Brighton anaota ndoto ya ajabu
akiwaona watu waliokufa siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick,
James na Anna. Baada ya ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa
anayemsababishia kesi ya mauaji ya mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi
inaunguruma mahakamani kisha anajikuta akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe
kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa gerezani
akisubiri tarehe za kunyongwa anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa amenunua
nyumba iliyokuwa ya marehemu James, naye Mack anaanza kumhadithia kisa
kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. Hatimaye siku ya kunyongwa inafika kweli, hata
hivyo anajikuta anakolewa kimiujiza na msichana aliyemsingizia kuua, yaani
Sharifa, anatolewa gerezani na kuwa huru kabisa. Sasa endelea...................
Mlango wa chumba kile ulikuwa umefungwa.
Nilishangaa kuona tunapenye kwenye ukuta kama vile tunapita sehemu yenye uwazi.
Tuliendelea
kutembea kwa hatua za madaha huku akiwa amenishika mkono. Tulitokezea mpaka nje
ya jengo tulilokuwemo. Tukaendelea kutembea kuelekea kwenye lango kuu la
kuingilia kwenye magereza hiyo.
Niliweza
kuwashuhudia askari magereza wakizunguka zunguka na wengine wakiwasimamia wafungwa
waliokuwa wanafanya kazi kwenye ngome ya gereza hilo.
Katika
fikra zangu nilijua kuwa kila mtu anatuona, nikaona nimuulize Sharifa,
“mbona tunatoka kwa kujiamini hivi? Hao askari
wakituona si tutapata tabu?”
“Hapa hatuoni mtu yoyote hata tupite palepale
aliposimama, labda ngoja nikupe mfano kwa ofisa yule tunayekutana naye.”
Alinijibu huku akinionyesha ofisa mmoja tuliyekuwa tunakutana naye.
Alipomsogelea
alimwasha kibao cha haja. Ofisa huyo aliishia kujipapasa tu na hakujua alikuwa
kapigwa na nani. Nilianza kucheka kwa kicheko cha chinichini baada ya
kukishuhudia hicho kisanga.
“Hata
ukicheka kwa sauti hamna atakayekusikia. Usiwe na wasiwasi upo kwenye mikono
salama kabisa.” Aliniambia baada ya kuniona nacheka kwa chinichini.
Tulitembea
mpaka tukafika kwenye geti kubwa. Tulipita bila ya kubughudhiwa na mtu yeyote.
Tulipofika nje akaniambia niende mpaka nyumbani kwangu halafu mambo mengine
tutayaongea hapo baadaye.
Nilipojaribu
kumuuliza kuwa yeye anaelekea wapi kwa wakati huo aliniambia sipaswi kujua.
Nilimuaga na kumshukuru kwa kuniokoa na adhabu iliyokuwa inanikabili kisha
nikaanza mdogomdogo kuchapa lapa kuelekea nyumbani kwangu.
Wakati
namuaga alikuwa kasimama barabarani. Nilitembea kidogo kisha nikageuka nyuma
kumwangalia. Lahaula! Sikumuona tena.
Akili
yangu ilibaki kuwa na kazi ya ziada japo kuwa nilikuwa nimetoka jela na
nimenusurika na adhabu ya kunyongwa. Kikubwa kilichokuwa kinaniumiza akili ni
hayo masharti yake. Mpaka muda huo nilikuwa sijajua ni masharti gani atanipa.
Kilikuwa ni kitendawili kigumu sana akilini mwangu.
Nilifuata
barabara nikitembea kwa miguu kwani mifuko yangu ilikuwa imetoboka, yaani
sikuwa hata na shilingi. Njiani nilikoma na moshi wa magari. Sikuwa na cha
kufanya zaidi ya kuyakenulia meno magari yote yaliyokuwa yakinipita kwa vile
sikuwa na nauli.
Safari
ya kutoka lilipokuwa gereza nililokuwa nimefungwa mpaka nyumbani kwangu ni
mwendo wa masaa mawili kwa miguu. Kibaya zaidi mambo ya kuombana lifti
hayakuwepo kabisa katika mji huo. Niliendelea na ‘ba funika ba funua’ mpaka
nikafika.
Nilifika
mpaka kwenye geti la fensi ya nyumba yangu, nikajaribu kulisukuma lakini likawa
gumu. Kwa kuwa kulikuwa na swichi ya kengele wala sikuhangaika. Nilipeleka
mkono wangu panapo swichi, nikabofya kistaarabu kisha nikakaa pembeni kusubiri
majibu.
Punde
si punde geti lilifunguliwa. Akatokea jamaa mmoja akiwa kifua wazi.
“Karibu!” Alisikika jamaa huyo akiniambia.
“Asante! Habari yako kaka?”
“Nzuri! Sijui nikusaidie nini?” Alihoji swali
hilo ambalo lilinifanya nimshangae.
‘Hivi
huyu hajui ya kuwa mimi ndiyo mwenye nyumba hii? Au anavyoniona nimekondeana
namna hii basi anajua kuwa mimi ni kapuku?’ Niliwaza huku nikiwa ninamwangali
jamaa huyo pasipo kummaliza. .
“Ndugu,
sema shida yako nina mambo kibao ya kufanya huko ndani, ila kama unakuja kupiga
kibomu kwa mheshimiwa kasafiri, tena hayupo kabisa ndani ya nchi hii.” Alizidi
kueleza jamaa huyo.
Maelezo
hayo yalinishtua na kunifanya nianze kupatwa na wasi wasi fulani. Niliyekuwa
nimemkabidhi nyumba pamoja na miradi yangu yote alikuwa ni kijana tu kama mimi.
Sasa nilizidi kuumiza kichwa uheshimiwa umetoka wapi kwa kijana kama huyo!
AISEEEH, KWA BRIGHTON SASA PANAITWA
KWA MHESHIMIWA, HUYO MHESHIMIWA NI NANI? PIA SHARIFA KAPOTELEA WAPI? JE, NA
MAISHA YA BRIGHTON YATAKUWAJE BAADA YA KUTOKA JELA? USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment