ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Gari lililokuwa limenichukua
liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani
**************************
SASA ENDELEA.......
Maisha ya jela ndiyo
niliyoanza kuishi kwa wakati huo. Niligundua tofauti kubwa sana kati ya jela na
mahabusu. Ukiwa mahabusu husumbuliwi kufanya kazi ama adhabu yoyote kwani
unakuwa bado ni mtuhumiwa tu.
Lakini ukiwa jela
unatakiwa kufanya kazi za hapa na pale zikiwa ni adhabu kwani tayari utakuwa
umeshahukumiwa. Na ndiyo maana watu wengine husema jela kuna mateso.
Yote hayo ni tisa,
kumi mkienda kulala, heheeeh! Kama utalemaa mithili ya kalio la kushoto basi
unaweza ukawa mke wa wanaume wenzio. Huko ndiyo kuna watu waliopinda, watu
wasiokuwa na dira na maisha.
Jela ni ubabe ubabe
tu, unyama na mikwara ndiyo hutawala hasa kwa mtu mgeni gerezani humo. Hata
hivyo kwa upande wangu hayo yote hayakutokea licha ya kuwa na muonekano wa
upole.
Kilichonisaidia
kutoionja adha ya ugeni wa jela ni kitu kimoja. Kuna jamaa mmoja nilimkuta humo
gerezani ambaye tulikuwa tukifahamiana na kuheshimiana sana. Huyo mtu ndiyo
alionekana kuwa msaada mkubwa sana kwangu kwani alikuwa kakaa humo kwa muda wa
miaka miwili hivyo mikikimikiki ya huko alikuwa kashaizoiea.
Mbali na kuizoea
mikiki mikiki ya humo; jamaa huyo alikuwa kashateuliwa kuwa mnyapara wa gereza.
Mnyapara wa gerezani ni yule mfungwa anayewaongoza wafungwa wezake gerezani
humo.
Jamaa huyo hakuwa mwingine
bali ni Mack. Uhusiano wetu haukuanza siku hiyo ama siku za karibuni, ulianza
miaka mingi iliyokuwa imepita. Tulikuwa tunafahamiana toka kitambo na tulikuwa
tumeshafanya mambo mengi.
Baada ya kifo cha
marehemu kaka James; mali zake zote nilizirithi mimi kwani ndiyo nilikuwa ndugu
yake wa pekee. Ikumbukwe kuwa mimi na marehemu James tulizaliwa tumbo moja ila
baba zetu ni tofauti.
Yeye ndiye alikuwa
kifungua mimba katika tumbo la mama yetu. Mama yetu alipata ujauzito kwa bahati
mbaya wakati anasoma elimu ya sekondari.
Baada ya kupewa
ujauzito alilazimika kukatisha masomo ili aulee huo ujauzito hivyo akashindwa
kuendelea na elimu na kujikuta akiishia kidato cha tatu.
Jamaa aliyekuwa
amempa ujauzito alikimbia na kupotelea pasipojulikana kwa kuogopa kushtakiwa na
wazazi wa mama yetu kwa kumrubuni na kumkatisha masomo mtoto wao.
Si wazazi peke yao
waliokuwa wakila sahani moja na wanaume waliobainika kuwapa mimba watoto wao,
hata serikali ilikuwa ipo mstari wa mbele kuhakikisha wanafikishwa mbele ya
sheria.
Tangu siku hiyo jamaa
huyo alipotea kabisa na hakuonekana tena kama walivyopotea wadudu aina ya
nzige. Nadhani waliozaliwa siku za nyuma kidogo wanakumbuka miaka ile ya
uvamizi wa nzige katika mashamba ya wakulima.
Nzige ni wadudu
hatari sana ambao hutembea katika kundi kubwa na wakivamia shambani mwako basi
wanakula mimea yote iliyomo shambani humo. Usiombe shamba lako livamiwe na
wadudu kama hao kwani wanakula hadi mashina ya mimea ya shamba wanalolivamia.
Sasa mwanaume
aliyekuwa amempa ujauzito mama yetu na kumsababisha kukatisha masomo alipotea
mithili ya wadudu hao.
Hakuonekana kabisa
wala hazikusikika fununu zake hata kidogo. Kutokana na hiyo hali; mpaka wa leo
haijulikani kama jamaa huyo bado yungali hai ama kashakumbwa na mauti.
Mama aliiingia katika
wakati mgumu sana baada ya kubebeshwa huo ujauzito. Kilichokuwa kinamfanya
apate tumbo joto ni jinsi baba yake alivyokuwa mkali na katili kupindukia,
yaani marehemu babu.
Babu yangu huyo
alikuwa ni mkali kama simba. Sijui kutokana na ujeshi wake aliokuwa nao, maana
alikuwa mbogo kupita maelezo. Alikuwa hataki kabisa ‘Ujinga jazz bend’ katika
familia yake.
Sasa ujauzito huo
ulimfanya mama yangu azidi kuchanganyikiwa, kibaya zaidi hata aliyekuwa amempa
huo ujauzito alikuwa kashakimbia na kutokusikika hata zile fununu zake.
Alichoamua ni
kutoroka na kuenda asikokujua kwani aliona hata akienda kwa ndugu wengine baba
yake angempata, na hapo ndiyo angelionja joto la jiwe.
Hakutaka kujiua wala
kuitoa hiyo mimba kwani alikuwa akiijua vyema dhambi iliyopo kwa binadamu
anayejiua ama anayeua. Hayo yote alikuwa ameyaweka akilini tangu utotoni
alipokuwa akipewa mafundisho ya dini.
Mama yangu alilelewa
katika maadili ya kidini sana japokuwa alikuja kuanguka dhambini na kurubuniwa
na kamjamaa kalikokuja kumpa ujauzito.
Huku ujauzito
aliokuwa nao ukiwa na miezi mitatu, mama aliamua kutorokea katika mji jirani
ili kujiepusha na hasira za baba yake. Kwa mtazamo wake alihisi suluhu ya hiyo
kashfa ni kulala mbele.
Alfajiri na mapema
alitoka nyumbani kama anaenda shule akiwa na sare zake za shule huku nguo
zingine akiwa ameziweka kwenye mfuko wake wa kubebea vitabu vya shule.
Kwa vile ilikuwa bado
asubuhi sana, hakuna mtu yeyote
aliyemuona kwa pale nyumbani wakati anatoka. Alitembea mpaka kwenye
stendi ya mabasi, akakata tiketi ya basi lililokuwa linaondoka muda si mrefu.
Wakati huo alikuwa
tayari kashazivua sare za shule na kuvaa nguo zake za nyumbani alizokuwa
ameziweka kwenye mfuko wa kubebea vitabu vyake vya shule.
Baada ya robo saa
alikuwa tayari kajikausha kunako viti vya basi hilo huku likichanja mbuga kwa
mwendo wa kasi.
Mambo yaligeuka kuwa
si mambo mara baada ya basi hilo kuupa mgongo mji huo. Liligongana uso kwa uso
na lori la mafuta na kusababisha ajari mbaya sana.
Basi hilo lilipiga
mweleka na kubingirika mpaka mara tatu, likawa nyang’anyang’a kutokana na ajari
hiyo.
Ilikuwa ni ajari
mbaya sana na ya kutisha ambapo watu kumi na sita walipoteza maisha papo hapo,
watu ishirini walikuwa ni mahututi na watu kumi na tano wakijeruhiwa ila siyo
sana. Kati ya wale mahututi na mama yangu naye alikuwa ni mmoja wao.
Haukupita muda sana
magari ya kubeba wangonjwa (ambulance) yakawa pale kubeba wahanga wa ajari hiyo
pamoja na maiti na kuwapeleka katika hospitali ya jeshi iliyokuwa karibu kabisa
na sehemu ilipokuwa imetokea ajari hiyo.
Mpaka anafikishwa
hospitali mama yangu alikuwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa kaumia vibaya sana
************************
ITAENDELEA.....!
No comments:
Post a Comment