ILIPOISHIA........
Kushindwa
kwenda kumkumbatia ndugu yangu huyo wa damu kuliniumiza sana moyoni. Nilishindwa
kupata uhakika ya kwamba na yeye alikuwa kaniona au la! Tatizo hata kuongea
kwenyewe sikuweza, japo ningemuita kwa sauti natumai angenisikia.
SASA ENDELEA.......
Mtu huyu si mwingine
bali alikuwa ni kaka yangu James, ndugu wa damu tumbo moja japokuwa baba
tofauti. Mtu aliyeonyesha umuhimu mkubwa sana
baada ya wazazi wangu kufariki.
Hakupenda kabisa
kuniona nikihangaika ama kusumbuliwa na shida yoyote katika dunia hii, siyo
siri alinipenda sana kaka James.
Upendo ulioshibishwa
na udugu wetu ndiyo ulionifanya nimuone mtu muhimu sana chini ya jua. Kila
msaada niliomuomba alinisaidia, iwe wa kifedha ama wa kimawazo.
Kwa kuwa hata vikombe
hugongana kabatini; siwezi kusema kwamba mimi na James hatukuwa tukikoseana.
Pindi tulipokoseana tulisameheana bila kujali ukubwa ama udogo wa kosa jenyewe.
Msamaha wetu ulikuwa wa kweli pindi
tuliposameheana. Hakika tuliishi maisha ya amani na furaha siku zote, vicheko
na matani ya kawaida vilitawala kila tulipokuwa pamoja.
Hata kilipotokea kifo
chake sikuweza kujikaza, niliumia sana
moyoni mpaka nikafikia hatua ya kupoteza fahamu. Fahamu ziliniijia baada ya
masaa matano, nilipozinduka nikashangaa kujikuta nipo hospitali. Niliangaza huku
na huko bila mafanikio ya kumuona nesi wala daktari zaidi ya wagonjwa wenzangu
waliokuwa wamelala katika vitanda vyao kila mmoja.
Kumbukumbu za kifo
cha kaka James zilinifanya nishindwe kuutambua umuhimu wa drip ya maji
niliyokuwa nimetundikiwa na kuanza kukimbia kwenda kumzika kaka yangu mpendwa,
ndugu yangu wa pekee aliyekuwa mtegemewa katika maisha yangu.
James alichukua
uamuzi wa kujiua kutokana na kusalitiwa na mwanamke ambaye alikuwa ni mchumba
wake, mwanamke ambaye alimwamini kupita maelezo; akamnunulia nyumba ya kifahari
pia na gari zuri la kifahari. Wakaanza mikakati ya kuoana wakaishi pamoja
kwenye hilo jumba la kifahari waendelee kuponda mali
wakiamini kabisa kuwa kufa kwaja.
Moyo wa James uligongomewa
mwiba wa sumu alipomkuta mwanamke huyo yupo na kibwana kingine.
Kibaya zaidi mwanamke
huyo baada ya kufumwa alijibu utumbo kwa
James na kumwambia hamtaki tena wala hana mpango wa kuolewa nayeye.
Mpaka naingia
kaburini mwanamke huyo nitakuwa namfananisha na nyoka ndumilakuwili, tena
mwenye sumu kali. Hii yote ni kutokana na kupoteza dira ya maisha yangu kwa
kuiangusha nguzo niliyokuwa nimeegemea ambayo ni kaka James.
Mwanamama huyo
ilibidi amweleze bayana James kuwa hakuwa na mapenzi ya dhati kwake. Pia
alizidi kujifaragua kuwa alijifanya anampenda ili amchune kisawasawa. Baada ya
kuridhika kuwa amemchuna vya kutosha ; pesa, nyumba pamoja na gari , mwanamke
huyo aliamua kusema ‘byebye’ kwa kaka James na kukitangaza rasmi kimjamaa
alichokuwa nacho kuwa hicho ndiyo kimume chake kitarajiwa.
Maneno kama yale
yenye kejeli za kila namna yalimkasirisha sana
James. Hasira ziliuzidi uwezo wake wa kufikiri, na ndipo alipoamua kufanya
mauaji ya kinyama kwa mwanamke huyo
pamoja na kimjamaa kile kwa kuwatwanga risasi kila mmoja.
Alipomaliza kufanya
tukio hili, moyo wa woga ulimwijia hatiye ukauzidi uwezo wa kuamua. Akaona
suluhisho la tatizo lake
ni kujimaliza hata yeye
pia. Ndipo alipoamua kujifyatua risasi ya kichwa na kufa papo hapo.
Nikiwa bado
nimeukodolea macho umati wa watu waliokuwa wamefariki kitambo, akiwemo kaka
yangu James, machozi yalizidi kunitiririka mithili ya mto usiokauka kila msimu.
Nguvu za kumsogelea nazo sikuwa nazo, nikabaki nikisaga meno na kutikisa kichwa
huku niking’ata kidole changu cha shahada na kuendelea kutikisa kichwa. Kufanya
hivyo kote hakukusaidia chochote, mambo yalikuwa bado yako palepale, sikuweza
kuongea wala kunena chochote.
Nilipumua kwa nguvu, sijakaa sawa nikamtambua
mtu mwingine. Nilishindwa kujizuia baada ya kumuona mtu huyo, nikajikuta nikitabasamu.
Kutabasamu kwangu
hakukuashiria kuona mlango wa wokovu kwa tatizo lililokuwa likinikabili; tukio
lenye maajabu, vitisho na mikikimikiki ya kila aina. Kumuona tena huyo jamaa
ndiyo kulinifanya nitabasamu kwani nilikumbuka visa na vituko alivyokuwa
akivifanya kipindi cha uhai wake.
ITAENDELEA..........
No comments:
Post a Comment