ILIPOISHIA........
Nilijaribu
kuangaza kwenye njia lakini sikuona mtu. Nikaamua kurudi ndani kuendelea
kushambulia boflo zangu na supu yangu ya kuku.
SASA ENDELEA.......
Wakati
namalizia zoezi nililokuwa nalo, zoezi la kupata kifungua kinywa, simu yangu ya
mkononi ilianza kuita. Niliangalia namba iliyokuwa inanipigia lakini nilishindwa
kuitambua, yaani ilikuwa ni namba ngeni ambayo haijahifadhiwa katika simu
yangu. Taratibu nilibofya kitufe cha kupokelea kisha nikapeleka simu sikioni.
Sauti
nyororo ilisikika kwenye spika za simu yangu, sauti iliyokuwa ikijitambulisha
kuwa ni mtu niliyeongea naye jana kule ufukweni. Nilipomuuliza yuko wapi aliniambia
yupo nyumbani kwao hivyo miadi yetu angependa iwe muda wa jioni.
Nilijaribu kumuuliza
kama alikuwa kaja nyumbani kwangu muda mfupi uliopita, naye aliniambia hajaja.
Pia aliongezea kuwa mpaka muda huo ananipigia simu alikuwa bado yupo kitandani
wala hajaachana na shuka.
Kwa
kweli nilianza kuchanganyikiwa upya, Kishoka alipoenda kufungua geti alimkuta
dada aliyedai kuwa nilionana naye jana kule ufukweni, huyo aliyenipigia simu
naye alijitambulisha kuwa nilikuwa naye ufukweni siku iliyopita.
Nilishindwa
kuelewa jinsi mambo hayo yalivyokuwa yakienda,
‘ufukweni mimi niliongea na msichana mmoja tu,
msichana ambaye alikuwa hataki hata kugeuka kunitazama. Sasa mbona wamefika
wasichana wawili wanaodai tumeonana ufukweni?’ Niliendelea kuumiza kichwa
nikiwaza juu ya tukio hilo la kushangaza na kustaajabisha.
Hata
hivyo nilishindwa kupata jibu. Niliishia kubetua mabega huku akili yangu
ikizidi kuchoka kutokana na maajabu hayo. Niliamua kuachana na suala hilo, nikaingia
chumbani kwangu kujiandaa ili nitoke kuelekea katika mizunguko ya kila siku
kwani tayari nilikuwa nimeshamaliza kustaftahi.
Wakati
nikiwa chumbani mlango wa chumba changu ulianza kugongwa. Nami nilienda
kufungua ili nimuone aliyekuwa anagonga. Nilimkuta Kishoka yupo pale mlangoni.
“Kaka umesema
ulipoenda getini hukumuona yule shori, mbona mpaka sasa hivi bado yupo?” Lilikuwa
ni swali la Kishoka aliloniuliza baada ya kufungua mlango.
Taarifa
hiyo ilizidi kunishtua, nikaanza kujawa na wasiwasi na hofu fulani. Hata hivyo
nilijikaza kiume na kumwambia Kishoka tuende wote mpaka getini tukahakikishe
kama kweli kuna mtu.
Tuliondoka
kuelekea getini, tulipofika hatukuona mtu yeyote, tuliangalia njiani lakini
hatukuona hata dalili za mtu kuondoka getini muda mfupi uliopita. Tulibaki
tukiangaliana bila kuongea chochote. Tukio hilo lilikuwa geni kabisa nyumbani
kwetu.
Pale
getini hapakuwa na sehemu ya kusema kwamba labda mtu huyo alikuwa anajificha,
palikuwa ni peupe kabisa. Sasa hata Kishoka naye alianza kuigiwa na wasiwasi.
Kutoka
hapo getini sikutaka hata kurudi ndani. Nilimwambia Kishoka akaufunge mlango wa
chumbani kwangu kisha anichukulie funguo zangu zilizokuwa zikining’inia kwenye
mlango wa chumba changu, naye akaenda.
Punde si punde
Kishoka alirudi na kunipa funguo zangu. Aliponikabidhi niliondoka zangu
kuelekea mitaani huku nikimuacha yeye yupo hapo nyumbani.
HAYA NDUGU MSOMAJI, MWANADADA
ANAZIDI KUWACHANGANYA AKILI BRIGHTON NA KISHOKA, JE NINI KITAENDELEA?
No comments:
Post a Comment