ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Hebu tuonyeshe kama mtu huyo yumo
humu ndani ya mahakama!”
“Ni yule pale kwenye kizimba.”
Aliongea msichana huyo huku akinisonta.
SASA ENDELEA.......
Mwendesha mashtaka aliichukua kamera na
kuipeleka kwa jaji kisha akasema amemaliza muongozo wake kwa shahidi.
Akili
yangu ilizidi kuchanganyikiwa. Ushahidi wa picha uliokuwa umetolewa na msichana
huyo ulizidi kuivuruga akili yangu. Japokuwa nilikuwa bado sijaziona hizo picha
lakini niliamini kabisa kuwa msichana huyo hawezi kupeleka kitu ambacho siyo
cha kweli mbele ya mahakama.
“Lazima kweli kuna
picha zangu kwenye kamera hiyo, lakini sasa hizo picha kazitoa wapi wakati mimi
sikumuua Kishoka?” Niliwaza na kuwazua bila kupata jibu.
Wakati nikiwaza hivyo
wakili wangu aliinuka na kuomba auone ushahidi wa vielelezo vya picha uliokuwa
umetolewa na shahidi huyo. Alipoletewa kamera hiyo alibaini kuwa picha hizo
zilikuwa ni zangu kweli.
Naye alizidi
kuchanganyikiwa. Akaomba nionyeshwe na mimi kisha akaruhusiwa. Nilipoonyeshwa
nilizidi kupigwa na butwaa baada ya kuona picha zikionyesha namchinja Kishoka.
Sikuamini kwa macho yangu.
Zilikuwa ni picha
kama saba hivi ambazo zilikuwa katika mapozi tofauti, yote yakiwa yanaonyesha
nikiwa katika hekaheka ya kumchinja Kishoka kama kuku. Nilizidi
kuchanganyikiwa.
Wakili wangu
aliniangalia huku akiwa amenywea kisha akatikisa kichwa. Aliondoka na kwenda
karibu kabisa na kizimba cha shahidi kisha akakaa mkao wa kuanza kumhoji
maswali shahidi aliyekuwa kizimbani ambaye ni Sharifa.
Hata hivyo alishikwa
na kigugumizi ghafla na kushindwa kabisa kuongea. Kila alipojaribu kuongea
alijikuta akigugumia na kushindwa kuyatamka maneno waziwazi.
Hali hiyo ilileta
taflani kubwa ndani ya mahakama hiyo. Kila mtu akaanza kushangaa ni kwa nini
wakili huyo amekuwa namna ile. Hali hiyo ilimfanya jaji aiahirishe tena kesi na
kuipangia singu nyingine.
Kwa upande wangu
sikushangaa sana kuona vioja hivyo kwani nilikuwa najua fika kuwa mwanamke yule
ambaye alikuwa amejitambulisha kwa jina la Sharifa alikuwa anatumia nguvu za
giza.
Nilirudishwa mahabusu
kama kawaida, rumande sasa ikawa ni makazi yangu ya siku nyingi. Mahabusu
wengine walikuwa wananikuta na kuniacha kutokana na kesi zao kufikia muafaka,
wengine walikuwa wanahukumiwa vifungo na wengine waliokuwa wakishinda
waliachiwa huru.
Kwangu mimi ilikuwa
kila siku danadana, limeisha hili linaingia lile. Ilifikia kipindi nikachoka
kabisa na maisha ya huko rumande, nikawa natamani hata kujiua lakini
niliyakumbuka maneno mazito ya marehemu Anna aliyoniambia nikiwa ndotoni ya
kuwa adhabu ya mtu anayejiua ni babu kubwa.
Kabla siku ya
kusikilizwa kesi yangu haijafika nililetewa taarifa kuwa wakili wangu kafariki
dunia. Tangu alipotoka mahakamani siku ile hakuweza tena kuongea, hata kile
kigugumizi alichokuwa akipapatua siku hiyo kilibadilika akawa haongei kabisa.
alikuwa ni zaidi ya bubu.
Taarifa hizo
ziliendelea kueleza kwamba zilipopita siku mbili alianza kuumwa sana hatimaye
akawa ameaga dunia. Habari hizo za tanzia ziliniuma sana; kumpoteza wakili
Jonas Mlyanyama, mtu ambaye alikuwa makini katika kazi yake.
‘Nilimwambia aiache
kesi yangu naye akang’ang’ania kuendelea kuisimamia, ona sasa yaliyomfika.
Laita kama angenisikia na kuachana na hii kesi asingekufa, huyu mwanamke ni
hatari sana.’ Nilijiwazia huku moyo wangu ukiwa na simanzi kubwa kutokana na
kifo cha wakili Mlyanyama.
Taarifa hizo ambazo
zilitoka serikalini ziliendelea kunijuza kuwa kwa wakati huo nilikuwa
natafutiwa wakili mwingine tena ambaye angeendelea kunitetea katika kesi yangu
hiyo. Hata hivyo niliwaambia wasihangaike kunitafutia wakili mwingine kwani
yangeweza kumtokea kama yaliyomtokea Jonas Mlyanyama.
“Hii kesi ina utata
mkubwa mno kwani tangu mwanzo wake ni mauzauza matupu. Mimi nawaomba
msinitafutie wakili yeyote, nitaimalizia mwenyewe.” Nilimwambia mtu aliyekuwa
kaniletea taarifa hizo.
“Lakini una haki kisheria kutafutiwa wakili wa
kukutetea?”
“Ndiyo nina haki, lakini kwa hali ilivyo
katika kesi hii sioni maana yoyote ya kusababisha watu kupoteza maisha yao kwa
ajili yangu, kesi yenyewe haina hata mwelekeo mzuri.”
“Haya bwana wewe wasema, mimi nitapeleka
taarifa kama ulivyotaka.” Alimalizia mjumbe huyo na kuondoka zake.
MASKINI, WAKILI WA BRIGHTON
ALIONYWA ILA AKAPUUZA, SASA YAMEMKUTA MAKUBWA! NINI HATIMA YA BRIGHTON? NA NI
KWA NN MSICHANA HUYO KAMUANDAMA! USIKOSE KUFUATILIA SIMULIZI HII!
No comments:
Post a Comment