ILIPOISHIA........
Punde
si punde Kishoka alirudi na kunipa funguo zangu. Aliponikabidhi niliondoka
zangu kuelekea mitaani huku nikimuacha yeye yupo hapo nyumbani.
SASA ENDELEA.......
Wakati wa jioni
nikiwa narudi nyumbani nilipitia sokoni kununua matunda, nikiwa sokoni nilimuona
msichana mmoja, msichana huyo alikuwa anafanana sana na yule niliyemuona kule ufukweni. Siyo kwa sura tu, bali mpaka
mavazi aliyokuwa amevaa siku ile ufukweni.
Nilimsogelea
na kumwambia dada mambo naye akanijibu poa. Baada ya kuisikia sauti yake nilibaini
kitu, sauti hiyo haikuwa na tofauti na sauti ya msichana aliyekuwa akinizingua
kule ufukweni, yaani sauti ileile ya mwanadada niliyekutana naye nikaanza
kumuita asikubali hata kunisubiri.
Sauti yake hiyo
iliyokuwa nyororo kiasi kwamba hata kama ulikuwa na homa ukiisikia tu unapata
afueni. Sauti ambayo husemekana inauwezo wa kumtoa chura mtoni aisikiapo.
Nilijikakamua
na kumuuliza kama alikuwepo ufukweni jana yake. Akakanusha kanu na kusema yeye
huwa hana kawaida ya kwenda ufukweni. Nilimuuliza tena kama ananifahamu mimi
naye akasema ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kuniona. Niliamua kuachana naye
baada ya kukumbuka usemi wa wahenga usemao kuwa duniani wawili wawili.
Lakini
sura yake, nguo alizokuwa amevaa pamoja na sauti yake havikuwa na tofauti hata
kidogo na yule msichana wa ufukweni. Nilibaki
kuwaza huku nikiendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani.
Nikiwa
njiani simu yangu ya kiganjani ilianza kuita, nikaitoa mfukoni na kuangalia
namba ya aliyekuwa ananipigia. Nilibaini kuwa kumbe alikuwa ni Kishoka, nilibonyeza
kitufe cha kupokelea kisha nikamsikiliza alichokuwa anasema.
“Kaka
uko wapi?” Aliniuliza nami nikamjibu nipo njiani kuelekea nyumbani. Baada ya
kumjibu hivyo aliniambia kuwa msichana aliyezuru kwetu asubuhi alikuwa kaja
tena na alikuwa ananisubiri. Nilimwambia nipo karibu kufika kisha nikakata simu
na kuirudisha mfukoni.
Nililazimika
kuongeza mwendo kama si kuanza ‘kutroti’ ili nimuwahi mgeni wangu niliyeambia
ananisubiria, mgeni ambaye tangu jana alikuwa ananizingua kule ufukweni. Wakati
mwingine woga flani ulianza kuniingia kutokana na maajabu aliyokuwa ananionyeshea
tangu asubuhi.
Nilipofika
mita chache kutoka kwenye geti la nyumba yangu simu yangu ilianza kuita tena,
nilipoiangalia namba niliikumbuka. Namba hiyo ndiyo iliyokuwa imetumiwa na
msichana huyo kunipigia asubuhi akidai miadi yetu iwe jioni.
Niliipokea
na kusikiliza kilichokuwa kinasemwa, mwanadada huyo alilalamika sana akidai
nimechelewa. Nilimwambia avute subira kidogo kwani mimi nilikuwa tayari nipo
getini kwa wakati huo.
Msichana huyo alikataa
katakata kuningoja akidai kwamba nimechelewa, muda aliokuwa ameutenga kwa ajili
ya miadi yetu ulikuwa umeisha.
Huku
nikifungua geti nilijitahidi kumsihi anisubiri japo kwa muda wa dakika sifuri
kwani nilikuwa nipo getini, hata hivyo aliendelea kushikilia msimamo wake akidai
ndiyo anaondoka ndani na hawezi kurudi tena.
Kauli hiyo ndiyo aliyomalizia
kuongea kisha akakata simu. Huku nimeshikilia simu mkononi nilifunga geti na
kuelekea ndani haraka haraka kumwahi mgeni wangu ambaye alikuwa kacharuka
kuondoka.
Nilijipa
matumaini kwamba ningekutana naye nje ya nyumba akielekea getini ama ningekutana
naye mlangoni. Na kama ningekutana naye basi ningejaribu kumbembeleza ili arudi
tena ndani japo dakika tatu ndipo aende zake, lengo langu ni kutaka kumuona
kwenye mwanga ili nimfaidi, nikishamuona basi hata aende zake.
Mpaka
nafika mlangoni sikukutana na mtu, nilifungua mlango na kuingia ndani nikijua
kuwa mgeni wangu huyo alikuwa kanielewa na kuamua kunisubiri. Wakati nafungua
mlango jicho lilikuwa ‘busy’ kuangalia kwenye sofa ili nimuone mgeni wangu.
HAHAAAA! HAPO PATAMU
MPENZI MSOMAJI, BRIGHTON ATAMKUTA HUMO NDANI HUYO MGENI WAKE? USIKOSE SEHEMU YA
13
No comments:
Post a Comment