Monday, September 9, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 9



ILIPOISHIA........
“Utanisamehe kaka yangu kwa sababu nina haraka kwelikweli, ila usijali, nitakuja kwako kesho asubuhi!” Alinijibu bila ya kugeuka kuniangalia.
SASA ENDELEA.......
             Niligutushwa na kauli yake hiyo, kauli ya kwamba atakuja kwangu kesho asubuhi. Akili yangu ilianza kuwaza mara mbilimbili bila kupata jibu.
‘Nimeiona sura yake kwa macho yangu mawili ya damu na nyama, tena mchana kweupe lakini sijamfahamu, sasa iweje yeye awe anapafahamu mpaka nyumbani kwangu?’ Nilizidi kuwaza.
            Nilimuuliza kama anapajua ninapoishi naye akasema anapajua. Nikamuuliza kama ananifahamu mimi, akanijibu kuwa ananifahamu, tena kwa kukata mzizi wa ubishi alinitajia hadi jina langu,
“wewe si unaitwa Brighton mdogo wake na marehemu James!” nilizidi kuchoka.
            Chaajabu maongezi yetu yalikuwa yanafanyika huku tukiwa tunatembea, yeye yupo mbele na mimi nipo nyuma, nikajaribu kumbembeleza ageuke ili nimuangalie kwa makini huenda na mimi ningemtambua lakini hakukubali.
            ‘Huyu mrembo mbona simuelewi? Anadai ananifahamu, kwa nini sasa asisimame japo kidogo tusalimiane? Kama ananifahamu kweli na pia anapafahamu ninapoishi, kwa nini asisimame japo dakika sifuri tukasabahiana kisha akaendelea na safari yake?’ Niliwaza na kuwazua huku nikiendelea kuchapa lapa nikiwa nyuma ya mlimbwende huyo.
            Nilitembea kwa takribani dakika kumi nikimfukuzia msichana huyo lakini alikuwa hajakubali kunisubiri au kugeuka kuniangalia. Hakutaka kabisa kunielewa kwani kujikomba kwangu kote ilikuwa ni sawa na kumuimbia kiziwi ama kummulikia kipofu.
            Niliamua kuachana naye huku nikijipa matumaini kuwa kesho siyo mbali,
‘tena si kasema mwenyewe kuwa atakuja kunako anga zangu? Hahaaaa!’ Nilijikuta nikiangua kicheko cha dharau huku nikigeuka nyuma kuanza kurudi ufukweni.
            Nilitafuta mahali palipokuwa pametulia ili nijipumzishe, nieendelee kufurahia upepo murua unaovuma bila bughudha kandokando ya bahari.
            Mawazo ya ndoto ambayo nilikuwa nimeiota masaa machache kabla ya kwenda ufukweni yalianza kupotea. Nikaanza kuamini usemi wa baadhi ya watu wanaodai kwamba ufukweni ni sehemu ya kupotezea mawazo na kutuliza akili. Kwa wakati huo usemi huo nilikuwa siutilii shaka hata kidogo.
            Kichwa changu sasa nilianza kukiona ki chepesi, uzito kiliokuwa nao mara baada ya kugutuka kutoka ndotoni nikawa siuhisi tena. Niliamua kuanza kurudi nyumbani kwani machweo nayo yalikuwa yamewadia.

                                  *******************************
JE, HUYO NSICHANA NI NANI NA KAMJUAJE BRIGHTON? USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA.........

No comments:

Post a Comment