidi kunifukuta.
“Mungu
wangu! Ni matatizo gani yaliyowapata?” Nilijikuta nikiuliza kwa mshangao
mkubwa.
“Yule jamaa uliyemuuzia ile kampuni ya
usafirishaji hayupo tena duniani.”
“Wewe! Kunesa alishafariki? Ilikuwaje?”
Nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa huku nikiuliza maswali dabodabo.
Mack
alianza kunieleza yaliyojiri huko moja baada ya jingine. Alianza na habari za
huyo Kunesa, jamaa niliyekuwa nimemuuzia kampuni ya usafirishaji niliyokuwa
nimerithi kutoka kwa kaka yangu.
Alinieleza
jinsi kifo cha Kunesa kilivyokuwa. Japokuwa hata yeye hakuwepo huko wakati kifo
hicho kinatokea ila alisimuliwa na baadhi ya ndugu na jamaa zake waliokuwa
wakienda kumuona pale gerezani.
Alieleza
kuwa Kunesa alikutwa kafa kwenye ofisi yake. Alikuwa kachinjwa huku kichwa
kikiwa mbali na kiwiliwili chake. Aliyefanya tukio hilo hajajulikana mpaka wa
leo.
Nilipouliza
watu wengine waliokumbwa na matatizo nikaambiwa ni wale jamaa waliokuwa wameyanunua
yale magari. Waliyakuta magari yanawaka moto yenyewe kwa nyakati tofauti na
chanzo cha moto huo wala hakikujulikana. Habari hizo zilizidi kunipa wasiwasi
mkubwa juu ya mali za kaka James. Nikazida kujiuliza kulikoni kuhusu hizo mali.
Walionunua
maduka walifilisika wote, maduka yaliisha na kubakia matupu kabisa. Nilianza
kuwaza endapo watu hao wangeamua kunitafuta sijui wangenifanya nini!
“Na
wewe umefikaje kwenye gereza hili wakati hata huko mahakama kuu ipo pamoja na
magereza ya kutosha kabisa.” Niliona nimuulize Mack swali hilo lililokuwa
linanitatiza tangu nilipomuona tu.
“Afya yangu ilianza
kuwa mgogoro mara baada ya kufungwa. Ndipo daktari wa hospitali ya gereza hilo
akashauri kwamba nihamishiwe gereza jingine akidai kuwa hali ya hewa ya pale
ilikuwa imenikataa. Ndipo nilipoletwa huku.”
Kwa
kweli zilikuwa ni habari nzito za kutisha na kusikitisha. Nilianza kujiona kuwa
ni muuaji kwani mtu kama Kunesa nilihisi kuwa nina mchango mkubwa mno juu ya
kifo chake, ukizingatia nilimbembeleza kuinunua hiyo kampuni baada ya kukosa
mtu wa kuinunua.
Hiyo
ilikuwa ni siku ya kwanza kukutana na Mack, siku ambayo ndiyo kwanza nilikuwa
nimetoka mahakamani kuhukumiwa.
***************************
DUH! HIZO MALI ZA URITHI WA
BRIGHTON KUTOKA KWA KAKA YAKE ZINA NINI? MBONA KILA ALIYEZINUNUA ANAPATA
MATATIZO? USIACHE KUFUATILIA SIKU SI NYINGI UTALIPATA JIBU!
No comments:
Post a Comment