ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Waliniamru
nipande nami nikajitoma bila ya ubishi. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza.
Gari lilitoka mbio utadhani lipo katika mashindano, tulitumia takribani dakika
kumi kufika mahakamani.
SASA ENDELEA.......
Tulipofika
mahakamani tuliwakuta watu kibao, baadhi yao niliwatambua, walikuwa ni wakazi
wa mtaani kwetu. Nilianza kuhisi kuwa taarifa za kesi yangu zilikuwa zimetapakaa sana huko mtaani.
Kamera
za mapaparazi nazo zilizidi kunisonga wakati naingia mahakamani. Nilijaribu
kujifunika usoni ili nisipigwe picha lakini haikusaidia chochote. Nilipelekwa
mpaka sehemu ya kukaa watuhumiwa wakati wanasubiri kupandishwa kizimbani.
Mara
ilisikika sauti... ‘koooort!’, sauti hiyo iliashiria kufunguliwa kwa mahakama.
Watu wote walisimama ili kutoa heshima katika mahakama kama ilivovyo ada, muda
mfupi waliketi na kesi zikaanza kusikilizwa.
Kesi
yangu ndiyo ilikuwa ya kwanza kutajwa. Nilipandishwa kwenye kizimba kisha
nikaulizwa dini yangu. Nilipotaja dini yangu nikapewa kitabu kitakatifu cha
dini husika na kuanza kuapishwa.
Baada
ya kuapishwa nilisomewa shitaka langu na kuambiwa sitakiwi kujibu chochote
kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kuendesha kesi ya mauaji. Baada ya
hapo nilitolewa kizimbani na kurudishwa rumande nikasubiri jalada la kesi yangu
lipelekwe mahakama kuu. Lakini rumande niliyopelekwa kwa mara hii haikuwa ile
ya kule kituoni bali ni rumande ya magereza.
Nilikaa
mahabusu katika rumande hiyo kwa siku kadhaa nikisubiri tarehe ya kutajwa kwa
kesi yangu kwa mara ya pili ambayo ilitakiwa kuhamishiwa mahakama kuu, mahakama
ambayo huwa na uwezo wa kuendesha kesi za mauaji.
Kawaida
ya sheria za nchi yetu ni kwamba, mshtakiwa yeyote wa kesi ya mauaji hutafutiwa
wakili na serikali kama hana uwezo wa kumlipa wakili. Wakili huyo humsaidia
kusimamia kesi yake mpaka mwisho.
Hicho
ndicho kilichotokea kwenye kesi yangu hiyo. Nilitafutiwa wakili ambaye alikuwa
ni wakili kutoka kwenye taasisi moja inayosimamia haki za binadamu.
Nikiwa
nasota kwenye rumande ya magereza nilipokuwa nimepelekwa baada ya kutoka mahakamani,
wakili alinifuata na kuanza kujadiliana nami jinsi ya kunisaidia katika
kunitetea kwenye kesi iliyokuwa ikinikabili.
“Hebu
nieleze ukweli wako wote ili nijue ni jinsi gani nitakusaidia.” Alisikika
wakili Jonas Mlyanyama kwa sauti iliyokuwa imejaa upole na yenye kubembeleza.
“Kusema kweli sikuhusika kabisa na kifo cha
Kishoka.”
“Ilikuwaje, hebu niambia A mpaka Z bila
kuficha kitu chochote.”
Nilianza
kumweleza tukio zima lilivyokuwa. Nikamweleza jinsi msichana wa kule ufukweni
nilivyokutana naye na kuweka miadi ya kunitembelea kesho yake nyumbani kwangu.
Sikuishia
hapo, niliendelea kusimulia jinsi mauzauza yalivyoanza kujitokeza kwa mwanadada
huyo pale alipokuja nyumbani na kukatalia getini baada ya kwenda kuambiwa na
Kishoka apite ndani. Hata Kishoka alipokuja kuniambia kuwa mgeni huyo kakataa
kuingia ndani bali ananitaka niende kulekule getini, nilienda lakini sikumkuta.
Niliendelea
kumhadithia kizaazaa hicho wakili Jonas Mlyanyama huku akiwa kanisikiliza kwa
makini kabisa. Hatimaye nilimaliza maelezo yangu kwa kueleza jinsi nilivyoikuta
maiti ya Kishoka ikiwa imelazwa juu ya kitanda changu.
“Nimeambiwa
kwamba alama za vidole vyako zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye
kisu kilichotumika kumuua marehemu, ulikigusa kisu au ile maiti?”
“Hapana wakili sikugusa chochote hapo, na
ndiyo maana nakuambia kwamba kesi hii ipo kimazingara. Hata mimi nashangaa
kuonekana alama za vidole vyangu.”
Wakili
Jonas Mlyanyama alivuta pumzi kisha akazishusha. Wakati natoa maelezo wakili
huyo alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo yangu kwenye kitabu alichokuwa amekuja
nacho.
Pamoja
na kuwa ‘busy’ wakili huyo alionekana kuwa makini sana kunisikiliza kila
nilichokuwa nakinena. Pia hakuacha kuhoji maswali pale ilipolazimu. Alikuwa na
maswali mengi utadhani mgambo wa kata.
Alinipa
moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa
nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.
JE, WAKILI JONAS MLYANYAMA
ATAFANIKIWA KUMTETEA BRIGHTON KATIKA KESI YA MAUAJI YA KISHOKA? USIKOSE TOLEO
LIJALO!
No comments:
Post a Comment