KWA WASOMAJI WAPYA.....
Brighton anaota ndoto ya ajabu akiwaona watu waliokufa
siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick, James na Anna. Baada ya
ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa anayemsababishia kesi ya mauaji ya
mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi inaunguruma mahakamani kisha anajikuta
akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa
ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa
anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James,
naye Mack anaanza kumhadithia kisa kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. sasa
endelea...................
Suala la kuandika barua kwa rais ndiyo
lilikuwa limetawala katika kichwa changu. Hiyo ndiyo fursa pekeee iliyokuwa
imebakia ya kujaribu kujitetea, si unajua tena mfa maji haishi kutapatapa.
Rais
anao uwezo wa kumsamehe mfungwa wa mauaji endapo ataandika barua kuelezea
ambavyo haki haikutendeka katika hukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu naye
akajiridhisha na sababu hizo.
Wazo
hilo alinipa Mack, akaniambia unaweza ukamwandikia barua rais na kumweleza
jinsi mazingira ya kesi yako yalivyokuwa. Kama akiridhika na maelezo yako
anaweza akakuachia ukawa huru.
Wazo
hilo nililiafiki na kulipokea kwa mikono miwili. Nikaandika barua na kuikabidhi
kwa mhusika gerezani hapo ambaye alifanya harakati za kuipeleka kwa mheshimiwa
rais. Nilijipa matumaini kuwa huenda mheshimiwa ataridhika na malalamiko yangu
na kuniachia huru.
Siku
zilizidi kukatika bila kupata majibu yoyote. Miaka kadhaa ilipita nikiwa
gerezani kusubiri siku za adhabu yangu ya kunyongwa. Ilibidi nikubaliane na
hali halisi ya kwamba kifo changu kitakuwa cha kupigwa kitanzi.
Hayawi
hayawi hatimaye yalikuwa. Siku moja nikiwa sina hili wala lile niliitwa na
kuambiwa masaa yangu yalikuwa yanahesabika. Yaani namaanisha siku yangu ya
kupigwa kitanzi ilikuwa ndiyo hiyo.
Nilipelekwa
kwenye chumba kimoja ambako niliambiwa nitakutana na mtumishi wa Mungu ili
anihubiri na kuniombea pia. Kama ningetaka kutubu dhambi zangu huo ndiyo
ulikuwa ni muda muafaka.
Nilijikuta mwili
ukinyong’onyea ghafla kwa hofu ya kifo. Usiombe kuijua siku na saa unayokufa.
Wakati
naukanyaga mlango wa chumba hicho nilimuona mwanamke aliyekuwa kainama chini
akisomasoma kitabu. Niliambiwa huyo ndiye mtumishi wa Mungu na nilipewa masaa
kadhaa ya kuongea naye kabla sijapelekwa kwenye chumba cha kunyongea.
Mwanamke
huyo alionekana kuwa bado yungali msichana. Hata hivyo mpaka nakaa nilikuwa
bado sijaiona sura yake kutokana na sababu kuu mbili; sababu ya kwanza ni
kutokana na yeye kuwa ‘busy’ na kusoma kitabu na sababu ya pili ni kutokana na
machozi kunifumba macho kwani nilikuwa nikilia kilio cha kimya kimya. Hicho
huitwa kilio cha ng’ombe; kilio cha kutoa machozi bila ya kutoa sauti.
HAYA SASA, HAYAWI HAYAWI MWISHO
YAMEKUWA, KWELI BRIGHTON ATANYONGWA?
USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment