ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Mpaka
namaliza kidato cha sita alikuwa ni tajiri wa kuogopeka mji mzima. Alikuwa na
magari mawili ya kifahari na nyumba mbili za kifahari.
SASA ENDELEA.......
Tulihamia kwenye
nyumba moja na kuanza kuishi pale. Mambo yalizidi kuwa safi kwa kaka James.
Nilizidi kupata wasiwasi kwa jinsi utajiri wake ulivyokuwa ukiongezeka kila
kukicha.
Kati ya miradi mikubwa
aliyokuwa nayo ni pamoja na kampuni ya usafirishaji ambayo ilikuwa na malori ya
kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi. Ilikuwa ni kampuni kubwa iliyokuwa
imeajiri wafanyakazi wengi mno.
************************
Mahusiano
ya kimapenzi kati ya kaka James na mwanadada Neila yalizidi kupamba moto. Hapo
awali mimi nilikuwa sijui chochote kuhusu uhusiano huo kwani alikuwa
hajanitambulisha.
Ilifikia
kipindi akanitambulisha rasmi na kuniambia Neila ndiye alikuwa tashtiti wake,
nyonga mkalia ini kama wasemavyo watu waliobobea kwenye mahaba.
Sikuwa
na pingamizi juu ya uhusiano wao ila niliwasisitiza tu watangulize uaminifu
mbele pamoja na upendo wa dhati kwa ujumla.
Mapenzi
yao yaliendelea kukolea kila siku iliyoenda kwa Mungu. Hapo ndipo Naila alianza
katabia ka kudai makuu ikiwemo kukabidhiwa nyumba kununuliwa gari zuri la
kifahari pamoja na kufunguliwa akaunti yenye hale nyingi.
Hayo yote hayakuwa
tatizo kwa kaka James maana pesa ilikuwa chekwa. Kila alichotaka mtoto wa watu
alitimiziwa, mpaka nikaanza kumuonea wivu kwani alizidi mno kumpiga ‘kibomu’
kaka yangu. Naye James kwa kutaka kumkoleza mwanadada huyo hakuona ajabu
kuvitoa vimilioni kwa ajili yake.
Siku
chache baada ya kaka James kumkamilishia mambo hayo; mwanamke huyo alibadilika
ghafla na kuanza kufanya vimbwanga vilivyokuwa vikileta kichefuchefu mbele ya
James.
Tabia
ya mwanamke huyo ilizidi kuwa mbaya, akawa anamletea kiburi kaka yangu huku
akimpa masharti mengimengi ikiwa ni pamoja na kuwa anatoa taarifa akitaka
kwenda kwake.
Siku
moja kaka James alienda kwa mwanamke huyo bila taarifa. Alichokikuta huko
hakuamini kwa macho yake kwani alikikuta kidume kimejilaza kitandani kikiwa na
mwanamke huyo huku wakiwa kwenye pozi la kimahaba.
Ghadhabu
zilimjaa sana kaka James baada ya kuyashuhudia yale mambo.
“Nini hicho unafanya mpenzi wangu?” Alisikika
James kwa sauti ya kitetemeshi akionyesha ni jinsi gani hasira ilivyokuwa
imepanda.
“Nani mpenzi wako?” Aliuliza mwanamke huyo kwa
jeuri na nyodo za kila aina.
Kauli hiyo ilizidi
kuipandisha hasira ya James. Hapo ndiyo alipojua ya kwamba mwanamke huyo ni
nyoka ndumilakuwili mwenye sumu kali.
“Sikia nikwambie
James; kama kusoma hujui basi jaribu hata kuangalia picha! Wewe ni zilipendwa
ndugu yangu, tangu lini mavi ya kale yakanuka?. Mwanaume mwenyewe upo
kianalojia utarandana vipi na mimi nipo kidigitali zaidi? Sasa nakutangazia
rasmi leo kuwa sikupendi na sikuhitaji, na huyu unayemuona hapa ndiye mwanaume
ninayempenda kwa dhati ambaye anastahili kuniona. Upo hapo? Hii ndiyo habari ya
mjini babu wee!” Alizidi kutamba mwanamke huyo kisha akamalizia kicheko cha
kishambenga,
“Heheheeeyah!”
“Kefle! Unajifanya
mjanja na kuniona bwege mimi, sasa anza kusali sala zako za mwisho kwani uhai
wako naukatisha sasa hivi?” Alidakia James kwa sauti ya juu iliyowashitua Neila
na jamaa yake aliyekuwemo humo ndani.
Siyo sauti ya juu
pekee iliyowafanya waduwae bali ni pamoja kitu alichokuwa amekishika mkononi.
Kitu hicho hakikuwa kingine bali ni kidubwasha mithili ya kipaja cha kuku
kilichoundwa kwa madini shaba. Alikuwa ameshika bastola.
Mwanamke yule alianza
kutetemeka na kuanza kuomba msamaha kwa James, kwa bahati mbaya alikuwa
amechelewa! Bila ya huruma James alikitekenya kitufe cha kufyatulia risasi
kisha akamtwanga mwanamke huyo ya kichwa.
Huku akiwa anatweta
kwa hasira aliisukuma risasi nyingine ambayo ilimpata yule jamaa aliyekuwa
akijaribu kulamba asali kwenye mzinga wa James.
Risasi hiyo nayo
ilimpata barabara kijana huyo, ikapenya kupitia kwenye paji lake la uso na
kumfanya naye aanguke chini. Hakuchukua muda akawa amerudisha jezi ya kuendelea
kuishi kwa mwenyezi Mungu, ikawa ni kwa heri mwalimu!
Mpaka hapo dhambi ya
mauaji ya watu wawili kwa mpigo ilianza kumtafuna kaka James. Hofu na woga
vilitanda katika moyo wake, akaanza kuona kesi ya mauaji ya watu wawili ilikuwa
inamkabili.
Baada ya kuwaza
kidogo alikumbuka kuwa bastola yake ilikuwa imebakiza risasi moja ndani. Ndipo
alipoamua kujimaliza na yeye kwa kujipiga risasi.
ITAENDELEA....
No comments:
Post a Comment