Tuesday, September 24, 2013

MIRATHI YA KAKA sehemu ya 21



ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.
SASA ENDELEA.......
            Baada ya maongezi hayo yaliyochukua takribani saa moja wakili huyo aliondoka zake na kuniacha nikirudishwa rumande kusubiri siku yingine ya kusomwa kesi yangu.
            Niliendelea na msoto wa rumande. Kila siku mlo mmoja kwa siku huku chakula chenyewe kikiwa ni ugali wa dona na maharage yenye uozo. Maisha hayo nilikuwa sijawahi kuishi hivyo ilikuwa ni vigumu sana kuyazoea.
            Hata hivyo sikuwa na jinsi, nililazimika kujikaza kisabuni huku nikisubiri kudura za Wahidi ziniokoe katika hilo janga. Ilikuwa inauma sana hasa pale nilipofikiria jinsi uhusiano wangu ulivyokuwa na mpangaji wangu Kishoka ambaye nilikuwa natuhumiwa kumuua.
            Tuliisha kwa ushirikiano mkubwa kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu huku kila mmoja akiwa na meno thelathini na mbili; yaani akiwa mtu mzima.
            Sikuhusika na kifo chake, lakini nilikuwa nikishtumiwa ya kwamba nilimuua. Kwa mtindo huo kwa nini sasa roho isiniume? Ilikuwa ni zaidi ya uchungu.
            Siku ya kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena iliwadia. Asubuhi asubuhi mimi na mahabusu kadhaa tulisweka kwenye karandinga la askari magereza huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza.
            Mara baada ya kufikishwa mahakamani tulishushwa huku tukilindwa kwa silaha za moto, siraha nzito nzito za kivita. Mapaparazi nao walikuwepo kama kawaida yao, wakaanza kutusonga ili wapate picha za kwenda kutuuzisha sura runingani na magazetini.
            Licha ya kukaripiwa na askari magereza waliokuwa wametutanguliza, mapaparazi hao walizidi kukomaa ‘kutufotoa’ na kamera zao. Tukaingia mpaka mahakamani tayari kabisa kwa kuanza kusomewa mashtaka yetu kila mmoja kwa awamu.
            Mimi ndiyo nilianzia kupandishwa kwenye jukwaa la watuhumiwa kisha nikaapishwa kama zilivyo taratibu za mahakama kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
            Baada ya kuapishwa kizimbani kesi yangu ilitajwa. Hata hivyo jaji Aneth Mwalukwa aliiahirisha tena kesi ili kusubiri jalada la kesi kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka. Kesi yangu ilipelekwa mbele kwa muda wa majuma matatu.
Niliteremshwa kizimbani na kurudishwa kwenye sello ya hapo mahakamani kusubiri mahabusu wengine wamalize kusomewa mashtaka yao kisha turudishwe rumande.
            Baada ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.
ITAENDELEA......

No comments:

Post a Comment