ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
Pumzi
zilianza kuniishia, nikajikuta nikipumua kwa shida huku kifua changu kikianza
kubana. Sijakaa sawa nikaanza kuhisi kama kizunguzungu na kuhisi kama nataka
kuanguka. Mpaka hapo nilipoteza ‘network’ na kujikuta sijitambui hata kidogo.
**********************
SASA ENDELEA.......
Fahamu zilinijia kama
mtu aamkapo kutoka usingizini. Kitanda nilichokuwa nimelalia si kile nilichokizoea,
kitanda chenye godoro la Dodoma ambacho ni futi sita kwa sita.
Kitanda nilichokuwa
nimekilalia kwa wakati huo kilikuwa ni tatu kwa sita,
‘piga ua hiki siyo kitanda changu.’ Nilijikuta
nashikilia msimamo huo.
Huku
nikipepesa macho niligundua kitu kingine, humo ndani kulikuwa na vitanda lukuki
vilivyokuwa vinafanana. Harufu ya dawa nilianza kuisikia, hapo ndipo nilipong’amua
ya kuwa nipo hospitali.
Huku
nikipiga miayo, nilitaka kupeleka mkono wangu wa kuume usoni kujaribu kupangusa
tongotongo endapo zipo, mkono uligoma kwenda. Nikaanza kujiuliza ni kwa nini
mkono wangu unang’ang’ania kwenye chuma cha kitanda?
Kabla
sijaangalia kilichokuwa kinakwamisha mkono wangu wa kulia kunyanyuka, nilitaka
kutumia mkono wangu wa pili kusafisha macho yangu, nao ulikuwa mzito kiaina.
Huku maruweruwe
yakififia kwenye mboni za macho yangu, niliinua kidogo kichwa changu kuangalia
kilichokuwa kinaufanya mkono wangu wa kushoto uwe mzito kunyanyuka. Ndipo nilipojionea
sindano kubwa ikiwa imeunganishwa na mrija wa plastiki ambao unaelekea kwenye
nguzo ya chuma iliyokuwepo karibu na kitanda nilichokuwa nimelazwa.
Nilipoufuatilia
mrija huo mpaka ulipoishia nilijionea drip ya maji imetundikwa, huku maji hayo
yakitoja taratibu na kuingia kwenye mrija huo kisha kuteremka mpaka kwenye mkono
wangu.
‘Nimetundikiwa
drip ya maji, ni nini kimenisibu mpaka nikafikishwa hapa?’ Nilibaki nikijiuliza
bila kupata majibu ya swali langu hilo.
Wazo
la kuangalia kilichokuwa kinaufanya mkono wangu wa kulia ung’ang’nie huko
kwenye chuma cha kitanda lilinijia, nikageuza shingo yangu kiasi kwamba mpaka nikaweza
kuona kwenye chuma cha kitanda nilichokuwa nimelalia. Moyo uliruka baada ya
kukiona kilichokuwa kimeufanya mkono wangu ugande kwenye chuma hicho.
‘Nimefungwa
pingu! Ni kosa gani nililofanya mimi mpaka nikafikia hatua ya kulazwa hospitali
huku nikiwa nimefungwa pingu. Mimi siyo jambazi na wala huwa sina fikra za kuja
kuwa, sasa iweje leo nifungwe pingu mithili ya jambazi aliyeshindikana kisha
akakamatwa kwa bahati mbaya?’ Fukuto la maswali mengi lilizidi kukisumbua
kichwa changu na akili yangu kwa ujumla.
Katika
kuangaza angaza niliwaona askari wawili waliokuwa wamekaa karibu yangu huku
mmoja akiwa ameshikilia mtutu.
‘Ama
kweli huu ‘msala’ si wa kitoto, nimewekwa chini ya ulizi kwa silaha za moto,
hivi nimefanya kitu gani mimi?’ Nilijaribu kuwaza na kuwazua ili nifahamu
kilichokuwa kimenisibu lakini ikawa ‘holla’.
Nilijikakamua
na kuamua kuwauliza hao hao waliokuwa wameniweka chini ya ulizi.
“Samahani afande, hivi ni tukio gani
nililofanya mpaka mmeniwekwa chini ya ulinzi ndani ya hospitali?” Nililibwaga
swali hilo kwa maafande hao ambao sura zao zilikuwa zimekunja ndita si mchezo.
“Unajifanya
hujui urichokitenda? Acha kuuriza maswari yasiyokuwa na tumbo wara mgongo mura.”
Alisikika askari ambaye alikuwa kashikilia cha moto huku rafudhi yake
ikinidhihirishia waziwazi kuwa ni mtu wa Mara, yaani mkurya. Tena alinijibu kwa
sauti ya ukali utadhani kanishika ugoni kwa mkewe.
Niliamua kujinyamazia
kwa kuhofia kupewa mikong’oto na maafande hao walioonekana kupinda kuzidi
maelezo. Alama za mia moja kumi na moja zilizokuwa zimejichora kwenye mapaji ya
nyuso zao kwa kukunja ndita zilikuwa zinanitisha.
NINI KITAENDELEA! SEHEMU YA 16 SI
YA KUKOSA!
No comments:
Post a Comment