ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
“Kwa nini kesho yake asubuhi
ulikuwa unatusumbua na Kishoka ukigonga geti na kupotea kimiujiza?”
“Sikuwa mimi?”
“Alikuwa nani?”
“Mimi sijui.”
SASA ENDELEA.......
Baada ya kuona msichana huyo anakikataa kila
nilichomuuliza hasira zilianza kuniingia. Ghafla likaniijia swali ambalo
nilijikuta namuuliza kwa mtindo wa kuropoka vile.
“Wewe
ni mchawi?”
“Hapana mimi siyo mchawi.”
“Wewe ni jini?”
“Hapana mimi siyo jini.”
“Kama kweli wewe siyo
jini hebu apa kwa Mungu ukisema kuwa wewe siyo jini?”
“Sasa niape ili iweje?” Aliongea Sharifa huku
naye akionekana kuanza kuhamaki.
“A-aaah! Wewe hebu apa na kama siyo jini kweli
hautadhurika na chochote.”
Huku
nikiwa nimechachamaa kumlazimisha Sharifa akiri kwa ulimi wake kuwa yeye siyo
jini, nilisikia sauti ya jaji akiingilia kati mahojiano yetu.
“Naona mshtakiwa umekosa maswali ya msingi ya
kumuuliza shahidi. Kama huna swali jingine sema ili nimruhusu shahidi atoke
kizimbani.”
“Mheshimiwa jaji huyu
mwanamke siyo mtu wa kawaida kabisa, na sielewi ni kwa nini kaniandama mimi tu
katika dunia hii. Amini nakwambia alianza kunifanyia mauzauza siku moja kabla
ya kifo cha Kishoka kutokea, hata wakili aliyekuwa akinitetea kayaona mauzauza
na ndiyo maana alishindwa kabisa kuongea siku ile. Alianza kwa kumuonya aachane
na kesi hii na kumuonya kuwa atamfanya kitu kibaya lakini wakili huyo
hakutishika. Alipoona vile akaamua kumuua kabisa kwa kuona kwamba kakaidi, hebu
muache aape kama kweli ni binadamu wa kaida, na endapo atakuwa siyo binadamu wa
kawaida Mungu anaenda kumuumbua hapahapa!” Nilijaribu kujitetea kwa jaji.
“Unaswali jingine
zaidi ya hilo?”
“Endapo ataapa maswali yatapatikana.”
“Shahidi, unaweza ukashuka kizimbani maana
mshtakiwa hana jipya.” Alitamka jaji na kunifanya niishiwe nguvu.
Nilipotupia
jicho kwenye kizimba cha mashahidi nilimuona Sharifa akiondoka kizimbani hapo
na kwenda kuketi. Kitendo cha kuondoka msichana huyo bila kufanya nilichokuwa
nimemtaka akifanye kiliniumiza sana moyoni.
Baada
ya Sharifa kushuka kizimbani upande wa mashtaka ulimpandisa shahidi mwingine
ambaye alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa wamekuja kunikamata siku ya
tukio.
Mpaka
anapanda kizimbani na kuapishwa kisha kutoa ushahidi wake, akili yangu haikuwa
katika ushahidi wake bali ilikuwa ikimfikiria Sharifa tu. Tena kichwa changu
kilikuwa kimevurugika vibaya vibaya kutokana na jaji kunikatalia ombi langu
kwani niliamini kuwa endapo angekuwa ni jini kweli basi angeumbuka.
Alipomaliza kutoa
ushahidi wake ambao haukuwa na tofauti kubwa sana na ule uliotolewa na askari
wenzake aliokuja nao kwangu siku ya tukio, jaji aliniuliza kama nina swali kwa
shahidi.
Kusema kweli nilikuwa
sijasikia hata neno moja alilokuwa ameongea shahidi huyo wakati anatoa ushahidi
wake kwa vile nilikuwa nimezama katika lindi la mawazo juu ya Sharifa. Sasa
ningeuliza nini ilhali nilikuwa sijayanyaka maelezo yake hata kidogo!
Ili kukata mzizi wa
fitina nilifumbua kinywa changu na kusema kwa mkato kwamba sina swali lolote
kwa shahidi huyo. Ndipo jaji alipomruhusu aende kuketi.
Baada ya hapo mwendesha
mashtaka aliinuka na kumwambia jaji kuwa upande wa mashtaka ulikuwa
umekamilisha mashahidi wake. Baada ya jaji kuambiwa hivyo aliniuliza kama nina
mashahidi ili baraza lijalo nianze kuwaleta.
Nilichomjibu ni
kwamba sina mashahidi kwani kesi yenyewe ilikuwa imeghubikwa na utata mkubwa, pia
kutokana na mazingira yake jinsi yalivyokuwa.
Baada ya kumwambia hivyo jaji aliutaka upande
wa mashtaka kuandaa maelezo ya mashtaka kuonyesha ni kwanini unamuona mshtakiwa
anahatia kwa mujbu wa ushahidi uliotolewa. Shauri hilo liliahirishwa tena kwa
mwezi mmoja.
*************************
ITAENDELEA.......
No comments:
Post a Comment