Wednesday, December 18, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 56


Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo uraiani na anachukuliwa na Sharifa na kupelekwa kwenye hoteli na kuanza kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake (yaani James) ulivyopatikana.......endelea

ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...

 Mara baada ya kuongea hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.

                        **************************   
SASA ENDELEA..........
Asubuhi ilifika, ilikuwa ni asubuhi ya kwanza kuiona nikiwa uraiani baada ya kukaa rumande na hatimaye gerezani kwa miaka mingi. Niliamkia kwenye hoteli hiyo hiyo niliyokuwa nimepelekwa na Sharifa jana yake.
Mara baada ya kuamka nilitupia jicho langu kitandani kuiangalia brificase iliyokuwa imejaa mapesa niliyokuwa nimeachiwa na Sharifa. Niliiona imetulia. Nikajiinua kisha nikaifungua na kuiona minoti imejaa tele.
Nilipoangalia mezani niliziona funguo za gari niliyokuwa nimeachiwa. Kwa bahati nzuri chumba nilichokuwa kilikuwa kipo upande tuliokuwa tumeegesha gari. Nikaamua kuchungulia nje ili kujiridhisha kama gari hilo lilikuwepo kweli. Nikaliona limetulia.
Wazo nililokuwa nalo usiku wakati Sharifa hajaondoka ni kukataa katakata kufuata masharti yote niliyokuwa nikishinikizwa kuyafanya; masharti ya kuoa mwanamke kisha akishanizalia mtoto nimtoe kafara pamoja na mtoto aliyemzaa, na baada ya hapo niwe natoa kafara mtu mmoja kila mwaka ambaye ni mfanyakazi wangu ama mteja wangu wa aina yoyote ile.
Hata hivyo baada ya Sharifa kunishika kichwani muda mfupi kabla ya kuyeyuka ghafla wazo hilo nalo liliyeyuka kabisa kichwani mwangu. Nikaanza kujiona kama mtu anayechezea shilingi kwenye tundu la msala.
Nililipima jambo hilo usiku kucha kwa mapana na marefu, nikaona hakuna sababu yoyote ya kulipiga teke debe la bahati kama hilo. Kitu kilichonipa moyo ni kwamba sikutakiwa kumtoa kafara ndugu yangu yeyote wa karibu zaidi ya mke ambaye nitamuoa kwa ajili hiyo pamoja mtoto nitakayemzaa kwa ajili hiyo.
Nikaona ni bora nikubaliane na shinikizo la Sharifa ili nitengeneze maisha yangu, niwe mmoja kati ya matajiri wakubwa nchini na duniani pia. Moyo wangu uliridhia kabisa kutajirika kwa njia hiyo, njia ya nguvu za giza na ya kishetani huku nikiwa tayari kuendelea kuteketeza watu kila mwaka kwa kuwatoa kafara ili nizidi kuulinda utajiri wangu huo.
Pesa nilizokuwa nimeachiwa na Sharifa zilizidi kunipa jeuri, jeuri ya kwenda kununua nyumba sehemu yoyote katika nchi hiyo. Jambo la kuendelea kuishi kwenye mji huo sikuwa nalo kabisa akilini mwangu, hivyo nikaamua kuondoka asubuhi hiyo kwenda mji mwingine uliokuwa mbali na mji huo.
Niliinuka na kwenda maliwatoni kujimwagia maji mwilini mwangu. Nilipotoka nilivaa nguo zangu kisha nikainua simu ya mezani iliyokuwemo hotelini humo kuangiza kifungua kinywa.
Haukupia muda sana mlango ukagongwa, nami nilifungua na kumuona dada aliyekuwa amebeba trei (chano) iliyokuwa imesheheni mazagazaga kwa ajili ya kifungua kinywa.
Kabla hajaondoka nilichukua noti moja iliyokuwa na rangi ya kaki na kumpa ikiwa ni malipo ya kifungua kinywa hicho.
“Haina haja ya kulipa maana kila kitu kimelipiwa.” Aliniambia mwanadada huyo.
Hata hivyo ili kumuonyesha kuwa nilikuwa ni bilionea mtarajiwa kwa wakati huo, nilimwambia achukue tu hiyo pesa kwani nilikuwa nimeshaitoa kwenye mahesabu. Naye bila kuvunga aliipokea, si alikuwa kapewa!
“Samahani dada yangu kama nitakukwaza, ningependa kulijua jina lako.” Nilijikuta namchombeza zikiwa ni harakati za kutaka kutangaza nia katika suala zima la mapenzi.
Bila kinyongo wala malingo msichana huyo alinionyesha jina lake kwenye kitambulisho chake cha kazi alichokuwa amekining’iniza shingoni.
Nililisoma jina na kujikuta naachia tabasamu.
“Kumbe unaitwa Anna, jina lako lina historia ndefu sana katika maisha yangu.”
“Historia gani tena kaka yangu?”
“Kwanza mama yangu mzazi alikuwa akiitwa jina hilo, pili kuna msichana ambaye nilitokea kumpenda kupita kiasi naye alikuwa akiitwa Anna, ni jina muhimu sana katika maisha yangu.”
“Kumbe! Basi na mimi naitwa hivyo!”
“Natabiri na wewe utakuwa na historia ndefu sana katika maisha yangu,”
“Yaweza kuwa!” Aliongea Anna na kuanza kunipa mgongo ili aondoke.
Bila kufikiri wala kuwaza nilijikuta naropoka kumuomba namba ya simu ama mawasiliano yoyote. Pale pale alinitolea kadi yake ya biashara (business card) iliyokuwa na kila aina ya mawasiliano aliyokuwa akitumia.
“Asante sana mrembo!”
“Usijali!” Alimalizia maneno hayo huku akifungua mlango na kuondoka zake.
Taratiibu kabisa nilijongea kwenye kimeza kilipokuwepo chano cha mapochopocho ya chakula cha asubuhi. Pasipo kuvunga nilikaa na kuanza kujichana kwa raha zangu. Kilikuwa ni kifungua kinywa cha haja, waswahili wa siku hizi wanakwambia ‘msosi draft’ulioenda shule.
Muda mfupi baada ya kumaliza kushambulia kifungua kinywa niliondoka kwa mwendo wa madaha mpaka kwenye mchuma wangu huku nikiwa nimening’iniza kibrificase changu mithili ya kibosile ama fisadi aliyefutuka tumbo kwa kuchakachua fedha za umma.
Mpaka nafika nje sikumuona Anna, nilitamani sana japo tupungiane mkono wa kuagana ili nimringishie gari langu la kifahari, lakini haikuwezekana. Nadhani alikuwa kwenye majukumu yake mengine hotelini hapo.

JE, BRIGHTON ATAMUONA TENA ANNA? NA KAMA ATAMUONA ATAMWAMBIA NINI? FUATILIA TOLEO LIJALO!

No comments:

Post a Comment