Sunday, September 8, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 8




                                        SEHEMU YA 8
ILIPOISHIA........
Aliniacha na kwenda zake, nikiwa bado nipo kwenye kitanda changu cha sita kwa sita, niliendelea kuitafakari ndoto ambayo nilikuwa nimeiota muda mfupi uliopita. Maneno ya Anna yenye ujumbe mzito yalizidi kujirudia kichwani mwangu.

SASA ENDELEA.......
            Niliangalia saa yangu ya mkononi, nikaona masaa yanayoyoma, saa kumi na nusu ilikuwa inaelekea. Wazo la kwenda ufukweni kupunga upepo lilinijia, nikaenda kuoga kwanza kabla ya kuanza safari yangu ya kuelekea ufukweni. Baada ya kuoga ‘nilitupia pamba’ za kufa mtu mwilini mwangu; kaputura ya  jinzi na fulana yenye mikono ya kuishia mabegani.
            Nilienda kwenye ‘dressing table’ langu kisha nikajipulizia marashi, nikaanza kwenda nilikokuwa nimekusudia kwenda. Nikiwa njiani nilizidi kuumiza pua za watu waliopita karibu yangu kwani marashi niliyokuwa nimejinyunyiza yalikuwa na harufu kali.
            Huku nikitembea taratibu nilianza kuisikia harufu ya bahari, mara nikaanza kuukanyaga ufukwe. Nikiwa naambaa ambaa kandokando mwa bahari, nilimuona mwanadada amekaa mbele yangu. Nilianza kumfuata ili nikampe ‘hai’, na ikibidi tupigepige soga kubadilishana mawazo.
            Nilipomkaribia akainuka, hapo ndiyo niliweza kuushuhudia uzuri aliojaaliwa na Muumba. Kichwani nywele ndefu, kifuani maziwa yaliyojaa kiasi, kiunoni palikuwa pamekatika kidogo kisha pakafuatiwa na wowowo la wastani.
            Nilizidi kukoshwa na hipsi zake sanjari na mguu wake wa bia. Mwanadada huyo alikuwa kavaa kipedo pamoja na kitopu. Kwa jinsi alivyokuwa ametokelezea nilijikuta nikivutiwa naye kabla hata sijaanza kuongea naye.
            Kabla sijafika alipokuwa nilimuona kajinyosha kisha akaanza kuchapa lapa, bila kujishauri mtu mzima nilijikuta nikiropoka kwa nguvu,
“samahani dada, naomba kuzungumza na wewe kidogo.”
Licha ya kutanguliza neno la kiungwana, yaani samahani, mwanadada huyo hakusimama wala hakugeuka kunitazama.
            Nilianza kumfuata kwa nyuma nyuma, nilipoanza kumfuata nilishangaa kumuona  anaanza kukazana. Nilishindwa kuelewa ni kwa nini alikuwa muoga kiasi hicho, nilimuita tena kwa mara ya pili lakini aliendelea kunichunia.
“Wewe dada, inamaana hujanisika au hujanielewa?” Hilo ndilo swali nililomtwanga huku nikimfuatia kwa nyuma.
            Kwa mara ya kwanza niliisikia sauti yake nyororo, sauti yenye kuweza kumtoa nyoka pangoni ama kumtoa sungura kwenye kichuguu. Sauti yake adimu ni moja ya sauti ambazo huaminika kuvuta mvua mpaka ikanyesha hata kama ni kiangazi.
“Utanisamehe kaka yangu kwa sababu nina haraka kwelikweli, ila usijali, nitakuja kwako kesho asubuhi!” Alinijibu bila ya kugeuka kuniangalia.
JE, MSICHANA HUYO NI NANI? PIA ATAKUBALI KUONGEA NA BRIGHTON? ITAENDELEA........

No comments:

Post a Comment