ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Sajenti
Bakari Mlongo alionekana kuwa na kigugumizi hatimaye akaganda mithili ya cd
kongwe iliyochakaa. Wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama alimwambia hakimu hana
la zaidi la kumuuliza shahidi huyo.
SASA ENDELEA.......
Hatimaye
shahidi wa pili kutoa ushahidi aliwadia. Shahidi aliyefuatia alikuwa ni Sajenti
Majaliwa Mbogo, askari ambaye yupo katika kitengo cha kupima alama za vidole
ambaye pia alikuwa ameambatana na kikosi kilichokuja kwangu siku ya tukio.
Sajenti
Mbogo baada ya kuapishwa alikumbushwa saa na siku ya tukio na mwendesha mashtaka
bwana Charles Ngonyani.
Sajenti
Mbogo alieleza kuwa siku hiyo alikuwa kwenye kituo chake cha kazi kama ilivyo
ada. Ndipo alipopata wito kutoka kwa mkuu wa kituo hicho na kuambiwa kuna
mauaji yametokea kwenye nyumba yangu.
“Tueleze ilikuwaje baada ya kuambiwa hivyo na
mkuu wako wa kituo.”
“Agizo lililokuwa limetolewa pale ni kwenda
kunako eneo la tukio, na ndicho kilichofuata.”
“Mlipofika eneo la tukio mlikuta nini?”
Mwendesha mashitaka aliendelea kuuliza maswali ya kuweza kumuongoza shahidi
huyo aendelee kutoa ushahidi.
Maelezo
ya Sajenti Mbogo hayakutofautiana sana na yale ya shahidi aliyekuwa
ametangulia. Mwisho shahidi huyo alieleza jinsi matokeo ya vipimo vya alama za
vidole yalivyonihusisha kuwa nilimuua Kishoka.
Hatimaye
mwendesha mashitaka alimaliza kutoa muongozo kwa shahidi huyo kisha akamwambia
mheshimiwa Jaji kuwa amemaliza na akaenda kuketi.
Wakili
wangu aliinuka tena na kusogea kwenye kizimba ambacho shahidi huyo alikuwa
amesimama. Alipofika akaanza kumuuliza maswali kama ilivyoada.
“Natumaini wewe upo
kwenye kitengo cha kupiga picha na kupima alama za vidole kwa muda mrefu katika
jeshi la polisi?”
“ Ndiyo.”
“Kama mimi nikishika kitu kisha mkaja kupima
alama zangu za vidole si zitaonekana?”
“Ndiyo.”
“Nikiiambia mahakama
kwamba mteja wangu alishika mwili wa marehemu pamoja na kisu baada ya kukuta
tukio limeshatokea chumbani kwake kwa kutokujua madhara yake ama kutokana na
kuchanganyikiwa unaweza ukakubaliana na mimi?”
“Hapana sitakubaliana na wewe.”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu hatukuona alama za vidole vya mtu
mwingine zaidi.”
“Mimi nitaiambia mahakama tukufu kwamba mteja
wangu alishika sehemu hiyo hiyo aliyokuwa ameshika muuaji na ndiyo maana
hazikuonekana alama za mtu mwingine.?”
“Haiwezekani, siyo rahisi kumshika mtu mpaka
kumuua usimguse sehemu kubwa ya mwili. Ingekuwa mtuhumiwa aliyepo kizimbani
hajafanya hilo tukio basi alama za vidole za mtu wa kwanza zingetapakaa mwili
mzima wa marehemu.”
“Je, mtu kama kavaa ‘groves’ mikononi alama
zake huonekana akishika sehemu?”
“Hapana.”
“Basi muuaji alikuwa kavaa groves wakati anaua
na ndo maana alama za vidole hazikuonekana!”
“Hapana, muuaji ni yule pale kizimbani maana
ndiyo tulimkuta eneo la tukio.”
“Shahidi aliyekutangulia amesema kwamba mtu
aliyetoa taarifa za awali juu ya kifo cha kishoka hakujitokeza hata kidogo
zaidi ya kupiga simu tu kituoni, unaweza kuniambia kwa nini hakutaka
kujitokeza?”
“Kwa kweli siwezi kujua.”
“Nikikwambia kuwa hajajitokeza kwa kuwa alikuwa
ni mharifu na huenda aliogopa kuja kuumbuka utakubaliana na mimi?”
“Hapo siwezi kusema chochote kwa sababu sijui
sababu zilizomfanya asijitokeze kituoni.”
“Basi huyo akipatikana na kufanyia mahojiano
kikamilifu huenda akawa na maelezo ya kutosha kuwasaidia katika upelelezi wa
kesi hii na huenda mtambaini muuaji halali wa Kishoka na siyo mteja wangu.”
Aliunguruma bwana Mlyanyama.
Mpaka
hapo Sajenti Majaliwa Mbogo hakuwa na la kuongea. Wakili wangu alimtazama jaji
na kumwambia kamaliza maswali ya kumuuliza shahidi huyo. Baada ya kusema hivyo
akaenda kuketi.
Jaji
aliiahirisha kesi na kutaja tarehe nyingine ambayo ingeendelea kusikilizwa.
Nilitolewa kizimbani na kupelekwa kwenye karandinga la magereza tayari kabisa
kwa kurudishwa mahabusu.
JE, KESI HII ITAISHAJE? USIKOSE
TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment