ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Pumzi
zilizidi kubana, ghafla nilijiona nikianguka mzima mzima huku macho yangu
yakipoteza upeo wa kuona. Kabla sijafika chini niliacha kujitambua na kupoteza
fahamu ghafla.
SASA ENDELEA.......
“Brighton,
unajisikiaje?” Ilikuwa ni sauti ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliyekuwa
kaketi pembeni mwa kitanda nilichokuwa nimelala.
“Mh! Wakili, hapa nipo wapi?” Nilijikuta
nikiuliza swali na siyo kutoa jibu baada ya kumfahamu mtu niliyekuwa naongea
naye.
“Hapa upo kwenye hospitali ya magereza,
ulianguka ghafla leo asubuhi wakati ukiwa kizimbani.” Alinijibu bwana
Mlyanyama.
Baada
ya kuniambia hivyo kumbukumbu zilinijia kwa kinagaubaga. Hapo ndiyo nilikumbuka
tukio zima lilivyokuwa, hata hivyo nikapata shauku kubwa ya kumuuliza wakili
wangu jinsi mambo yalivyokuwa kule mahakamani.
Wakati
mimi ninashauku hiyo, yeye naye alikuwa na shauku ya kujua ni kitu gani
kilinifanya nipoteze fahamu nilipokuwa pale kizimbani. Kila mmoja akawa na hamu
ya kusikia maelezo kutoka kwa mwenzake.
Nilishusha
pumzi ndeefu kisha nikamwambia bwana Mlyanyama,
“hivi nilianguka mpaka chini kabisa?”
“Ndiyo! Kwani ilikuwaje?”
“Kaka, ni mambo ya ajabu niliyoyaona mle
mahakamani!”
“Mambo gani hayo?” Aliniuliza wakili huyo kwa
upole kabisa huku akikaa mkao wa kula kisikia kilichonifanya nianguke na kuzua
gumzo mahakamani hapo.
Ndipo
nilipoamua kumpasulia kile nichokuwa nimekiona mahakamani.
“Yule msichana aliyeinuka kutoa ushahidi ndiyo
muuaji kaka.” Nilimwambia wakili wangu kwa sauti ya kunong’ona.
“Muuaji ki vipi?” Naye alihoji kwani somo
lilikuwa bado halijamwingia akilini.
“Yule ndiyo msichana mwenye mauzauza
niliyekusimulia.”
“Yule uliyeonana naye ufukweni kisha kesho
yake akawa anagonga geti lakini mkienda kumfungulia mnakosa?” Alizidi kuhoji
wakili Jonas Mlyanyama.
“Haswaah! Wala hjakosea kaka. Sasa kitendo cha
kumuona msichana huyo moyo wangu ulishtuka ghafla mpaka nikaanza kujihisi
napata shida kupumua. Baada ya hapo sikujitambua tena.”
Mpaka
hapo wakili wangu akawa ameshakifahamu kilichonifanya nizirai huku nikiwa
kwenye kizimba. Nilipotupia jicho kwa wakili Mlyanyama nilimuona kajishika tama
huku akionekana kuwaza kwa kina, baada ya hapo akashusha pumzi ndeefu iliyoashiria
mtu kuchoka ama kukata tamaa.
“Kwa
kweli hii kesi inautata sana. Tangu niwe wakili sijawahi kukutana na kesi yenye
kizaazaa kiasi hiki. Pamoja na kukaa katika kazi hii kwa miaka zaidi ya kumi na
mitano hii ndiyo mala ya kwanza kukumbana na kesi ngumu kama hii. Ama kweli hii
ni kali, tena ni kali ya karne.” Alisikika bwana Jonas Mlyanyama.
“Ehe, baada ya kuanguka nini kiliendelea?”
Nikazidi kudodosa.
“Kesi yako imeahirishwa, itapangwa tena pale
afya yako itakapoimarika.”
“Na yule mwanamke
alielekea wapi baada ya hapo?”
“Hata sikumfuatilia.” Alinijibu na kuonekana
tena kuzama kwenye lindi la mawazo.
“ Sasa subiri nikaandae hoja za kisheria za
kuja kumkabili siku ya kusikilizwa tena kesi yako, labda asije.”
“Yule ni mchawi kaka sidhani kama utamuweza.”
“Pamoja na uchawi wake hapa kagonga mwamba.”
Aliongea Mlyanyama huku akijipigapiga kifuani kuonyesha kujigamba fulani hivi.
“Yangu
macho na masikio siku hiyo, lakini mimi nimeshamnyanyulia mikono huyo ibilisi.
Nashangaa sijui kwa nini kaniandama sana na kunisababishia ndege mbaya katia
maisha yangu, kanipotezea dira ya maisha kabisa, isitoshe hata hatima yangu
haijulikani.” Nilijikuta nikiongea kwa uchungu huku nikionyesha kukata tamaa
kwa hali zote.
ITAENDELEA.....
No comments:
Post a Comment