ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Afande huyo nilimuona akifunga
faili lake na kuniambia nijiandae kwenda kuozea jela. Alichodai ni kwamba laiti
kama ningeeleza ukweli basi angeweza kunisaidia.
************************
SASA ENDELEA.......
Nikiwa
rumande machozi yalizidi kunitiririka bila kukauka utadhani chemichemi za mto
Naili, chemichemi ambazo hutiririka bila kukauka misimu yote; iwe masika ama
kiangazi. Mifereji ya machozi ilikuwa inatiririka kutoka machoni ikipitia
mashavuni mpaka kwenye kidevu.
Harufu
mbaya ya humo kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa ilinifanya nipige chafya mara kwa
mara. Nilijaribu kujikaza kiume nijizuie kulia lakini cha ajabu machozi yalizidi kunitoka. Nilikuwa sijawahi kuswekwa
rumande hata siku moja tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia.
Siku
niliiona kama haiendi, masaa nayo yalikuwa kama yamesimama. Tangu saa tano za
asubuhi baada ya kuruhusiwa hospitali niliingia humo, mpaka muda huu ambao nilikuwa nauhisi ni kama
saa tisa za jioni nilikuwa nimeiva sawasawa. Kwa muda mchache huu ambao nilikuwa
nimekaa ndani nilikuwa najiona kama
nimekaa mwezi mzima.
Mawazo
kibao yalikuwa yametawala kichwa changu; niliwaza biashara zangu zitasimamiwa
na nani, zaidi ya yote kilichokuwa kinaniumiza kichwa ni hatima ya kesi yangu
iliyokuwa inanikabili, kesi ya mauaji.
Ilipofika
usiku nilizidi kuipata freshi, tena ni freshi ya mwaka. Sulubu iliyokuwemo
kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa haielezeki, yaani ni sulubu ya kufa mtu. Hapo
ndiyo nilianza kuamini kuwa kweli rumande siyo kanisani ama msikitini.
Mbu
walinishambulia si mchezo, nilijaribu kuwaua mmoja baada ya mwingine lakini wakawa
hawaishi wala kupungua, suala la kupata usingizi walau dakika moja lilikuwa ni
ndoto; tena ndoto yenyewe ni ndoto ya kuota mchana kweupe.
Siyo
mbu peke yao walionipa kero usiku huo, kunguni na viroboto nao walizidi kuleta
adha katika mwili wangu.
‘Kama rumande ya polisi tu hali ndiyo hii,
kule gerezani sasa hali ikowaje?’ Nilizidi kutafakari huku nikiwa ‘buzy’
kupambana na wadudu hao wasiyokuwa na chembe ya adabu hata kidogo.
Niliwatumbua
kwa hasira kila nilipowabahatisha wakigema damu yangu, lakini nao ndiyo kwanza
walizidi kuongezeka utadhani walikuwa wakialikana.
‘Kwa mtindo kama huu kufikia asubuhi nitakuwa
nimepoteza lita kadhaa za damu katika mwili wangu. Lakini chanzo cha mateso
haya yote ni yule msichana aliyemuua
mpangaji wangu Kishoka.’ Niliendelea kunung’unika peke yangu. Manung’uniko
ambayo hayakuzaa matunda ya wokovu wa kesi yangu hata kidogo.
Hayawi
hayawi mwisho yakawa, jogoo la kwanza nililisikia likiruka ‘bonanza’ kuashiria
alfajiri inawadia. Mara nilisikia jogoo la pili na hatimaye la tatu. Kulionekana
kupambazuka huku nikiumaliza usiku kwa kuutoboa, yaani namaanisha sikusinzia
hata sekunde moja zaidi ya kupepesa macho pale ilipobidi.
Ikawa
asubuhi, siku ambayo sikujua itaishaje. Nilitegemea kupandishwa kizimbani kwa
mara ya kwanza ili kusomewa shauri lililokuwa linanikabiri. Lakini mambo yakawa
sivyo.
Mara mlango
ulipofunguliwa niliwaona askari wawili waliokuwa wameshikilia bunduki kila mmoja
wamesimama mlangoni kisha wakanitaka nitoke. Nilipotoka walinifunga pingu
mikononi kisha wakanitanguliza mbele mpaka kwenye chumba kimoja katika kituo
hicho kisha mahojiano yakaanza upya.
ITAENDELEA.....
No comments:
Post a Comment