ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Mpaka
anafikishwa hospitali mama yangu alikuwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa kaumia
vibaya sana
************************
SASA ENDELEA.......
Taarifa za ajali
ziliwafikia wazazi wa mama majira ya mchana, walipigiwa simu na mwalimu mkuu wa
shule aliyokuwa akisoma mama na kuambiwa kuwa mtoto wao kapata ajali katika
moja ya basi lililokuwa likienda mji jirani muda mchache baada ya kutoka mjini
hapo.
Walishangaa sana
kusikia habari hiyo, wakaanza kujiuliza mtoto wao alikuwa kapanda gari hilo
kuelekea wapi! Walipojaribu kumuuliza mwalimu kuwa labda alikuwa na taarifa na
hiyo safari naye aliruka kimanga na kudai hana ajualo.
Hapo ndiyo wazazi
walizidi kuchekecha akili wakijiuliza kuwa mtoto wao alikuwa anasafiri kuenda
wapi na ni kwa nini aondoke bila ya kuaga ama kutoa taarifa?
Hata hivyo hilo
halikuwa la kujadili sana kwa wakati huo, kilichokuwa cha msingi kwa wakati huo
ni kwenda hospitali kumuona mtoto wao, hata hayo maswali yao yote yangeweza
kupata majibu hukohuko kwa kumuuliza mwenyewe.
“Au labda alikuaga
wewe lakini unanificha tu?” Ilikuwa ni sauti ya babu yangu akimuuliza mkewe
wakati gari yao inachoma mafuta kuelekea hospitali aliyokuwa kalazwa mama.
“Aka! Mimi sijui chochote kuhusu safari hiyo,
atakuwa kajiamulia mwenyewe.”
“Maana nyie wanawake wakati mwingine huwa
mnakula njama na watoto wenu hasa hasa watoto wa kike.”
“Mimi siwezi nikafanya ujinga kama huo.”
Mara
baada ya maongezi hayo ukimwa ulitawala katika safari hiyo. Hawakuchukua muda
wakawa wamefika kwenye hospitali ambayo majeruhi na maiti waliopatikana katika
ajali ya asubuhi walikuwa wamehifadhiwa.
Wakaanza
kumtafuta mtoto wao kwenye wodi walizokuwa wameweka majeruhi. Kwa bahati nzuri
hawakuhangaika sana wakawa wamemuona, ila alikuwa bado hajazinduka.
Fahamu
zilimrudia muda wa usiku, akashangaa kujiona yupo hospitali huku akiwa na
majeraha mwili mzima. Hata hivyo tukio zima alilikumbuka mara baada ya kuvuta
kumbukumbu. Ndipo akakumbuka kuwa
alikuwa akitoroka kwa kuogopa kugundulika nyumbani ya kuwa ni mjamzito.
Akili
yake ikamtuma kuwa huo ndiyo ulikuwa ni muda muafaka wa kuomba radhi kwa wazazi
wake kwani hata zile hasira za baba yake zisingewaka sana juu yake kwa vile
alikuwa anaumwa na yupo hospitali. Alijua fika mpaka kuja kupata nafuu baba
yake atakuwa kashapunguza hasira kama siyo kuisha kabisa na hapo asingekipata
kichapo cha paka mwizi.
Kesho yake asubuhi
baba na mama yake walikuwa wameshafika hospitali hapo kumjulia hali. Kwa wakati
huo hali yake ilikuwa inaendelea vizuri ingawaje alikuwa bado ana maumivu
makali.
Ndipo alipopata fursa
ya kuwaeleza wazazi wake kinaga ubaga juu ya tatizo lililokuwa likimsumbua
kiasi kwamba mpaka akachukua uamuzi wa kutoroka nyumbani.
“Huyo bwege aliyekupa
ujauzito huo ni nani na yuko wapi?” Lilikuwa ni swali la baba yake baada ya
kusikia hivyo.
“Kashakimbia, hicho nacho ndicho kimechangia
kunifanya nichukue uamuzi huo kwani ana wiki mbili sasa hayupo.” Alijibu mama
yangu kwa shida.
“Jamani, mimi sioni sababu yoyote ya kuanza
kuyajadili mambo haya huku hospitali, haya mambo ni ya kuyajadili tukiwa
nyumbani.” Aliingilia kati bibi yangu.
Hata
hivyo mama alikuwa na hofu kwamba maelezo hayo akiyatoa wakiwa nyumbani
yanaweza yakaupandisha ‘mzuka’ wa baba yake na kuanza kumshushia kichapo.
Lakini alipiga moyo konde na kusema litakalokuwa na liwe. Kizuri zaidi alikuwa
tayari kashatoa utangulizi wa jambo hivyo hasira za baba yake zisingekuwa
nyingi sana.
Baada
ya wiki moja mama yangu aliruhusiwa kutoka hospitali, afya yake ilikuwa
inaimarika vizuri ingawaje majeraha mengine yalikuwa hayajapona ikiwemo mkono
wake ambao ulikuwa umevunjika hivyo alikuwa kawekewa ‘p.o.p’
Siku
hiyo hiyo alipofika nyumbani hakutaka kulaza damu, aliianzisha tena mada kwa
kuwaomba msamaha wazazi wake kwa kile kilichokuwa kimejitokeza.
Suala
hilo liliongelewa na kufikia muafaka, akawa ameambiwa asiwe na wasiwasi kwani
kuteleza si kuanguka.
“Usiwe na wasiwasi mwanangu mimi na mama yako
tumeshakusamehe, ila ole wake huyo mpumbavu aliyejifanya rijali apatikane, hapo
ndiyo atajua kuwa kumbe koti huwa halichomekewi, atajuta kuzaliwa.” Mzee wa
kazi alimalizia kuongea kisha akaondoka zake.
Mama
aliendelea kuilea mimba yake akiwa nyumbani. Mpaka miezi tisa ilipoada ndipo
alipojifungua mtoto wa kiume ambaye ndiyo alikuwa kifungua mimba wake, huyo
hakuwa mwingine bali ni kaka James.
Kuzaliwa
kwa kaka James ndiyo kulikuwa hivyo. Wakati huo mimi nilikuwa bado sijafikiriwa
hata kuiona hii dunia. Nilikuwa bado nipo mbinguni nikicheza na kufurahia tu na
malaika.
ITAENDELEA......
No comments:
Post a Comment