KWA WASOMAJI WAPYA.....
Brighton anaota ndoto ya ajabu akiwaona watu waliokufa
siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick, James na Anna. Baada ya
ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa anayemsababishia kesi ya mauaji ya
mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi inaunguruma mahakamani kisha anajikuta
akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa
ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa
anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James,
naye Mack anaanza kumhadithia kisa kilichompelekea afungwe jela, sasa endelea...................
Pale
pale nikajishauri kuwa nimkatishe Mack kwa kumuuliza swali tena kwani kuuliza
ilikuwa siyo dhambi na nilikuwa sijakatazwa. Ndipo nilipomuuliza kuwa msichana
huyo alijitambulisha kwa jina gani.
“Alisema
kuwa anaitwa Sada, mwenyeji na mzaliwa wa Matopeni ila wazazi wake walikuwa
wameshafariki kwa kipindi hicho.” Hilo ndilo lilikuwa jibu la Mack kwa swali
nililokuwa nimemuuliza, jibu ambalo lilianza kunitoa katika hisia zangu juu ya
msichana huyo.
“Alikuwa
yukoje yukoje kimuonekano?” Nilizidi kudodosa nikidhani ya kuwa huenda alikuwa
kabadilisha tu majina.
“Alikuwa ni mwembamba halafu kaenda hewani
kimtindo, mweupe na mwenye mwanya. Akiwa anaongea sauti yake ilikuwa nzito
kiana.” Alidadavua Mack.
Jibu hilo pekee
lilitosha kuitengua hoja iliyokuwa imejengeka akilini mwangu ya kwamba mwanamke
huyo alikuwa ndiyo Sharifa. Nilimuacha Mack aendelee kunipa michapo labda kwa
baadaye ningeweza kung’amua kitu kuhusu mwanadada huyo.
Aliendelea
kunielezea. Akasema kuwa baada ya siku mbili kupita mwanamke huyo alijileta
mwenyewe kwa Mack akija kumwambia anampa onyo la mwisho, kama hatahama vitendo
vingefuata.
Mack alitaka sana
kuumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani akiamini kabisa kuwa yote yanawezekana
kwa nguvu ya hoja. Alimsihi mwanadada huyo waende kwenye ofisi za serikali ya
mtaa ili wakaliongelee shauri hilo.
Hata hivyo mwanamke
huyo alimjibu kwa nyodo nyingi akisema kuwa hana muda mchafu wa kwenda kuonana
na hao viongozi wa serikali za mtaa. Siyo muda peke yake, hata hadhi yake
ilikuwa siyo ya kwenda kuvimbisha tumbo lake mbele ya watu kama hao aliowaita
majuha.
Mack aliyapeleka
majibu hayo kwa hao viongozi, nao wakamwambia ya kuwa asubiri hatua
atakayochukua mwanamke huyo huku wakiahidi kuwa mstari wa mbele kumtetea.
Wiki moja baada ya
hapo kioja kilitokea nyumbani kwa Mack. Wakati anatoka kwenye mihangaiko yake
ya kila siku, alikutana na askari polisi waliokuwa wakimsaka kwa udi na uvumba.
Walipompata walimweka chini ya ulinzi wakimwambia ametoka kuua mtaa wa
Matopeni.
Alishangaa sana
kusikia hivyo, akawaambia kuwa yeye hajaua. Wakamwambia kuwa ameua kwani nyumba
aliyokuwa ameenda kufanya tukio hilo ilikuwa na kamera maalum za kunasa wezi na
wahalifu mbalimbali.
Alipouliza kamuua
nani akaambiwa kuwa kamuua mwanadada mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la
Sada, mwanamke aliyekuwa akiishi katika mtaa wa Matopeni.
Mack aliendelea
kubisha. Askari hao wakaanza kupekua kwenye gari lake. Katika pekua pekua
waliona bastola ndani ya gari la lake, kitu ambacho kilikuwa ni kigeni kabisa
kwake.
Kiukweli alikuwa hana
bastola na alikuwa hajawahi kumiliki siraha kama hiyo katika maisha yake, hata
kule kuishika masikini wa Mungu alikuwa hajawahi. Cha ajabu sasa ilipatikana,
tena ndani ya gari lake. Alizidi kuchanganyikiwa.
Askari waliendelea
kueleza kuwa kwenye kamera hizo Mack alianza kuonekana tangu anafika kwenye
nyumba ya Sada na zilikuwa zimerekodi tukio zima.
Kati ya askari
waliokuwa wamemkamata mmoja alikuwa akimfahamu, hivyo baada ya kuiona picha
yake kwenye kamera hizo akawa amemtambua.
Habari hiyo ilikuwa
ni ngeni kabisa kwa Mack. Aliwaeleza askari hao kuwa yeye hakuua ingawaje kweli
alikuwa katika mgogoro wa nyumba na huyo Sada. Alizidi kujitetea kuwa hata
nyumbani kwake (yaani kwa Sada) alikuwa hapafahamu kwani siku moja alienda
kumtafuta ili waende kwenye ofisi za serikali ya mtaa kuuongelea mgogoro wao
lakini hakufanikiwa kumpata msichana huyo.
Pamoja na kujitetea
kote huko, Mack aliambulia kuwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa kwenye kituo
cha polisi cha kati. Alikaa hapo kwa siku moja na nusu kisha jalada la kesi
yake likapelekwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi.
DAH! MAUZAUZA YANAHAMIA KWA MACK.
HUYO SADA NI NANI NA ANAUHUSIANO WOWOTE NA SHARIFA ALIYEKUWA AKIMSUMBUA
BRIGHTON? USICHOKE KUFUATLIA MWISHO WA SIKU MAJIBU YOTE UTAYAPATA.
No comments:
Post a Comment