ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Haya bwana wewe wasema, mimi
nitapeleka taarifa kama ulivyotaka.” Alimalizia mjumbe huyo na kuondoka zake.
SASA ENDELEA.......
Siku
ayami zilipita, ukakaribia kuisha mwezi bila kupata taarifa zozote za kuendelea
kwa kesi yangu kutoka mahakamani. Kadri siku zilivyozidi kwenda nilizidi
kuingiwa na ujasiri wa kuja kukabiliana na mwanamke huyo siku tutakayokuwa
kizimbani. Tena nikawa na shauku kubwa ya kumbana na kumhoji maswali,
ukizingatia kauzoefu kakuhoji maswali nilikuwa nimeshaanza kukapatapata.
Nilijikuta
napania kumkaba maswali ya kufa mtu mwanadada yule. Japokuwa nilijua fika kuwa
uwezekano wa kuwa bubu kama ilivyokuwa kwa wakili Mlyanyama ulikuwepo. Lakini
sikujali kutokana na kuchoka na vimbwanga vya mwanamke huyo.
Nikiwa
mahabusu nilizidi kujipanga kwa maswali ya kwenda kumkabili huku pointi zangu
nikizipangilia kiuanasheria. Nikawa nimeandaa maswali mithili ya gwiji la
mawakili.
Siku
moja nikiwa sina hili wala lile nilipewa taarifa kuwa kesi yangu ingesikilizwa
tena wiki moja mbele. Niliingojea kwa hamu siku hiyo huku nikiamini kuja
kuushangaza umati wa watu wote watakaohudhuria siku hiyo mahakamani kwa kuuliza
maswali yenye mantiki na yaliyosimama kisheria.
Wiki
moja haikukawia, nilitinga ndani ya kizimba cha mshtakiwa huku upande wa
mashtaka ukimpandisha mwanadada Sharifa kuendelea kutoa ushahidi.
“Kwa vile shahidi alitoa maelezo siku
tuliyomalizia kusikiliza kesi hii, sasa upande wa utetezi utaendelea kumuuliza
maswali.” Ilikuwa ni sauti ya jaji.
Bila
kuchelewa wala kuzubaa nikakohoa kidogo kuisafisha sauti yangu, na baada ya
hapo nikamfakamia kwa maswali shahidi huyo.
“Ulisema jina lako unaitwa nani vile?”
“Sharifa.”
“Sharifa unaweza
ukaeleza mbele ya mahakama ulikuwa na uhusiano gani na Kishoka?”
“Ni ndugu yangu.”
“Ndugu yako kivipi?”
“Kaka yangu!”
“Kabla ya hii kesi
mimi ulikuwa unanifahamu?”
“Ndiyo!”
“Ulikuwa unanifahamu ki vipi?”
“Nilikuwa nakufahamu kama mmiliki wa nyumba
alipokuwa amepanga kaka yangu.”
“Siku ya tukio
ilikuwa ni mara yako ya ngapi kufika hapo kwangu?”
“Ilikuwa ni mara ya kwanza?”
“Sasa mimi ulinijulia wapi wakati ilikuwa ni
mara yako ya kwanza kuja kwangu?”
“Nilikujulia mitaani.”
“Wakati unaniona
mitaani nilikuwa na nani?”
“Ulikuwa peke yako?”
“Sasa ukajuaje kuwa mimi ni mwenye nyumba wa
pale anapoishi kaka yako?”
“Nilijua tu!”
“Sharifa, nikikuambia
kuwa wewe unajaribu kutunga uongo uwe ukweli nitakuwa nadanganya?”
“Ndiyo utakuwa unadanganya.”
“Ngoja nikwambie kitu, mimi Kishoka nilikuwa
namjua kuliko mtu mwingie hapa, siri zake zote alikuwa akiniambia, na kati ya
siri alizoniambia ni kwamba hana ndugu hata mmoja katika nchi, sasa wewe unadai
kuwa ni ndugu yake kutoka wapi?”
“Labda alikudanganya, lakini mimi ni ndugu
yake.” Alijibu Sharifa.
“Wewe
unajishughulisha na nini?”
“Mimi ni fundi cherehani!”
“Siyo mpiga picha?”
“Siyo!”
“Siyo mwandishi wa habari?”
“Siyo!”
“Na wala siyo mtalii?”
“Nimekwambia mimi ni fundi cherehani?”
Alitamka Sharifa kwa ukali.
“Usiwe mkali Sharifa.
Sasa ilikuwaje siku hiyo utembee na kamera? Au ulikuwa unajua kwamba ukifika
kwa Kishoka utakuta tukio kama hilo upige picha za ushahidi?”
“Mimi huwa na kawaida ya kutembea na kamera
ili kuchukua matukio muhimu pale inapobidi.”
“Tulipoonana
na wewe kule ufukweni siku moja kabla ya tukio la kuuawa kwa Kishoka ulikuwa na
kamera?”
“Sijawahi kuonana na wewe ufukweni?”
“Kwa nini kesho yake asubuhi ulikuwa
unatusumbua na Kishoka ukigonga geti na kupotea kimiujiza?”
“Sikuwa mimi?”
“Alikuwa nani?”
“Mimi sijui.”
ITAENDELEA.......
No comments:
Post a Comment