KWA WASOMAJI WAPYA.....
Brighton anaota ndoto ya ajabu akiwaona watu waliokufa
siku nyingi kwa kujiua wakiwemo mzee Mboma, Patrick, James na Anna. Baada ya
ndoto hiyo anazongwa na mwanadada Sharifa anayemsababishia kesi ya mauaji ya
mpangaji wake, yaani Kishoka. Kesi inaunguruma mahakamani kisha anajikuta
akihukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe kwa kosa la mauaji ya Kishoka, kosa
ambalo alikuwa hajalitenda. Akiwa gerezani akisubiri tarehe za kunyongwa
anakutana na Mack, jamaa aliyekuwa amenunua nyumba iliyokuwa ya marehemu James,
naye Mack anaanza kumhadithia kisa kilichompelekea afungwe jela.
Kwa
kusimuliwa na Mack, Brighton anayasikia mengi kuhusu mali alizokuwa amerithi
kutoka kwa marehemu kaka yake kwa kila aliyekuwa amemuuzia aliishia kupatwa na
matatizo akiwemo Mack mwenyewe. Hatima siku ya kunyongwa inafika kweli, anaambiwa
akafanyishwe maungamo kwa mtumishi wa Mungu. Je, atanyongwa kweli? Sasa
endelea...................
Mara
baada ya kuketi mwanamke huyo aliinua kichwa chake, mbona nilizidi kuchoka!
Niliweza kumtambua barabara. Huwezi amini ndugu msomaji mwanamke huyo alikuwa
ni Sharifa, mwanadada aliyenisingizia kuwa nimeua kisha akaonyesha ushahidi wa
picha na kunifanya nihukuniwe kunyongwa.
Baada
ya kumuona hasira zilinijaa ghafla, nikasema potelea pote lolote na liwe,
hakuna cha maungamo wala nini. Moyo wa kulipa kisasi ulinijaa mtoto wa kiume,
nikatamani nimraruwe mle mle kwenye chumba hicho ili hata kama ninanyongwa na
yeye awe ameshakufa.
Hata
hivyo nilipiga moyo konde na kujishauri nitulize munkari na kuzizuia papara
zangu ili nimsikilize ananiambia nini.
Aliniangalia
kisha akaachia bonge la tabasamu. Hapo ndiyo niliweza kuuona uzuri wake
ulivyokuwa wa shani, mtoto masharah alikuwa kamili kila idara.
Hata
hivyo sikutishika na tabasamu lake hilo kwani nilijua wazi kuwa tabasamu hilo
lilikuwa ni la kinafiki. Nikazidi “kumlia buyu” nikisubiri aanzishe yeye
mjadala.
Alikuwa katupia suti
ya kike rangi nyeusi huku macho yake yakipendezeshwa na miwani midogo iliyokuwa
imemkaa kisawasawa.
“Sharifa, leo hii
wewe ndiyo mtumishi wa Mungu?” Niliamua kumuuliza bila woga baada ya ukimya
mrefu kidogo kutawala.
“Tulia Brighton na unisikilize kwa makini.”
Sauti nyororo ya msichana huyo ilipenya kupitia kwenye ngoma za masikio yangu,
sauti ambayo ilinikumbusha ufukweni siku niliyoanza kabisa kukutana naye.
“Hivi
unajua ni kwa nini matatizo yote hayo yamekuaandama?” Alinihoji huku nami
nikiwa makini kumsikiliza.
“Sijui labda uniambie wewe kwa maana
umeonekana kuyasakama sana maisha yangu.” Nilijibu kwa mkato na kukaa kimya.
“Chanzo cha matatizo hayo yote ni mirathi ya
kaka yako James.”
“Mirathi ya kaka yangu James! Imefanya nini?”
“Ujio wangu siyo kuja kujadili chanzo cha
matatizo yako, ila nilikuwa nakutaarifu tu ili ukae unajua.”
“Kwa hiyo umekuja kufanya nini?” Nilizidi
kumtwanga maswali bila woga wowote.
“Lengo
la mimi kuwa hapa ni kuja kukuokoa na adhadu ya kunyongwa kama utakuwa tayari
kutekeleza masharti nitakayokuambia.”
“Masharti yapi hayo?” Nilihohoji huku hisia za
wokovu wa chupuchupu nikizitazamia.
Hata
hivyo kazi ilikuwa kwenye hayo masharti. Ingawa alikuwa hajaniambia ila
nilihisi yangekuwa magumu mno.
“Huhitaji kuyajua kwa sasa hayo masharti, kama
upo tayari nikuokoe sema.” Aliongea Sharifa na kuzidi kuniweka katika wakati
mgumu.
Akili
yangu ilikuwa ikizunguka kama korona kwa wakati huo huku nikiwaza na kuwazua ni
uamuzi gani nichukue, lipi nishike na lipi niache.
Kibaya
zaidi nilikuwa sijaambiwa masharti nitakayopewa, hapo ndiyo nilizidi
kuchanganyikiwa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani, isitoshe kufa
kwa kunyongwa nako kulikuwa kukinitisha.
‘Hii
ni bahati ya mtende nisiiachie Brighton mimi. Hayo masharti nitahangaika nayo
mbele kwa mbele, kikubwa ni kwamba niwe nimeokoka na adhabu ya kunyongwa.
Yakienda kunishinda si nakataa tu, atanifanya nini wakati gerezani tayari
kashanitoa?’ Niliwaza kimoyomoyo huku nikionekana kuukubali msaada wa Sharifa.
Nilitulia
kidogo kama nawaza kitu fulani kwa kina, ghafla niligutushwa na sauti ya
Sharifa iliyokuwa ikiniambia nifanye maamuzi yangu haraka kwani nilikuwa
namchelewesha.
“Sawa
nimekubali niokoe” Nilijikuta najiropokea tu wala nilikuwa sijakamilisha
sawasawa.
Baada
ya kuongea hivyo nilimuona Sharifa akitoa tena tabasamu lake la ukweli,
tambasamu ambalo nilikuwa nikilifurahia kila alipolitoa. Aliinuka kwenye kiti
alichokuwa amekaa kisha kitabu alichokuwa nacho mkononi akakitumbukiza kwenye
mkoba wake aliokuwa nao. Akaja upande niliokuwa nimekaa, akaniambia nami
niinuke. Nilipoinuka akanishika mkono na kuniambia tuondoke zetu.
HEHEEEH! MAKUBWA.MIRATHI YA JAMES
INAMSABABISHIAJE MATATIZO BRIGHTON? PIA WATAFANIKIWA KWELI KUTOKA KWENYE NGOME
YA MAGEREZA? NA KAMA WAKITOKA NI MASHARTI YAPI SHARIFA ATAMPA BRIGHTON? USIKOSE
TOLEO LIJALO.
No comments:
Post a Comment