Saturday, October 5, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 23




ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia,
“Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.
SASA ENDELEA.......            
            Ilifika zamu ya wakili wa upande wa utetezi kumuhoji shahidi aliyekuwa kizimbani. Wakili huyo bwana Jonas Mlyanyama alisimama na kusogea karibu na kizimba cha shahidi wa upande wa mashitaka sajenti Bakari Mlongo.
            “Umesema mlipoingia chumbani mlimkuta mtuhumiwa anazunguka zunguka huku kisu kikiwa kinaambaa ambaa sakafuni, si ndiyo?” Mlyanyama alimhoji shahidi huyo.
“Ndiyo!” alijibu na kumsikiliza wakili wangu aendeleee kuongea
“Nikiiambia mahakama tukufu ya kwamba mteja wangu alikuwa katika kustaajabu baada ya kulikuta tukio hilo limefanyika katika chumba chake nitakuwa nakosea?”
“Ndiyo utakuwa unakosea kwa vile alama za vidole zilionekana kwa mtuhumiwa baada ya kuchukua vipimo, yote hayo yatakuja kuelezewa na mtaalamu wetu wa mambo ya picha na alama za vidole ambaye tulikuwa tumeambatana  naye siku hiyo.”
            “Na ikiwa labda mtuhumiwa alikishika kisu pamoja na mwili wa marehemu wakati tukio limeshafanyika ikiwa kwa kutokujua au kutokana na kuchanganyikiwa na hali ya tukio lilivyokuwa?”
“Kwenye vipimo hatukuona alama zingine zaidi ya alama za mtuhumiwa tu.”
            “Huyo aliyewapigia simu kituoni kuwapasha taarifa za tukio alikuja kituoni?”
“Hapana!”
“Mlichukua namba yake ya simu baada ya kumaliza kuongea naye?”
“Hatukuweza kuchukua namba yake ya simu kwa sababu alipiga kwenye simu ya mezani.”
            “Mpaka jalada la  upelelezi wa kesi hii linakamilika mtu huyo aliwahi kufika kituoni japo mara moja nanyi mkapata kumfanyia mahojiano juu ya tukio hilo?” Wakili Jonas Mlyanyama alimtwanga swali hilo tena shahidi wa upande wa mashitaka.
“Hapana!”
“Sasa mimi naiambia mahakama kuwa mteja wangu hakuua bali mwanamke huyo ndiye mbaya na huenda ndiye aliyeua au anafahamu mwanzo mpaka mwisho juu ya mauaji ya Kishoka.”
“Siyo hivyo, mtuhumiwa ni yule pale kizimbani kwa sababu hata alama zake zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kinachosadikika kutumika kumchinja marehemu.”
“Sasa kwa nini mtoa taarifa wa awali asijitokeze kituoni kutoa maelezo na kuwa tayari kuja kutoa ushahidi mbele ya mahakama?”
“Kwa kweli hilo siwezi kujua ni kwa nini hajaonekana kituoni.”
“Basi kubaliana na mimi ya kuwa yule ndiyo mhalifu.”
            Sajenti Bakari Mlongo alionekana kuwa na kigugumizi hatimaye akaganda mithili ya cd kongwe iliyochakaa. Wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama alimwambia hakimu hana la zaidi la kumuuliza shahidi huyo.
ITAENDELEA..........

No comments:

Post a Comment