ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Niliamua
kujinyamazia kwa kuhofia kupewa mikong’oto na maafande hao walioonekana kupinda
kuzidi maelezo. Alama za mia moja kumi na moja zilizokuwa zimejichora kwenye
mapaji ya nyuso zao kwa kukunja ndita zilikuwa zinanitisha.
SASA ENDELEA.......
Nilitulia
na kuamua kuvuta kumbukumbu mwenyewe ili niweze kung’amua kilichotokea na
kuniweka matatani kiasi kile. Kumbukumbu zangu zilianza kuniijia kwa mbaali,
nilijaribu kuwa makini ili niweze kuyakumbuka matukio yote yaliyokuwa
yametendeka tangu asubuhi kwenye mizunguko yangu.
Nilikumbuka
jinsi nilivyoshuhudia kioja cha mwanadada wa asubuhi, mwanadada aliyekaribishwa
na Kishoka akakataa kuingia ndani kisha nilipoenda kumwangalia sikumkuta.
Kumbukumbu zilizidi kutiririka sasa kwenye fikira zangu, nikakumbuka jinsi
nilivyoachana na kioja cha dada huyo na kuondoka zangu.
Ratiba
nzima ya mizunguko yangu nilifanikiwa kuikumbuka kwa marefu na mapana, niliendelea
kukumbuka nilivyopigiwa simu na Kishoka wakati narudi nyumbani akaniambia kuwa
mgeni wa asubuhi ananisubiri.
Mpaka nilipofika
getini na kuongea naye dada huyo kwa njia ya simu akiniaga kuwa anaondoka kwa
madai ya kuchoka kunisubiri, licha ya kumbembeleza kwa kumwambia kwamba
nilikuwa getini lakini bado mwanadada huyo aligoma kunisubiri.
Mpaka
naingia ndani kwangu sikuweza hata kumuona japokuwa nilitegemea ningekutana
naye. Kumbukumbu ziliendelea kutiririka mpaka nilipoingia chumbani kwangu na
kumkuta Kishoka kauawa juu ya kitanda changu.
Wakati
nikitafakari la kufanya watu wawili waliingia na kuniweka chini ya ulinzi. Hapo
ndipo kumbukumbu zangu zilifikia kikomo, sikukumbuka tena kilichoendelea zaidi
ya kujikuta nipo kwenye mahakama ya magonjwa, sehemu ambayo magonjwa yote
yanayowasumbua binadamu hushtakiwa na kutolewa hukumu, yaani namaanisha
hospitalini.
‘Sasa
nimeelewa, nitakuwa ninadhaniwa kumuua Kishoka. Muuaji atakuwa ni yule
mwanamke, lakini lazima nishakiwe mimi kutokana na mazingira ya kifo chenyewe;
kweli leo nimeamini kuwa akamatwaye na manyoya ndiye mwizi wa kuku.’ Nilijisemea
kimoyomoyo baada ya kukumbuka mkanda wa tukio zima.
Nilianza
kujuta kumfahamu msichana huyo, nilijilaumu mno kwa kumsemesha kule ufukweni
siku niliyoanza kumuona. Kama nisingemsemesha huenda yasingetokea haya, ama kweli
siku zote busara huja baada ya kutenda.
‘Hivi
tukio hili ni la kweli au naota?’ Niliendelea kuwaza.
‘Lakini hii siyo ndoto, hii ni ‘laivu’, tena
ni ‘laivu’ bila chenga.’ Nilijikuta nikijijibu mwenyewe.
Niliamua
kumwachia Mungu kwani yeye ndiye mweza wa yote, yeye ndiye alikuwa anajua
suluhisho la kesi iliyokuwa inanikabili, kesi ya mauaji ambayo sikuhusika nayo
hata kidogo. Nilijipa matumaini kuwa maadamu sina hatia basi Mungu atakuwa na
mimi.
“Afande,
kama vipi richukue maerezo maana tayari rimeshazinduka.” Alisikika afande aliyekuwa
ameshikilia bunduki akimwambia mwenzake ambaye alikuwa kashika faili mkononi.
“Hamna tabu afande, hata mimi nilikuwa
ninalifikiria hilo kichwani mwangu.” Alijibu afande huyo.
JE, KATIKA KUCHUKULIWA MAELEZO
BRIGHTON ATASEMAJE KUHUSU KUUAWA KWA KISHOKA? ITAENDELEA........
No comments:
Post a Comment