ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Jaji
aliiahirisha kesi na kutaja tarehe nyingine ambayo ingeendelea kusikilizwa.
Nilitolewa kizimbani na kupelekwa kwenye karandinga la magereza tayari kabisa
kwa kurudishwa mahabusu.
SASA ENDELEA.......
Ilikuwa ni kesi
iliyonipa wakati mgumu sana kwa kipindi chote nilichokuwa mahabusu nikisubiri
hatima yake. Kila wakati nilikuwa siishi kuwa na wasiwasi mithili ya mbuzi wa
shughuli.
Wasiwasi
pamoja na kuwaza huko kulizidi kuifanya afya yangu izidi kuwa mgogoro zaidi ya
vile ilivyokuwa awali. Niliiona kesi inapelekwa polepole sana, nikawa natamani
bora nihukumiwe ili nijue moja, kama kusubiri kunyongwa ama kuponea kwenye
wokovu wa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.
Pamoja
na maneno ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama ya kunitia moyo na
kunihakikishia kuibuka kidedea katika kesi hiyo, bado nilikuwa naona kama
ananikebehi na kunipa faraja za kijinga kwa vile niliamini kabisa kuwa hata
yeye alikuwa anauona ugumu wa kesi yangu ulivyokuwa.
Kibaya
zaidi sikuwa hata na shahidi ambaye angesimama kizimbani na kujaribu kunitetea.
Kesi yenyewe ilikuwa imejaa utata mtupu. Hata wewe mpenzi msomaji uliona wapi
alama za vidole zionekane kwenye kitu ambacho hukuwahi hata kukishika? Huo ni
utata, kama siyo kubambikiwa basi ni kiini macho.
Tarehe
ya kusikilizwa tena kesi yangu iliwadia. Siku hiyo tena upande wa mashitaka
ulitakiwa kupeleka mashahidi wake wawili. Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani
kutoa ushahidi alikuwa ni Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Kishoka.
Akiwa
kizimbani huku akiongozwa na mwendesha mashitaka, daktari huyo alieleza jinsi
alivyoupokea mwili wa marehemu Kishoka na kuufanyia uchunguzi. Baada ya hapo
alitoa maelezo ya ripoti ya postimotam kabla ya kuwasilisha nakala ya ripoti
hiyo kwa Jaji.
Wakili
wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kumuuliza shahidi huyu hivyo hakutumia
muda mrefu sana kumhoji alipokuwa kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.
Ripoti
ya daktari huyo ilikiri kuwa kweli Kishoka aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye
ncha kali mpaka akapoteza uhai wake.
Baada
ya shahidi huyo kutoa ushahidi, upande wa mashitaka ulitakiwa kupeleka shahidi
mwingine. Shahidi aliyekuwa ameandaliwa ni mmoja wa askari waliokuwa wamekuja
nyumbani kwangu kuja kunikamata baada ya kupewa taarifa za kifo cha Kishoka.
Nilimuona
mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali akisimama na kumwambia jaji
kuwa shahidi aliyetakiwa kupanda kizimbani haonekani na huku alikuwepo wakati
mahakama inaanza.
“Hata
hivyo kuna shahidi mwingine kajitokeza ambaye ni muhimu sana katika kesi hii.
Mtu mwenyewe ni yule mwanamke aliyetoa taarifa za awali kituo cha polisi
kuhusiana na kifo cha Kishoka.” Nilimsikia mwendesha mashtaka akimwambia jaji.
Moyo
ulinilipuka puu baada ya kusikia kauli hiyo. Tumbo langu likachemka ghafla huku
maswali mia mia nikijiuliza ya kuwa huyo mtu aliyetoa taarifa kituoni
akinisingizia kuua ni nani.
Hata
hivyo kwa upande mwingine nilifurahi ili nimuone mtu huyo mwenye moyo wa
kinyama na roho ya kishetani kwa kunisakizia kwesi ya mauaji ilhali sikuua.
Baada
ya jaji kuruhusu shahidi huyo apande kizimbani, nilimuona dada mmoja akiinuka
na kuanza kutembea mwendo wa maringo kuelekea kwenye kizimba cha kutolea
ushahidi.
Kitendo
cha kumuona mwanadada huyo kilinifanya nianze kuhisi kupumua kwa shida huku
mwili wangu ukianza kuishiwa nguvu. Pumzi zilizidi kubana, ghafla nilijiona
nikianguka mzima mzima huku macho yangu yakipoteza upeo wa kuona. Kabla
sijafika chini niliacha kujitambua na kupoteza fahamu ghafla.
No comments:
Post a Comment