ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Vijana
hao niliwafananisha na mazuzu ambao mishipa ya fikra ilishakatika kichwani
mwao. Rumande siyo sehemu ya kukimbilia kama una akili yako timamu.
*************************
SASA ENDELEA.......
Watu walikuwa wamefurika kusikiliza kesi mbalimbali zilizokuwa
zikiunguruma katika mahakama kuu ikiwemo kesi yangu. Kesi nyingi zilizokuwa
zikitajwa siku hiyo zilikuwa ni za mauaji.
Wakati
huo nilikuwa nipo kwenye kizimba cha washtakiwa nikiapishwa. Mara baada ya
kuapishwa, kesi ilisomwa.
“Ni
kweli au si kweli?” Lilikuwa ni swali la mwendesha mashitaka Charles Ngonyani ambaye
alikuwa ni wakili wa serikari.
Hata
hivyo wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliniambia nikane, nami nikatikisa
kichwa kukataa kisha nikasema,
“si kweli”
Baada
ya hapo kesi iliahirishwa tena kwa muda wa wiki moja ili upande wa mashtaka
uanze kupeleka mashahidi wake.
Nilirudishwa
tena gerezani nikiwa bado mahabusu. Mpaka hapo nilikuwa nimeshaipata freshi ya
kwenda na kurudi mahakamani, kesi yenyewe ilikuwa haijaanza hata kusomwa.
Niliendelea
kukaa rumande mpaka siku ya kesi yangu ikawadia tena. Siku ilipofika kama
kawaida karandinga la magereza lilitusomba mpaka mahakamani mahabusu ambao kesi
zetu zilikuwa zinasomwa siku hiyo.
Shahidi
aliyeanza kutoa ushahidi kutoka upande wa mashitaka alikuwa ni Sajenti Bakari
Mlongo ambaye ndiye alikuwa amelibeba jukumu la kuipeleleza kesi yangu.
Huku
akiongozwa na wakili wa serikali, Sajenti Bakari Mlongo alieleza kuwa siku ya
tukio akiwa kazini kwake kwenye kituo cha polisi cha kati alipigiwa simu
kupitia simu ya kazini na mwanamke mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni ndugu
yake na Kishoka.
“Baada ya mpigaji
kujitambulisha hivyo aliwaambia nini?” Aliuliza wakili wa serikali bwana
Charles Ngonyani.
“Mtu huyo alieleza kuwa kuna mauaji ya kutisha
yaliyokuwa yamefanyika kwenye nyumba ya bwana Brighton David.” Alisikika
Sajenti Mlongo akijibu.
“Mtu huyo alieleza kuwa nani kauawa?”
“Ndiyo alieleza. Alisema kuwa aliyekuwa
ameuawa ni ndugu yake aitwaye kishoka.”
Sajenti Mlongo
aliendelea kueleza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alitoka yeye na askari wengine
wanne na kuelekea kunako eneo la tukio.
“Mlifika mpaka eneo
la tukio?”
“Ndiyo tulifika.”
“Ikawaje?”
“Kwanza tulilikuta geti la ngome ya nyumba
hiyo lipo wazi, tulipofika kwenye mlango wa kuingilia wa nyumba ya mtuhumiwa
tuliuona uko wazi. Ndipo tulipoingia kwa tahadhari kubwa. Hata hivyo pale
ukumbini hakukuwa na mtu zaidi ya runinga iliyokuwa imewashwa.”
“Baada ya kuona
hapana mtu sebuleni mlichukua uamzi gani?”
“Tulijaribu kuangaza na kubaini kuwa mlango wa
chumba kimojawapo kwenye hiyo nyumba
ulikuwa wazi na taa ilikuwa ikiwaka. Ndipo mimi na afande mmoja
tuliingia kwenye chumba hicho.”
“Endelea kuieleza mahakama mlichokikuta baada
ya kuingia kwenye chumba hicho!”
“Tulimkuta mtuhumiwa
ambaye ni bwana Brighton akizunguka zunguka humo chumbani huku mwili wa Kishoka
ukiwa kitandani huku kichwa kikiwa mbali na kiwiliwili chake. Vile vile kisu
ambacho tulishuku kutumika katika kutekeleza mauaji hayo kilikuwa kikiambaa
ambaa sakafuni.”
“Baada ya kuona hivyo mlichukua uamuzi gani?”
“Tulimuweka chini ya ulinzi mtuhumiwa, lakini
kabla hatujamfunga pingu alianguka ghafla na kupoteza fahamu.” Aliongea Sajenti
Mlongo.
“Huyo mtuhumiwa
mliyemkamata siku hiyo ukimuona unaweza kumtambua?” Aliuliza wakili Charles
Ngonyani.
“Ndiyo ninaweza.”
“Hebu ionyeshe mahakama tukufu mtu huyo kama
yumo humu!”
“Yule pale kwenye kizimba.” Sajenti Mlongo
aliongea huku akinisonta pale nilipokuwa.
Wakili
wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia,
“Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.
KESI HII ITAISHAJE? USIKOSE SEHEMU
YA 23!
No comments:
Post a Comment