ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Baada
ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya
magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.
SASA ENDELEA.......
Tukiwa
njiani moyo wangu ulizidi kuumia kwa kupotezewa muda kwa kesi ambayo
sijashiriki wala kuifanya. Akili yangu yote ilikuwa kwenye hatima ya hiyo kesi.
Mpaka tunafika kwenye ngome ya gereza nilikuwa nimezama kwenye mawazo mazito.
Nilighutushwa na sauti ya mlango wa karandinga ulipokuwa ukifunguliwa ili
tushuke. Tulishuka na kuswekwa kwenye gheto la watuhumiwa kuendelea na msoto.
Wiki
mbili zilikatika nikiwa rumande, niliziona ni nyingi sana. Hali yangu kiafya
ilizidi kuwa mgogoro kila siku iliyoenda kwa Mungu. Kudhoofu huko hakukutokana
na ugonjwa bali mawazo, aiseeeh! Acha kabisa kitu mawazo, tena mawazo ya kesi
ya mauaji ambayo hukushiriki hata kuitenda. Kila wakati nilijikuta nikichoka
kabisa.
Wakili
wangu alinitembelea tena siku moja kabla ya siku ya kwenda mahakamani.
Tuliongea mawili matatu huku akinipa moyo kwa kuniambia nitashinda tu na haki
itatendeka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
“Halafu
mbona umekonda sana?” Lilikuwa ni swali la Jonas Mlyanyama baada ya kuongea
mambo yetu muhimu yaliyokuwa yanahusiana na hiyo kesi yangu.
“Mawazo kaka, unajua kesi hii inanipa wakati
mgumu sana katika kichwa changu.” Nami nilimjibu.
“Acha kuwaza sana ndugu yangu, kwanza hii kesi
mimi hainipi presha hata kidogo. Hapo tutashinda tu.” Alisikika wakili Jonas
akiniambia.
Maneno
yake hayo niliyaona kama ya kunifariji tu ili niache kuwaza, lakini hatari
iliyokuwa mbele yangu ilikuwa kubwa mno. Piga ua kifo cha kunyongwa kilikuwa
kinaninyemelea. Suala la kuokoka lilikuwa adimu kama kaburi la baniani.
“Najaribu
kujikaza lakini najikuta nikiwaza tu, kila nikikaa mawazo yananijia, hata
usingizi nashindwa kupata, chakula nacho hakipandi hata kama kwa kukilazimisha.”
“Usijali ndugu yangu, amini nakwambia Mungu
yupo na atakusaidia.” Ilikuwa ni sentensi ya mwisho kutoka kinywani kwa wakili
Jonas Mlyanyama.
Bila
ya muda kupotea tayari nilikuwa mbele ya askari aliyekuwa akilalama kuwa
tumetumia muda mwingi kwa kupiga soga kama tumekutana sokoni.
Alinipeleka
moja kwa moja kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa lililokuwepo gerezani hapo.
Nikawakuta mahabusu wenzangu ambao tulikuwa tumeshaanza kuzoeana.
Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale. Hata
hivyo mimi mawazo yangu yote hayakuwa pale hata kidogo. Nilikuwa nikiwaza mambo
lukuki kwa awamu, mara namuwaza Kishoka, mara nawaza kesi yangu itakavyokuwa.
Wakati mwingine
taswira ya msichana aliyenisababishia matatizo hayo ilinijia kichwani mwangu;
msichana ambaye mimi ndiyo nilikuwa nikiamini kwa asilimia mia tano kuwa ndiye
alihusika na kifo cha Kishoka.
Hali
ya rumande ndugu yangu wee acha tu. Hata kama kungekuwa na masofa pamoja na
runinga mimi nisingeweza kuyafurahia kwani uhuru hamna.
Ilipofika
mida ya jioni vijana wawili waliletwa kwenye ‘sello’ tuliyokuwemo. Mahabusu
mmoja akaninong’oneza kuwa vijana hao walikuwa wameifanya rumande kuwa ni
maskani yao.
Kukatisha
mwezi hawajaswekwa humo ilikuwa ni vigumu kwao. Kila waliporudi uraiani baada
ya kumaliza kutumikia adhabu za vifungo walizokuwa wakipewa, vijana hao
walifanya makosa tena na kurudishwa rumande.
Niliwashangaa
sana baada ya kuambiwa kuwa walikuwa na kasumba hiyo. Sehemu mbaya kama ile wao
walikuwa wakiifurahia! Ama kweli kila shetani na mbuyu wake. Nilipojaribu
kuuliza kipi hasa ambacho huwafanya waione rumande kama maskani niliambiwa kuwa
ni ugumu wa maisha.
Kumbe
huo ndiyo ulikuwa ni mfumo wao wa maisha, si unajua tena huko kula ni bure na
kulala ni bure! Kwao siku zilisonga kwa mtindo ule.
Hata
hivyo mimi niliona ni ujinga na umbumbumbu uliokuwa ukiwasumbua. Mbona kuna
shughuli kibao huko uraiani ambazo wangefanya zingewapatia riziki ya halali.
Vijana
hao niliwafananisha na mazuzu ambao mishipa ya fikra ilishakatika kichwani
mwao. Rumande siyo sehemu ya kukimbilia kama una akili yako timamu.
*************************
ITAENDELEA........
No comments:
Post a Comment