ILIPOISHIA........
Kumuona tena huyo
jamaa ndiyo kulinifanya nitabasamu kwani nilikumbuka visa na vituko alivyokuwa
akivifanya kipindi cha uhai wake.
SASA ENDELEA.......
Jamaa huyu ni
Patrick, Patrick Chibehe; kijana wa kihehe aliyetia fora kwa madeni pale mtaani
kwetu. Walipokusanyika watu watano basi watatu au wanne walikuwa wakimdai.
Ulevi wake wa pombe
ya kienyeji ijulikanayo kama mabonge ndiyo uliomfanya awe na madeni lukuki.
Wakati mwingine alidiriki kuuza hata nguo alizokuwa amevaa kisha kubaki kifua
wazi au kubaki na kaputura tu ili apate pesa ya kununulia pombe.
Vituko alivyokuwa
navyo wakati wa uhai wake ndivyo vilivyonifanya niachie tabasamu likifuatiwa na
kutikisa kichwa. Nilikumbuka jinsi alivyotuingiza mjini kwa kutuuzia TV moja
watu watatu tofauti.
Kumbukumbu zilizidi
kunijia jinsi kijana huyu alivyopoteza uhai wake kimzaha mzaha. Aliamua
kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake baada ya kuambiwa kuwa wadai wake
tumemshitaki kituo cha polisi. Aliona njia pekee ya kujiokoa na hilo janga ni kujinyonga.
Kwa kweli nilishindwa
kabisa kuamini kwa hicho nilichokuwa nakiona, nikabaki nikijiuliza kwa nini
kila niliyemtambua katika kundi hilo alishakufa. Nilianza kufikiria kuwa labda
hata wale wengine ambao nilikuwa siwatambui katika hilo kundi walikuwa wameshakufa.
‘Kwa hali kama hii
huenda hata wazazi wangu nitawaona.’ Wazo hilo lilinijia baada ya kuwaona mzee
Mboma, kaka James pamoja na Patrick.
Niliendelea kukodoa
macho walipokuwa watu hao, nikazidi kuumia kutokana na vilio walivyokuwa wakivitoa.
Nikazidi kujiuliza;
‘Watu husema kuwa mtu akifa huenda kupumzika
kwa amani, mbona sasa hawa wanalia?’ Nilikosa jibu kabisa.
Nilikomaa kuangaza
angaza nikijipa moyo ya kwamba huenda nitamtambua mtu mwingine, hasahasa shauku
yangu ilikuwa ipo kwa wazazi wangu waliofariki kitambo nikiwa bado nipo darasa
la tatu. Pamoja na kukodoa kwangu macho niliambulia kapa, sikufanikiwa kuwaona
baba yanga na mama yangu katika kundi hilo.
Katika harakati za
kuhangaika kutafuta mtu mwingine ambaye ningeweza kumfahamu kutoka kwenye hilo
kundi, nilimuona mtu ambaye aliamsha machungu ndani ya mtima wangu. Donda
lililokuwa limeanza kupona moyoni mwangu sasa lilitoneshwa tena na kitendo cha
kumuona mtu huyu, tena lilitoneshwa kwa msumari wa moto.
Niliyasikilizia
maumivu hayo yazidiyo maumivu ya mwanamke anayeumwa na uchungu wa kujifungua,
hasa uchungu wa mimba ya kwanza.
Marehemu Anna,
aliyekuwa kipenzi cha moyo wangu, ndiye niliyemuona kwa wakati huo. Naye
alikuwa analia kama walivyokuwa wanafanya wale wengine katika hilo kundi. Nilivuta
na kushusha pumzi, nikakodoa macho pima zaidi ya vile nilivyokuwa nimekodoa
mwanzo huku mdomo ukiwa wazi!
‘Ama kweli leo ndiyo
leo, ngoja nisubiri hatima yake.’ Niliwaza kimoyomoyo huku mdomo ukiendelea
kuwa wazi, kamasi pamoja na machozi vilianza kunitoka hata sikuwa na muda wa
kuviondoa badala yake nilizidi kuviachia vitiririke mpaka basi.
ITAENDELEA.......
No comments:
Post a Comment