ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
‘Wamewasha hadi taa utadhani ni chumbani kwao, hizi sasa
ni dharau. Kwa nini asimpeleke chumbani kwake?’ Nilizidi kujisemea kimoyomoyo.
SASA ENDELEA.......
‘Lakini
Kishoka huwa hana kawaida ya kuingia chumbani kwangu kama sipo, na hata kama
angekuwa na kawaida hiyo asingefanya hivyo kwani alikuwa kanipigia simu muda si
mrefu kunijuza kuwa kuna mgeni wangu ananisubiri nami nikamwambia nipo njiani.’
Nilizidi kuwaza huku masikio yakiwa makini kusikilizia chumbani kama kuna
mihemo ama miguno ya watu wakifanya matusi.
Lakini suala la
Kishoka kusahau kuufunga mlango wangu ama kuacha kwa makusudi lilikuwa
haliniingii akilini hata kidogo kwani alikuwa ni mtu mwaminifu sana. Sasa
aliingiwa na ibilisi gani mpaka akaamua kutofunga mlango wangu. Na kama alikuwa
kafunga aliingiaje wakati funguo nilikuwa nazo na nilikuwa sina kawaida ya
kuziacha? Funguo nilikuwa natembea nazo utadhani pete ya ndoa kwa mwanandoa
mwaminifu!
Nilizidi kujiuliza
maswali teletele huku nikiusogelea mlango. Nilipousukuma mlango nilizidi
kuchanyikiwa baada ya kukiona kisu kilichokuwa kimetapakaa damu kikiambaa ambaa
pale mlangoni kunako tambala la kufutia miguu.
Nililazimika kuingia
kwa tahadhari kubwa wakati chumba kilikuwa ni changu, chumba ambacho nilikuwa
nimeshakizoea kiasi kwamba hata liwemo giza totoro lakini swichi ya taa
sitashindwa kuiwasha. Siku hiyo nilijikuta nikinyata wakati taa ilikuwa
inawaka!
Kwa
mwendo wa kunyata niliuvusha mguu wangu wa kwanza pale mlangoni huku ukifuatiwa
na mguu wa pili. Nilijaribu kuangaza mbele usawa wa mlango lakini sikuona
chochote kigeni zaidi ya kabati langu la nguo na meza ya kujipodolea yenye kioo kikubwa cha kuweza
ujiona nusu mwili; yaani kuanzia kiunoni kwenda juu.
Wakati
huo nilikuwa sijaangalia upande wa kulia wa chumba changu, upande ambao kitanda
changu cha sita kwa sita kilipokuwa, si unajua tena mambo ya mila na desturi
kitanda sharti kiwe pembeni!
Niligeuka mzima mzima
huku nikitupia jicho langu pale kitandani. Jicho lilipotua kitandani nilijikuta
nikibaki mdomo wazi huku nikikodoa macho bila ya kupepesa.
Lahaula!
Mambo yaliyokuwa yametendeka juu ya kitanda changu ni vioja, nilishindwa
kuelewa ni nani aliyefanya unyama huo usiokuwa na breki hata kidogo. Nguvu zilianza
kuniishia, nikabaki nimeduwaa huku nisijue la kufanya. Sikutegemea kabisa
kukuta tukio la kutisha na la umafia namna ile likiwa limetendeka kwangu, tena
juu ya kitanda changu.
Tukio
jenyewe lilikuwa ni la mauaji ya kutisha, kichwa cha Kishoka kilikuwa
kimetenganishwa na kiwiliwili chake. Kisu kilichokuwa mlangoni kikiwa kimetapakaa
damu nadhani ndicho kilichotumika kumchinja mpangaji wangu, yaani Kishoka.
‘Chinjachinja ni nani
sasa kama siyo yule mgeni wangu? Na kama ndiyo yeye, kajificha wapi sasa wakati
sijamuona akitoka?’ Nilizidi kuchoka.
‘Kumbe msichana huyo ni hatari! Sioni mtu
mwingine wa kufanya kitendo kama hiki zaidi yake, atakuwa ni huyohuyo!’ Nilizidi
kunena kimoyomoyo huku nikiisogelea maiti ya Kishoka, maiti ambayo ilikuwa
haitamaniki kutokana na kutenganishwa
kikatili, kichwa na kiwiliwili havikuwa pamoja tena.
Wakati
nikitafakari hatua ya kuchukua kwa wakati huo, nilishangaa baada ya kuona watu
wawili wanaingia mpaka humo chumbani kwangu utadhani ni kwao vile, wote walikuwa
na jinsia ya kiume. Sijakaa sawa wakanipiga ‘henzapu’ na kuniambia nipo chini
ya ulinzi.
Pumzi
zilianza kuniishia, nikajikuta nikipumua kwa shida huku kifua changu kikianza
kubana. Sijakaa sawa nikaanza kuhisi kama kizunguzungu na kuhisi kama nataka
kuanguka. Mpaka hapo nilipoteza ‘network’ na kujikuta sijitambui hata kidogo.
**********************
SALAAAAALEH! HAPO PATAMU
KWELIKWELI NDUGU MSOMAJI, HEBU FUATILIA TOLEO LIJALO UONE NI NINI KITATOKEA.
No comments:
Post a Comment