ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Kuzaliwa
kwa kaka James ndiyo kulikuwa hivyo. Wakati huo mimi nilikuwa bado sijafikiriwa
hata kuiona hii dunia. Nilikuwa bado nipo mbinguni nikicheza na kufurahia tu na
malaika.
SASA ENDELEA.......
Baada ya kujifungua
mama yangu hakupata tena nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kwani huo
mfumo umekuja miaka ya hivi karibuni. Zamani ukinasa huku bado unasoma basi
hiyo ndiyo nitolee tena.
Haikuwa kama siku
hizi ambapo msichana akipata mimba yungali anasoma anaruhusiwa kwenda kuilea
mimba kisha akishajifungua anaendelea na masomo. Miaka ile haikuwa hivyo.
Hata hivyo mama yangu
alikuja kujiunga na ualimu wa UPE enzi zile rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano
wa Tanzania hayati Mwl. Julias Kambarage Nyerere alipotangaza elimu ya UPE.
Kwa wale wenzangu na
mimi ambao wamezaliwa juzijuzi kuelekea
kwenye mfumo wa digitali, maana ya UPE ni mpango ulioanzishwa na aliyekuwa rais
wa kipindi hicho hayati Baba wa taifa Mwl. Nyerere ambao ulitaka kila mtoto wa
kitanzania asome elimu ya shule ya msingi.
Hapo ndipo ulipotokea
upungufu mkubwa wa walimu wa shule za msingi kiasi kwamba walimu waliokuwa
wametoka vyuoni wakawa hawakidhi mahitaji.
Ndipo serikali
ilipotangaza nafasi za ualimu hata kwa wale waliokuwa wameishia njiani na
kushindwa kumaliza kidato cha nne pamoja na wale waliokuwa wamemaliza darasa ya
saba nao walichukuliwa na kupewa jukumu ya kuwa walimu.
Kati ya hao walimu wa
UPE na mama yangu naye alibahatika kuwamo. Akawa amepangiwa shule ya
kufundisha.
Ilipita miaka kadhaa.
Huku akiwa mwalimu alipata mume na kumuoa. Ndipo nilipozaliwa mimi.
Wakati huo kaka James
alikuwa akiishi na wazazi wake na mama, yaani namaanisha kwa bibi na babu.
Mpaka walipokuja kufariki ndipo alipochukuliwa na mama na kukaa pamoja katika
familia moja.
Baba yangu
alimchukulia kaka James kama alivyokuwa akinichukulia mimi, yaani alimlea kama
mwanae wa kumzaa wakati alikuwa ni baba yake wa kufikia.
Hapakuwa na ukambo
ukambo hapo, baba yangu alikuwa kapenda boga pamoja na maua yake. Alikuwa
tofauti kabisa na baadhi ya wanaume ama wanawake wengine wanaowachukia watoto
wa kambo.
Kama zawadi
alituletea wote bila ya upendeleo, kama adhabu alitoa bila ya kupendelea, kama
ni mapenzi basi alitupatia mapenzi mema wote wawili.
Kaka James hakuwahi
kuwa na upweke kwa kulelewa na baba wa kambo. Alikuwa akithaminiwa kama
kawaida, hakika maisha yake yalikuwa ni ya furaha siku zote.
Nadhani upendo
tuliokuwa tukiupata kutoka kwa baba na mama ndiyo ulioimarisha uhusiano wetu na
udugu wetu uliokuwa wa kushibana kama vile mapacha.
Hata hivyo furaha
yetu ilikuja kubadilika na kuwa majonzi pale wazazi wetu walipokuja kupata
ajari mbaya ya gari na kupoteza maisha papo hapo. Vifo vya wazazi wetu kwa
mkupuo vilichimba donda kumbwa mno moyoni mwangu.
Usiombe ndugu msomaji
kuwapoteza wazazi wako kwa wakati mmoja, maumivu yake ni zaidi ya msumari wa
moto ukandamizwapo kwenye kidonda kinachoelekea kupona.
Tukio hilo huwa
sipendi hata kulielezea kwani huwa linaibua machungu makubwa mno ndani ya moyo
wangu. Yaani wee acha tu. Kama ukitaka nianze kububujikwa na machozi basi
nikumbushie tukio hilo tu, aisee! Bora niachane na hizo habari kwani zitanifanya
nishindwe hata kuendelea kukuhadithia yanayohusu mirathi ya kaka.
Wakati wazazi wetu
wanatutoka mimi nilikuwa nipo darasa la tatu na kaka James alikuwa ndiyo
kahitimu kidato cha nne.
Mara baada tu ya
wazazi wetu kufariki kaka James alitaka tugawane mali tulizokuwa tumeachiwa.
Kwa kuwa mimi nilikuwa mdogo sana, sikuwa na la kuamua wala kushauri zaidi ya
kuwa kama bendera nikifata maamuzi ya kaka yangu.
Tuligawana mali zote
huku nyumba akiniachia mimi. Hata hivyo tuliendelea kuishi hapo wote licha ya
nyumba kuwa mikononi mwangu. Baadhi ya mali
nilizokuwa nimegawiwa kutoka kwenye mirathi hiyo tuliziuza ili
zinisaidie katika masomo.
Kaka James yeye
aliuza kila kitu, lakini hakutaka tena kuendelea na shule badala yake alianza
kufanya biashara huku akiwa na mtaji wa kutosha kutokana na kuuza mirathi yake
yote.
Nilifanikiwa kusoma mpaka kidato cha sita huku
kaka yangu yeye akiishia kidato cha nne tu. Lakini mpaka namaliza shule
mwenzangu alikuwa kashakuwa tajiri huku biashara zake zikishamiri vizuri.
Kasi ya kupata
utajiri kwa kaka James ilikuwa kubwa sana mpaka nikaanza kushangaa.
Nilipojaribu kumuuliza kaka James kulikoni naye aliniiambia ni baraka kutoka
kwa Mungu. Hilo ndilo lilikuwa jibu lake pindi nilipomuuliza kuhusu utajiri huo
aliokuwa akiupata kwa kasi.
Mpaka namaliza kidato
cha sita alikuwa ni tajiri wa kuogopeka mji mzima. Alikuwa na magari mawili ya
kifahari na nyumba mbili za kifahari.
ITAENDELEA......
This comment has been removed by the author.
ReplyDeleteNilifanikiwa kusoma mpaka kidato cha sita huku kaka yangu yeye akiishia kidato cha nne tu.NowMing Lakini mpaka namaliza shule mwenzangu alikuwa kashakuwa tajiri huku biashara zake zikishamiri vizuri.
ReplyDelete