ILIPOISHIA........
Nilipigwa na bumbuwazi baada ya
kufumbua macho kwani sikumuona Anna wala lile kundi la wale kina mzee Mboma.
Nilishangaa kujiona nipo kitandani kwangu kwenye chumba changu. Kumbe ilikuwa
ni ndoto tu.
******************
SASA ENDELEA.......
Nilikukuruka
huku nikihema. Kumbe nilikuwa nimepiga yowe kwa nguvu kabla ya kughutuka, yowe
hilo nililolitoa bila kujijua lilimfanya mpangaji wangu atoke chumbani kwake na
kuja kwenye mlango wa chumba changu kufahamu kulikoni. Nikiwa bado nahema
nilisikia mlango ukigongwa, nilijikaza na kuuliza ni nani aliyekuwa anagonga.
Sauti ya Kishoka
ilisikika ikinijibu, taratibu niliinuka kwenda kufungua mlango baada ya
kung’amua kuwa mgongaji wa mlango ni mpangaji wangu.
Baada
ya kumfungulia aliniuliza,
“kulikoni kaka, mbona umepiga yowe kwa nguvu
sana, ni nini kimekusibu?”
“Kaka mimi nilikuwa nimelala, wakati nimelala
nikaota ndoto lakini siikumbuki!” Hilo ndilo lilikuwa jibu langu kwa swali la
Kishoka.
“Basi utakuwa umeta ndoto ya kutisha sana
maana makelele uliyokuwa unapiga yalikuwa siyo ya kawaida.” Aliniambia kwa
sauti iliyojaa kila aina ya upole.
“Ndoto
niliyoota ni ya kutisha lakini sikumbuki jinsi ilivyokuwa, isitoshe huwa sina
kawaida ya kuota mchana.” Nilimalizia kwa kushusha pumzi huku akili yangu
ikijaribu kurudisha kumbukumbu nyuma.
Kumbukumbu
zilianza kunijia kwa mbaali sana, zikawa zinakuja na kuondoka utadhani
‘network’ ya simu zilizochakachuliwa, simu zinazouzwa na matapeli chini ya
mnara. Katika kukumbuka nilianza kukumbuka kuwa nimemuona marehemu Anna
ndotoni.
Akili
yangu sasa ikawa ‘busy’ zaidi ya ‘customer care’ wa mtandao wa simu wenye
wateja lukuki wanavyokuwaga. Nilizidi kuvuta kumbukumbu juu ya ndoto niliyoota,
ndoto ya kutisha ambayo nilikuwa nimeiota muda mfupi uliopita nilipokuwa nimelala,
ndoto ya mchana.
Mara
nikaikumbuka yote, nikaanza kumsimulia Kishoka ndoto hiyo ilivyokuwa, nilimsimulia
mwanzo mpaka mwisho.
Nikamsimulia jinsi
ndoto yangu ilivyokuwa imetawaliwa na watu waloikufa kitambo, tena vifo vyao ni
vya kujiua kila mmoja. Kipenzi changu Anna, Kaka James, mzee Mboma, Patrick
pamoja na watu wengine lukuki ambao sikuweza kuwatambua niliwashuhudia kwenye
hiyo ndoto .
Kishoka
akaniambia kuwa hiyo ni ndoto tu kama zilivyo ndoto zingine. Alianza kwa kunifafanulia
tafsiri ya neno ndoto; akaniambia ndoto kwa jina jingine huitwa njozi ama ruya.
Aliendelea kuniambia
kuwa ndoto ni mkusanyiko wa mawazo makuu yaliyokuwa yametawala katika kichwa
cha muotaji kipindi hajalala ama siku za nyuma. Akili inapokuwa imepumzika
wakati mtu yupo usingizini kichwa huweza kukumbuka matukio hayo na kuyaundia
picha ambayo huwa kama tukio halisi.
Maelezo
ya Kishoka hayakuniingia akilini kabisa, nikamkubalia tu ili turudi kwenye
pointi yetu ya msingi, yaani fasiri ya ndoto niliyokuwa nimeota. Nilimuuliza ndoto
hiyo ina maana gani?
Hata
hivyo alinijibu kuwa yeye siyo bwana njozi, lakini alivyokuwa anahisi ni kwamba
akili yangu itakuwa imetawaliwa sana na kuwawaza watu wawili, watu ambao hata
kwenye ndoto hiyo nilikuwa nimewaota, yaani marehemu kaka James pamoja na
mpenzi wangu wa zamani marehemu Anna.
Kuondokewa
na watu hawa katika maisha yangu kulikuwa kumeniathiri sana kisaikolojia na
ndiyo maana nikawaota. Hivi ndivyo Kishoka alivyoning’amua.
Nilimuuliza
kuhusu mzee Mboma, Patrick na wengineo ambao sikuwatambua; sikuwa na mawazo
sana juu yao, wengine nilikuwa sijawahi hata kuwaona. Sasa kwa nini nao
waonekane kwenye ndoto yangu? Kweli sikatai kuwa kifo cha mpenzi wangu na kaka
yangu kilikuwa kimeniathiri sana kisaikolojia, lakini siyo hao wengine, sasa kwa
nini nao niwaone?
Jibu
alilonijibu Kishoka ni kwamba hakuna mechi isiyokuwa na washangiliaji, pia
akaongezea kuwa hakuna ‘muvi’ inayochezwa na kinara peke yake, lazima pawepo na
wahusika waalikwa. Hivyo wahusika wakuu wa ndoto yangu walikuwa ni Anna na
James, wengine wote walikuwa wahusika wadogowadogo. Mpaka hapo nilikuwa nimemuelewa
kwa kiasi fulani.
Aliniacha
na kwenda zake, nikiwa bado nipo kwenye kitanda changu cha sita kwa sita, niliendelea
kuitafakari ndoto ambayo nilikuwa nimeiota muda mfupi uliopita. Maneno ya Anna
yenye ujumbe mzito yalizidi kujirudia kichwani mwangu.
JE, NINI KTATOKEA BAADA YA
HAPO? ITAENDELEA.......
No comments:
Post a Comment