ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Alirudi
ndani haraka huku akiwa na hasira kisha akaufunga mlango kwa kuukomea ili
kumkomoa mtu aliyekuwa akileta ubishi pale mlangoni. Sikutaka kumuuliza
chochote kwani kama ningeongea basi sauti yangu ingesikika na kisha mpango wetu
kubumbuluka.
SASA ENDELEA..........
Alijitupia kitandani
huku akimlaumu mwanamke huyo kwa kuwa mbishi bila sababu. Huku akiwa bado
analalama, tuliuona mlango ukifunguka licha ya kukomea wakati anaufunga.
Pamoja na ubabe aliokuwa nao Benja alijikuta
akinywea baada ya kuona mlango unafunguka. Hakuendelea tena kubwabwaja badala
yake alibaki mdomo wazi huku hofu na woga vikimjaa.
Baada ya mlango
kufunguka msichana aliyekuwa anabishana na Benja mlangoni aliingia mpaka
chumbani. Kumbe alikuwa ni Sharifa, msichana aliyekuwa kanisababishia kufungwa
kisha kuniokoa dakika chache kabla ya kunyongwa kitanzini.
Sasa nilikuwa
nimeshaanza kumzoea msichana huyo.
“Ooh! Sharifa, kumbe ni wewe, samahani kwa
yote yaliyojitokeza kwani mwenzio nalazimika kuishi kama digidigi.” Nilimwambia
huku nikimlaki kwa kumkumbatia.
Wakati
huo Benja alikuwa aking’aang’aa sharubu tu, nikamtambulisha kwa Sharifa huku
tukiwa bado tumekumbatiana. Alishusha pumzi kwa nguvu na kurudi katika hali
yake ya kawaida.
“Mbona
unaishi kwa woga na wasiwasi hivi?” Sharifa alinitwanga swali hilo.
“Naogopa kugundulika kuwa nimetoroka jela,
maana jambo hilo tulilifanya tu kwa uwezo wako ila ni la hatari mno.” Nilijibu vile.
“Wasiwasi wako tu. Hakuna mtu yeyote
atakayekuuliza juu ya hilo hata kama uende gerezani hapo hapo.” Aliongea tena
Sharifa kunitoa wasiwasi.
Hata
hivyo maneno yake sikuyasadiki hata kidogo ila nilikubali ili yaishe.
Nilipomuomba tukae japo pale kwenye godoro ili anisaidie ushauri juu ya suala
lililokuwa linaumiza kichwa changu
alikataa. Akasema alikuwa amekuja kunichukua ili tuende kumalizia
maongezi yetu tuliyokuwa tumeyabakisha kule gerezani kabla ya kutoroka.
Nilipomuuliza
tunaenda kuongelea wapi aliniambia anajua yeye, nilichokuwa natakiwa kufanya ni
kumfuata kokote ambako ataniambia tuende.
Nilimuaga
Benja kisha tukaondoka na Sharifa. Sikuwa na nijualo juu ya safari hiyo. Tulipotoka nje ya nyumba alimokuwa kapanga
Benja tuliingia kwenye gari moja la kifahari ambalo alikuwa amekuja nalo
msichana huyo. Safari ya kuelekea nisikokujua ilianza huku dreva akiwa ni yeye.
Baada
kama ya nusu saa tulikuwa tupo kwenye hoteli moja mashuhuri sana mjini hapo.
Hoteli hiyo ilikuwa siyo ngeni kwangu japokuwa nilikuwa sijawahi kuingia ndani
zaidi ya kuliona jengo lake kwa nje nikiwa napita karibu nayo.
Wakati
tunashuka kwenye gari hiyo mara baada ya kufika hotelini hapo, Sharifa
alichukua ‘brificase’ na kushuka nayo akiwa kaishikilia mkononi.
Sikuelewa
kama tayari alikuwa kashalipia chumba au vipi kwa sababu tulipapita mapokezi
bila kusimama, tukaenda moja kwa moja kwenye lift. Tulipofika lift
ikatupandisha mpaka ghorofa ya saba, tukatembea kwenye korido mpaka kwenye
chumba namba 138.
Tulipofika
kwenye chumba hicho Sharifa alifungua mlango kwa kadi maalumu nao ukafunguka
kisha tukazama ndani. Chumba kilikuwa matawi ya juu kweli kweli, kila huduma
inayopatikana kwenye vyumba vya hoteli kubwa kubwa basi hata humo ilikuwepo.
Kimawazo
nilikuwa mbali sana wakati huo. Akili yangu ilikuwa inazunguka kuwaza ni
masharti gani nitapewa na msichana huyo ikiwa ni malipo ya kuniokoa kutoka
kwenye kunyongwa kwa kitanzi.
Mwili
wangu ulikuwa umezizima mithili ya mtu aliyetota kwa kunyeshewa mvua. Nilikuwa
mdogo kama pilton.
Tulipoingia
tulikaa kwenye sofa za nguvu, ndipo mazungumzo yetu yalipoanza.
“Brighton mwana wa David!” Sharifa alichokoza
mada kwa kuanza kuniita.
“Naam!” Niliitikia na kukaa kimya kusikilizia
kitachachoongewa.
“Bila shaka unapenda sana kuwa tajiri, maana umekuwa
ni mtu mwenye kujituma na kujishughulisha ukiwa na lengo la kuusaka utajiri!
Kweli ama si kweli?”
“Ni kweli, lakini utajiri ninaopenda mimi ni
ule wa kuupata kwa njia za halali zenye kumpendeza Mungu.”
Baada
ya kujibu hivyo nilimuona Sharifa akiangua kicheko cha dharau kisha akaendelea
kusema,
“hayo ni mawazo finyu ambayo hayataleta tija
katika maisha yako. Utajiri hauji kwa njia za halali hata siku moja na Mungu
hawezi akakuletea utajiri. Tangu lini kitu haramu kikaja kwa njia halali?”
Kauli
hiyo iliniacha njiapanda kidogo. Ikanifanya nirejee kwenye mafundisho ya dini
niliyoyapata nikiwa bado kinda wakati huo, mafundisho yaliyozungumzia matajiri
wa kale ambao miongoni mwao ni kina Ibrahim na kina Ayubu, mbona wao walikuwa
ni wacha Mungu wazuri tu?
Nikakumbuka
tena maneno ya Yesu kristo alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake kuwa ni vigumu
kwa tajiri kuingia kwenye ufalme wa Mungu kuliko hata kwa ngamia kupenya katika
tundu la sindano.
‘Je, maneno haya huenda ndiyo yanaashiria
anachokisema Sharifa?’ nilimalizia tafakuli yangu kisha nikatoa jibu kuwa si
matajiri wote wanaoupata utajiri kwa njia za mkato.
“Tuendelee!”
niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu, hivyo kama
unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali nitakayokuambia.”
Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua brificase iliyokuwa
mezani.
JE, NI MAMBO GANI BRIGHTON
ATAAMBIWA NA SHARIFA AMBAYO YATAMFANYA AWE TAJIRI? USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment