Kwa wasomaji wapya....
Brighton anajikuta akitupwa gerezani na kuhukumiwa adhabu
ya kunyongwa mpaka afe baada ya kusingiziwa kumuua mpangaji wake kishoka. Hata
hivyo mtu aliyemsingizia anaenda gerezani na kumtorosha huku akimwambia kuwa
kuna masharti atampa baada ya kukamilisha hilo zoezi. Sasa Brighton tayari yupo
uraiani na anachukuliwa na Sharifa na kupelekwa kwenye hoteli na kuanza
kuambiwa jinsi utajiri wa marehemu kaka yake (yaani James) ulivyopatikana.......endelea.
ILIPOISHIA TOLEO LILLOPITA...
Hayo
ndiyo mambo yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa
ya kaka yangu kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha
yake na ya wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila
Sharifa ndiye aliyekuja kuning’amua.
SASA ENDELEA..........
Pamoja na maelezo
hayo kuhusu kifo cha kaka James nilikuwa bado na maswali mengi sana kichwani
mwangu. Maswali menyewe ni pamoja na yeye Sharifa anahusika vipi na kafara hiyo
ama ana uhusiano upi na mganga wa kaka James?
Pia swali jingine
lililokuwa limetanda kwenye ubongo wangu ni kwamba mimi kosa langu lilikuwa ni
lipi hapo wakati aliyefanya maagano na mganga ni kaka yangu tu? Sikuwa na
majibu yake ila niliamini kuwa maswali hayo yangejibika kwa Sharifa.
Sikusita kumuuliza
kwani mpaka wakati huo nilikuwa nimemzoea na kumuona kama alikuwa ni mtu wa
kawaida wakati alikuwa si wa kawaida.
Nilianza na kutaka
kujua hao wataalamu hasa ni kina nani na wanapatikana wapi? Swali lilijibiwa.
Nikaambiwa kuwa wataalamu ni wale viumbe waliokuwa wamemuweka mganga huyo ili
aweze kufanya mawasilo nao katika kumpatia mtu utajiri aombapo. Sikutaka
kuendelea tena kudodosa juu ya swali hilo kwani tayari niling’amua kuwa
wataalamu hao ni majini ama pepo wachafu.
Nikahamia kwenye
swali la pili ambalo ni kutaka kujua Sharifa anahusikanaje na huyo mganga.
Alichonijibu wala sikukitila shaka, nikaachana na swali hilo mara baada ya
kupewa jibu.
“Na wewe una shirika
gani na yule mganga?”
“Ni mmoja kati ya wataalamu wake. Na mimi
ndiye nilichaguliwa kuhakikisha James anaaga dunia pamoja na kukuandama wewe
ili tukutie adabu, na ukiwa mgumu wa kuelewa utamfuata kaka yako aliko.”
Sikutaka
hata kuendelea kudodosa kwani majibu yenyewe yalikuwa yanajitosheleza. Tangu
mwanzo wa kuniandama mpaka kunitoa jela nilikuwa nimeshabaini kuwa Sharifa
hakuwa kiumbe wa kawaida. Alikuwa ni jini.
Hofu
ilizidi kujengeka alipotamka kauli ya kwamba hata mimi nikileta za kuleta
atanitia adabu ya kumfuata kaka James alikokuwa. Tafsiri ya maneno hayo ilikuwa
ni kwamba ataniua kwani James hakuwa Marekani wala Dubai bali alikuwa kuzimu.
“Kosa
langu hapo mimi ni lipi mpaka uniandame hivi?”
“Mirathi ya kaka yako.” Alijibu kwa mkato
kisha akafunga bakuli lake, yaani namanisha akanyamaza kimya.
Bado
kichwa changu kilikuwa na maswali ya kumhoji Sharifa. Mirathi ya kaka ilikuwa
imefanya nini? Nilizidi kuwaza kabla sijalitupia swali hilo kwa Sharifa.
Nilipomuuliza
alinijibu kuwa mali ya aina hiyo huwa haitakiwi kurithiwa na mtu yeyote yule.
Nilifanya kosa kubwa sana kurithi mali alizokuwa ameziacha kaka James wakati
zilikuwa ni za maagano.
Mpaka
hapo niliweza kuelewa kiini cha matatizo yangu. Nilijikuta nikianza kujuta
kurithi hizo mali pamoja na kuzaliwa pia. Niliweza kubashiri hatari iliyokuwa
inaninyemelea mbele yangu huku chanzo chote kikiwa ni mirathi ya kaka James.
“Kumbe
chanzo cha misukosuko yote hii ni hicho, sasa utanisaidiaje ili nijinasue
kwenye hili balaa?” Niliamua kumuuliza hivyo ili nijue hatima yangu.
“Dawa ya hapo ni moja tu”
“Ipi hiyo?”
“Kufanya yale yote tunayokutaka uyafanye,
zaidi ya hapo anza kujihesabu kuwa ni marehemu mtarajiwa.”
Hakuna
anayependa kufa jamani. Sikujua nifanye nini ili kujinasua kwenye urimbo
niliokuwa nimenasa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani. Sasa
nilizidi kuwa katika wakati mgumu.
Maelezo
ya mwanadada huyo hayakuwa na chembe ya utani ndani yake hata kidogo.
Alichokuwa anakisema alikuwa anakimaanisha. Uwezo wa kufanya hivyo alikuwa nao.
Tulibaki
tukiwa tumetumbuliana macho, mimi nikiwaza yangu kutokana na uzito wa jambo
ulivyokuwa. Nilikuwa najiona dhahiri ninavyodumbukia kwenye shimo lenye kina
kirefu nisiloweza kutoka tena.
Wakati
nikiwa katika lindi la mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa
kuniita jina langu.
“Brighton!”
“Naam!” Nami nilimwitikia.
“JE, SHARIFA ATAMWAMBIA NINI BRIGHTON? Tukutane
kwenye toleo lijalo.
No comments:
Post a Comment