Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo
mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna
masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
“Tuendelee!”
niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.
“Huo ulikuwa ni utangulizi tu,
hivyo kama unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali
nitakayokuambia.” Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua
brificase iliyokuwa mezani.
SASA ENDELEA..........
Aliifungua
brificase na kuniambia niangalie. Naam! Ilikuwa imesheheni fedha za kigeni,
fedha ambazo zilikuwa zimebanwa katika maburungutu. Nilijikuta nikimeza mate
baada ya kuviona vitita hivyo.
“Kama
utakubaliana na ninachoenda kusema basi matumizi yako kwa siku yatakuwa ya pesa
kama hizi.” Mwanadada huyo alizidi kunitamanisha japokuwa nilikuwa sijajua
atakachokitaka kutoka kwangu.
Nilishusha
pumzi huku nikiongeza umakini wa kumsikiliza. Nilizidi kuwa katika wakati mgumu
kwa kujua kwamba kama nitamuendekeza sana msichana huyo basi pepo ya Mwenyezi
Mungu nitakuwa nimeipa kisogo.
Hata
hivyo nilijiambia ngoja kwanza nimsikilize, uamuzi si ulikuwa ni wangu bwana,
kama ningetaka kukubali basi ningekubali na kama ningetaka kukataa basi
ningekataa.
“Najua
mwanzo ulikuwa ukinichukia sana, hasa hasa pale niliposimama mbele ya mahakama
kutoa ushahidi juu ya kesi yako. Lakini sasa hivi hunichukii tena, hasa baada
ya kukuokoa kutoka kwenye kunyongwa, uongo?”
“Ni kweli.”
“Mateso yote uliyokuwa ukiyapata tangu kifo
cha marehemu kaka yako ulikuwa ukitumikia adhabu.”
Maneno
hayo yalinishtua na kunifanya nigutuke.
“Adhabu! Adhabu kwa kosa lipi? Na kosa hilo
nilikuwa nimemkosea nani?” Niliuliza.
“Kosa hukutenda wewe bali ni kaka yako James.”
“Alitenda kosa gani kaka yangu?”
“Usiwe na pupa, nipo hapa kukufunulia kila
kitu hivyo nitakueleza siri nzito aliyokuwa nayo kaka yako.”
Hilo
nalo lilikuwa neno; kujua kile kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia wakati wa
uhai wa kaka James, nilizidi kuongeza umakini. Kikao chetu kilizidi kutia fora,
sasa nikawa na shauku ya mambo matatu. Jambo la kwanza ni shauku ya kujua siri
nzito iliyokuwepo kwa kaka James.
Jambo
la pili lilikuwa ni shauku ya kujua masharti ambayo nilikuwa nimeambiwa
nitapewa wakati natoroshwa gerezani. Jambi la tatu ni shauku ya kutaka kujua
madhara yatakayonipata endapo ningeshindwa kutekeleza masharti hayo.
Sharifa
alianza kunieleza habari ya kaka James. Habari ambayo iliyaamsha machungu ya
moyo wangu, nikahisi maumivu makali yakipenya barabara kunako mtima wa moyo
wangu.
Kaka
James alipokuwa anamalizia masomo yake ya kidato cha nne aliambiwa na rafiki
yake mmoja kuwa kuna mganga wa kikongo aliyekuwa kaingia nchini. Mganga huyo
alikuwa akiwatengenezea watu dawa ya kupata utajiri.
Kutokana
na tamaa za kutaka kupata utajiri, kaka James alimtaka rafiki yake huyo
ampeleke kwa mganga huyo ili akatengenezewe dawa ya kuwa tajiri. Ndipo
alipopelekwa.
Alipofika
kwa mganga huyo aliambiwa kuwa masharti ya kupata utajiri ni lazima uingie
maagano na majini. Maagano hayo yalikuwa ni maagano ya kafara za damu huku
yakiwa katika madaraja matatu.
Daraja la kwanza
lilikuwa ni kuwatoa kafara wazazi wako wote pamoja na ndugu yako mmoja wa damu.
Ndugu aliyetakiwa katika daraja hili ni mdogo wako, kaka yako ama dada yako.
Kama wote hao huna basi mjomba ama shangazi hutakiwa.
Baada ya hapo utajiri
unaanza kwa kasi ya kawaida. Ukishakaa miaka mitano unatakiwa kutoa tena kafara
ya mtoto wako wa kwanza pamoja na mama yake kama wewe ni mwanaume. Lakini kama
ni mwanamke basi unatakiwa kumtoa mtoto wako wa kwanza pamoja na baba yake.
Ukishakamilisha
kafara za daraja la kwanza na la pili unatakiwa sasa kuhamia kwenye daraja la
tatu ambalo kafara yake huendelea mwaka hadi mwaka. Kafara katika daraja hili
ni ya mtu yeyote ama awe mfanyakazi wako au anayetumia vitu vyako mfano abiria
katika magari yako, mpangaji katika nyumba yako na kadhalika.
Masharti
hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia
kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika
ajali ya kutisha.
HAYA SASA, MAMBO NDO YANAFIKIA
PENYEWE, NINI KITATOKEA? USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment