ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Mpaka
nafika mlangoni sikukutana na mtu, nilifungua mlango na kuingia ndani nikijua
kuwa mgeni wangu huyo alikuwa kanielewa na kuamua kunisubiri. Wakati nafungua
mlango jicho lilikuwa ‘busy’ kuangalia kwenye sofa ili nimuone mgeni wangu.
SASA ENDELEA.......
Tofauti na matarajio
yangu, jicho langu halikuona chochote kwenye sofa, kulikuwa ni kweupe. Hapakuwa
na mgeni wala Kishoka lakini tv ilikuwa inawaka na redioni ilikuwa inasikika ZBC
radio ikiunguruma kwa mbaali, kituo cha radio ambacho mimi na Kishoka hupenda
kukisikiliza kila wakati. Hata kama tv iwe imewashwa, midundo ya ZBC radio
ilikuwa ikisikika kwa chini chini.
Ndivyo
ilivyokuwa hapo sebuleni kwa wakati huo, lakini aliyekuwa akisikiliza radio
wala kuangalia tv sikumuona. Nilijaribu kumwita Kishoka lakini hakuniitikia, nikaamua
kwenda mpaka kwenye chumba chake kumwangalia, niliukuta mlango umefungwa, nikajaribu
kugonga lakini sikujibiwa.
Nilijaribu
kuusukuma mlango nao ukafunguka, nikaangalia chumbani humo lakini sikuona mtu,
nikaamua kurudi tena sebuleni nikidhani nitakuta mabadiliko, nilipofika nilikuta
hali ni ileile kama ya awali, hapakuwa na Kishoka wala mgeni.
Nilipata
wazo la kumpigia simu Kishoka ili nimuulize alipo, nilipopiga simu ilianza kuita mpaka ikakata. Mlio wa
kupokelea wa simu hiyo ulisikika ukiita kwenye chumba changu. Nikabaki nikijiuliza
kuwa Kishoka kaenda kufanya nini chumbani kwangu, vilevile kwa nini sasa
alikuwa hapokei simu? Nilijiuliza kimoyomoyo baada ya simu kuita bila
kupokelewa.
Niliamua kwenda mpaka
chumbani kwangu kuona alichokuwa anakifanya Kishoka kiasi kwamba mpaka
anaichunia simu yangu. Nilianza kuhisi kuwa huenda alikuwa anafanya kamchezo
kachafu na mgeni wangu kwani naye kwa mambo hayo alikuwa hajambo, alikuwa
havumi tu lakini yumo.
Lakini bado kuna kitu
kilikuwa kinanichanganya, katika kumbukumbu zangu wakati natoka mlango ulikuwa
umefungwa na funguo nilikuwa nazo, hiyo simu ya Kishoka ilifikafikaje chumbani
kwangu? Kishoka mwenyewe alikuwa kaingiaje huko chumbani wakati funguo nilikuwa
nimeondoka nazo? Au asubuhi nilisahau kuufunga mlango? Nilibaki na maswali
ambayo majibu yake yangepatikana baada ya kumhoji Kishoka.
Shauku ya kutaka
kujua alichokuwa anakifanya Kishoka humo chumbani kwangu ilinikaa rohoni.
Nilikuwa nikiwaza mambo mia kidogo kabla ya kufika mlangoni;
‘huyu Kishoka yuko peke yake au yupo na huyo mgeni, maana mpaka naingia ndani
sijakutana naye wakati mara ya mwisho kuongea naye kwenye simu nilikuwa
nimekaribia getini kwangu. Angekuwa ni mtokaji basi ningekutana naye walau karibu
na geti kama siyo mlangoni.’
Nilipofika mlangoni nilibaini
kuwa mlango ulikuwa haujafungwa bali ulikuwa umerudishiwa tu. Nilizidi
kujiuliza kuwa umefunguliwaje wakati kipindi naondoka funguo niliondoka nazo? Nilizidi
kuduwaa.
Mara nilikumbuka kuwa
wakati natoka mlango sikuufunga mimi bali aliufunga Kishoka.
‘Kama alikuwa amesahau kuufunga au alikuwa
ameuacha kwa makusudi basi atakuwa kaingia kiulaini, lakini kaingia kufanya
nini chumbani kwangu? Bila shaka Kishoka anafanya matusi na mgeni wangu
chumbani kwangu.’ Mawazo yangu yalianza kunituma vile kwa wakati huo.
Ndipo nilipouona
mwanga wa taa ikiwaka chumbani, nikazidi kujawa na ghadhabu.
‘Wamewasha hadi taa utadhani ni chumbani kwao,
hizi sasa ni dharau. Kwa nini asimpeleke chumbani kwake?’ Nilizidi kujisemea
kimoyomoyo.
JE, KISHOKA ANAFANYA
NINI CHUMBANI KWA BRIGHTON? NA MGENI BADO YUPO HUMO NDANI AU VIPI? USIKOSE
SEHEMU YA 14.
No comments:
Post a Comment