ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA...
Nilizidi
kuchanganyikiwa kwa kuona maisha yangu yakiandamwa na mikasa, mikosi na ndege
mbaya kila wakati. Kichwa kilizidi kuuma.
SASA ENDELEA.......
Maisha ya gerezani
yalizidi kusonga huku nikiwa nasubiri siku yangu ya kutundikwa kwenye kitanzi
ifike, siku ambayo nilikuwa sijui tarehe yake, mwezi wala mwaka wake.
Huko gerezani
nilishangaa sana kumkuta jamaa mmoja ambaye nilikuwa namfahamu. Jamaa huyo ni
yule niliyekuwa nimemuuzia nyumba aliyokuwa kahongwa Neila, mwanamke aliyeuliwa
na James baada ya kumuonyeshea utapeli wa mapenzi na nyodo za kila aina.
Nilishangaa sana
kumkuta jamaa huyo aliyekuwa anajulikana kwa jina la Mack. Alikuwa kakaa gerezani
kwa muda mrefu kiasi kwani alikuwa kashapewa mpaka unyapara wa humo gerezani.
“Kulikoni tena ndugu
yangu na wewe umeletwa huku?” Lilikuwa ni swali la Mack siku ya kwanza kabisa
kuingia jela mara baada ya kuniona.
“Matatizo makubwa
ndugu yangu, hapa nilipo sina hata hamu! Na wewe lini tena humu na kipi
kilichopelekea kuletwa sehemu hii isiyofaa?” nilimuuliza nikiwa na shauku kubwa
ya kujua kilichokuwa kimemsibu.
Kabla ya kunijibu
aliguna kisha akavuta pumzi ndefu na kisha
kuzishusha.
“Ni stori ndefu mdogo wangu, hebu anza kwanza
wewe kunieleza mkasa uliokusibu mpaka ukaletwa humu.”
Niliamua kuanza
kumsimulia jinsi mambo yalivyokuwa. Nikamweleza kinaga ubaga, hatua kwa hatua
tangu kipindi nahama mji tuliokuwa tunaishi na kaka James.
Wakati namsimulia alikuwa
katulia tulii huku akinisikiliza kwa umakini mkubwa. Nilipomaliza nikamuachia
naye aweze kufunguka. Alianza kwa kusema,
“Kisanga chako hakina tofauti sana na kile
kilichonitokea mimi.” Alitulia kidogo kumeza mate.
Nilishtuka
sana baada ya kusikia hivyo. Nikawa na hamu ya kusikia mambo yalivyokuwa huko.
Aliendelea kuniambia kuwa mara baada ya kumuuzia nyumba ile alihamia. Akawa
anaishi pale yeye na familia yake ambayo ilikuwa na jumla ya watu watatu, yaani
yeye mwenyewe, mke wake na mtoto wake mmoja.
Kabla
hajamaliza hata mwezi kuna msichana alijitokeza na kumtaka ahame pale akidai
kuwa nyumba ile ni yake. Baada ya kuambiwa hivyo hakutishika kwani ushahidi
wote wa kuonyesha kuwa nyumba ile ni mali yake ya halali alikuwa nao.
Mwanadada
huyo alizidi kumwandama kwa kumtisha na vitisho kedekede. Pamoja na vitisho
hivyo Mack aliendelea kukaidi madai ya mwanadada huyo.
“Huyo
msichana ulikuwa unamfahamu kabla?” Nilimtwanga swali hilo nikiwa najaribu
kudadisi juu ya msichana huyo.
“Hapana! Nilikuwa sijawahi hata kumuona kabla
ya hapo.” Mack alinijibu kama hivyo.
“Alisema yeye ni mwenyeji wa wapi?” Niliuliza
tena.
“Alidai kuwa ni mwenyeji wa palepale mjini
mtaa wa Matopeni. Lakini mimi niliona ni muongo kwani Matopeni nilikuwa
mwenyeji kidogo na nilikuwa sijawahi kuona sura kama yake.”
Niliona
niachane na kuuliza uliza maswali kwani yalikuwa yanakatisha uhondo wa stori
yenyewe. Nikamuacha Mack aendelee kunipa michapo hatua kwa hatua.
Aliendelea kueleza
kuwa baada ya kukaidi mwanamke huyo hakuchoka kumghasi akimwambia ahame katika
nyumba ile.
Baada ya Mack kuona
kero imezidi aliamua kulipeleka shauri hilo kwenye uongozi wa serikali za mtaa
ili wamsaidie kuipata suluhu. Alipowaeleza viongozi hao walimwambia aende na
mlalamikaji huyo ili wakapate kuyasikiliza malalamiko yake.
“Nikaenda kumtafuta
mtaa wa Matopeni lakini sikufanikiwa kumuona. Kila niliyemuuliza alisema
hamfahamu.” Alisikika Mack akiniambia.
Sikutaka kutia swali
katika maelezo yake, nikachombeza tu kwa kumwambia aendelee, naye akaendelea.
“Baada ya kumkosa nilirudi nyumbani. Nikaamua
kumsubiri atakapokuja nimkamatishe na kumpeleka kwenye ofisi za serikani za
mtaa.”
Huku
nikimsikiliza lakini kwenye ubongo wangu kulikuwa na mjadala mzito uliokuwa
ukiendelea. Suala la kulifahamu jina la msichana huyo ndiyo lilikuwa nimetawala
kwenye akili yangu. Mawazo yangu yote yalikuwa yananituma kuwa piga ua galagaza
yule msichana alikuwa ni Sharifa, msichana aliyenisababishia matatizo ya
kupatikana na hatia ya kuua wakati sijaua.
JE, MSICHANA HUYO NI NANI NA KWA
NINI ANAMSUMBUA MACK? USIKOSE TOLEO LIJALO.
No comments:
Post a Comment