Sehemu ya kwanza.
Kiza kinene kilikuwa
kimetanda pande zote za dunia, sikuelewa kama nipo peke yangu ama tupo
wengi kutokana na kutoona umbali hata wa
sentimita moja mbele yangu.
Nilifikicha macho na
kutazama huku na kule,
‘Mungu wangu! Nipo wapi huku, nimefikaje
na nimefika saa ngapi?’ Nilishindwa kupata jibu.
Nilikodoa macho kwa
nguvu kama mtu aliyeshikwa ugoni; bado nilikuwa sioni chochote mbele ya mboni
za macho yangu zaidi ya weusi wa giza totoro lililokuwepo.
Niligeuka kushoto sikuona
chochote, nikageuka kulia pia sikuona chochote. Niliamua kugeuka mzimamzima,
bado sikupata picha hata kidogo, moyo wa woga ulianza kuniingia, nikataka kukimbia lakini nikashindwa.
Nilipojaribu
kunyanyua mguu wangu wa kuume nipige hatua kuelekea mbele, mguu ulikuwa mzito.
Ndipo nilipogundua
kuwa nguvu zimeniishia, viungo vyote vya mwili nilivihisi vimelegea; vilikuwa vimekufa ngazi kabisa. Nilibaki
nikitetemeka palepale, nikajaribu kufumbua kinywa changu angalau nipige yowe la
kuomba msaada. Hata hivo nilijikuta nikishindwa kuongea, nikaishia
kumung’unyamung’unya maneno utadhani anaongea bubu vile. Kinywa kilikuwa kizito
kufumbuka.
Kijasho chembamba
kilianza kunitoka, nikajikuta nimelowana chepechepe mwili mzima utadhani
nimemwagiwa maji. Ghafla nikadondoka chini mzimamzima, nikaanguka puu kama gunia la mtama liangukavyo
linapotupiwa chini hasahasa na mtu mzembe ama aliyechoka kubeba.
Nilianza kuona mwanga
mweupe, mwanga huo ulikuwa ni mkali mara kumi zaidi ya ule wa radi; mwanga huo
ulizidi kujirudiarudia.
Ghafla mwanga ulisitisha kumulika; mara
nikamuona mtu mbele yangu, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu iliyong’aa japokuwa
gizani. Nilijaribu kuinua kichwa changu nimwangalie huenda nitang’amua
kuwa ni nani.
Nilijikuta nikipigwa
na butwaa baada ya kuinua macho yangu kwani nilimuona mtu huyo ni wa ajabu mno.
Ni miaka ishirini na saba sasa tangu nizaliwe lakini sijawahi kuona mtu mrefu
namna hii hapa chini ya jua. Nilijaribu kukifuatilia kiwiliwili chake ili nione kichwa chake
kilipoishia .
Niligundua kuwa mtu
huyo alikuwa ni mrefu kuzidi maelezo kwani nilishindwa kuuona mwisho wake.
Sijakaa sawa mtu huyo
akapotea, nilibaki nikiwaza bila kupata jawabu. ‘Nitasalimika kweli leo?’
Nilijiuliza kimoyomoyo bila kutoa sauti. Nikaangaza pande zote, giza lilikuwa
bado lipo palepale. Nilijaribu kuinuka ili nikimbie, hata hivo nilishindwa kwa vile mwili ulikuwa bado hauna
nguvu.
Sauti za ngurumo kama
za radi zilianza kusikika kwenye ngoma za masikio yangu. Zilizidi
kujirudiarudia kabla ya kusindikizwa na tetemeko kubwa la ardhi. Nilihisi ardhi
yote inatikisika, woga ukazidi kuongezeka. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda
kasi zaidi.
‘Nitapona kweli leo?’
Huu ni mfano wa baadhi ya maswali yaliyokuwa yanaisumbua akili yangu kwa
wakati huo. Nilikosa majibu ya maswali yangu, nikaishia kujisemea kuwa Mungu yupo.
Itaendelea......
No comments:
Post a Comment