Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa
gerezani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa
kumuua mpangaji wake kishoka. Hata hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na
kumtorosha huku akimwambia kuwa kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo
zoezi. Sasa Brighton tayari yupo uraiani na anachukuliwa na Sharifa na
kupelekwa kwenye hoteli na kuanza kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake
(yaani James) ulivyopatikana.......endelea
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Wakati nikiwa katika lindi la
mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.
SASA ENDELEA..........
“Usiwaze sana kwani kazi nzito ilishafanywa na
kaka yako, unachotakiwa wewe ni kuikamilisha tu na utakuwa bilionea wa
kuogopeka.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
“Daraja la kwanza
utakuwa umeshalivuka kwani wazazi wa James ni wazazi wako, pia kufa kwake
kutachukua nafasi ya ndugu wa karibu, kafara ambayo ilikuwa utolewe wewe.
Kitakachohitajika kwako ni kuoa mke kisha mkishazaa mtoto unamtoa kafara
akifuatiwa na mama yake, hapo utakuwa tayari umeshakamilisha daraja la pili.”
Alipozi kidogo.
Wakati wote huo
nilikuwa nimemsikiliza kwa makini. Baada ya kupozi kidogo aliendelea kuniambia
kuwa nikishaimaliza daraja la pili lile lililokuwa linafuata ni mteremko.
Daraja hilo ambalo ni daraja la tatu lilikuwa ni kumtoa kafara mtu mmoja kila
mwaka, mtu huyo anaweza kuwa ni mfanya kazi wako ama ni mteja wako. Hiyo hatua
ndiyo ilikuwa ni nyepesi kuliko zote kwani pale unamtoa mtu ambaye siyo ndugu
wa karibu.
Hata hivyo bado
ulikuwa ni mzigo mzito moyoni mwangu. Dhambi ya kuua nilikuwa naichukia na
nilikuwa sitegemei kabisa kuitenda katika maisha yangu.
Nilivuta kumbukumbu
ya maneno ya marehemu kipenzi changu Anna aliyoniambia kwenye ile ndoto niliyoota,
ndoto ya kutisha. Katika maneno yake alinisisitiza sana nisiue wala kujiua
kwani adhabu yake huwa ni kubwa mno.
Alinisisitiza nizidi
kutenda mema huku nikiongeza upendo kwa watu wote wanaonizunguka ili siku zangu
zikiisha duniani nikapumzike kwa amani na siyo kwa mateso.
Sasa mwanamke
aliyekuwa mbele yangu alikuwa ananishawishi nianze kuua kwa ajili ya kupata
utajiri, tena siyo kuua mara moja bali ni kuua kila mwaka mpaka pale maisha
yangu yatakapofika kikomo duniani. Niliogopa sana.
Kibaya zaidi jambo
lilikuwa limekaa kwenye njia panda, kama nisingefanya hivyo basi ningeuliwa
mimi. Kweli maisha ni matamu sana mithili ya asali mwitu japokuwa ni mafupi
zaidi ya watu wa Uturuki.
Hapo ndipo nilizidi
kuumiza kichwa. Lakini kumbukumbu ya maneno ya marehemu Anna ilionekana kunipa
nguvu. Nikajisemea kimoyomoyo kuwa ni bora nife kuliko kubeba dhambi mbaya na
nzito kama hiyo, dhambi ya kuua.
Nikiwa katika kuwaza
wazo lilinijia, nikaliona linafaa kulifanyia kazi. Nikataka kufumbua kinywa
changu ili nieleze msimamo wangu juu ya jambo lililokuwa lipo mbele yangu.
Kabla sijaongea chochote nilimuona Sharifa akisimama na kuniwekea mkono wake
kichwani. Mwili wote ulisisimka, nikajihisi kama nimepigwa shoti ya umeme.
Alipotoa mkono wake
juu ya kichwa changu aliniambia gari tuliyokuwa tumeenda nayo hotelini hapo
imekuwa yangu kuanzia wakati huo. Pia akaniambia pesa zote zilizokuwemo kwenye
brificase iliyokuwa mezani zote ni zangu.
Mara baada ya kuongea
hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua
alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.
**************************
ITAENDELEA..........
No comments:
Post a Comment