Sunday, September 22, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 19



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Nikiwa rumande machozi yalizidi kunitiririka bila kukauka utadhani chemichemi za mto Naili, chemichemi ambazo hutiririka bila kukauka misimu yote; iwe masika ama kiangazi. Mifereji ya machozi ilikuwa inatiririka kutoka machoni ikipitia mashavuni mpaka kwenye kidevu.
SASA ENDELEA.......
Mahojiano hayo yalichukua takribani masaa mawili na nusu, hata hivyo hapakuwa na kipya zaidi ya kurudia kuulizwa maswali niliyokuwa nimeulizwa hata kule hospitali. Pia katika mahohjiano hayo yaliambatana na vitisho lukuki vya kunitaka nikiri kuwa nilimuua Kishoka. Hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo ya kuwa sijaua.
“Wewe ni muuaji ila unajifanya ni mbishi, mbona ripoti ya postimotamu imeonyesha kuwa wewe ndiyo umeua?”
“Hapana afande, mimi sijamuua Kishoka. Maelezo niliyoyatoa ndiyo yana ukweli wote.”
“Mbona kwenye kisu kilichotumika kumuulia marehemu tumeona alama za vidole vyako, vilevile kwenye mwili wa marehemu alama za vidole vyako zipo?”
            Hilo nalo lilikuwa ni neno. Nilishtuka sana kusikia hivyo. Ukweli ni kwamba wakati naingia chumbani kwangu sikujaribu hata kukigusa kisu kilichotumika kumchinja Kishoka. Isitoshe hata mwili wake sikuugusa; sasa jambo la alama zangu za vidole kuonekana kwenye kisu hicho na kwenye mwili wa marehemu lilizidi kunichanganya. Wakati mwingine nilihisi huenda ni mitego tu ya makachero hao ili kumfanya mtu aropoke kama kweli katenda kitendo hicho.
            “Hilo ni jambo geni kwangu, kile kisu sikuwahi hata kukigusa zaidi ya kukitumbulia macho. Hata mwili wa Kishoka sikuwahi kuugusa zaidi ya kuukodolea macho, sasa alama za vidole vyangu zilifikafikaje kwenye kisu na maiti ya Kishoka?”
“Unatuuliza tena sisi! Naona wewe huna jipya ila ni ubishi tu unaokusumbua. Kesho faili lako tunalipeleka mahakamani kwani uchunguzi wetu sisi umeshakamilika.” Alimalizia kuongea askari huyo aliyekuwa amevaa nguo za kiraia kisha akaamuru nirudishwe rumande.
Baada ya mahojiano hayo nilirudishwa tena rumande. Kilichokuwa kinasubiriwa pale ni kufika asubuhi nyingine kisha nipelekwe mahakamani kujibu shauri lililokuwa likinikabili.
 Nilisweka tena ndani na kuanza kuburudika na adha ya humo. Joto la kufa mtu nilikuwa linanisumbua kwa wakati huo. Hamkuwa na mkeka wala busati hivyo nililazimika kujilaza kwenye sakafu.
Ilipofika jioni mbu walicharuka tena. Ikawa tafrani mtindo mmoja, usiombe mbu wa rumande ndugu msomaji, wanauma mpaka kwenye nyayo. Nahivi sikuwa na shuka wala blanketi, heheee, nakwambia nilikoma kuringa.
Asubuhi nyingine ilifika japokuwa kwa shida sana. Mbavu zote zilikuwa zikiniuma kutokana na kulala kwenye sakafu usiku kucha. Mikononi na niguuni vilikuwa vimejitokeza vipele vingi kutokana na kutafunwa na mbu usiku mzima.
Mara mlango wa selo ulifunguliwa kisha nikawaona askari watatu wakinitaka nitoke. Nami bila ubishi nilitoka. Nilipotoka tu hawakunichelewesha, wakanifunga pingu kisha wakanipeleka sehemu ambako kulikuwa na karandinga.  
            Waliniamru nipande nami nikajitoma bila ya ubishi. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza. Gari lilitoka mbio utadhani lipo katika mashindano, tulitumia takribani dakika kumi kufika mahakamani.
HAYA SASA BRIGHTON KASHAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MARA YA KWANZA. JE, KESI YAKE ITAENDAJE?

No comments:

Post a Comment