ILIPOISHIA........
‘Ama
kweli leo ndiyo leo, ngoja nisubiri hatima yake.’ Niliwaza kimoyomoyo huku
mdomo ukiendelea kuwa wazi, kamasi pamoja na machozi vilianza kunitoka hata sikuwa
na muda wa kuviondoa badala yake nilizidi kuviachia vitiririke mpaka basi.
SASA ENDELEA.......
Mrembo Anna,
niliyezoea kumuita ‘queen’; msichana aliyekuwa amefanikiwa kuuteka moyo wangu
kwa kiasi kikubwa, siku hiyo alikuwepo mbele yangu. Msichana niliyemuamini
kiasi kwamba niliapa kumzika endapo asingenizika. Tena aliniahidi kunitunzia
zawadi adimu, zawadi ambayo wasichana wengi wa siku hizi wamepungukiwa, zawadi
ya usichana wake ama bikira yake. Hakika nilikuwa naingojea kwa hamu kubwa.
Zawadi hiyo alikuja
kuipoteza pasipo yeye kutaka; siku ambayo alimsindikiza dada yake kwenye
‘birthday’ ya mpenzi wake. Walipofika huko mambo yalikuwa ndivyo sivyo;
alitokea kijana mmoja ambaye alimtaka kimapenzi.
Anna hakuwa tayari
kwa vile alikuwa akinipenda na kunithamini pia. Hakutaka kabisa kunisaliti wala
kumzawadia kidume mwingine yeyote tunu adimu kama
ile. Kikombe kile kilikuwa ni halali yangu kukivunja.
Kwa kuwa mazingira
yenyewe yalikuwa hatarishi, msimamo wa Anna haukuzaa matunda yoyote. Kijana
huyo aliamua kutumia ubabe baada ya sera zake kugonga mwamba, na kweli
alifanikisha. Aliamua kumbaka Anna, kitendo ambacho kiliyavunja maagano yetu.
Baada ya Anna
kunieleza habari hizo, habari ambazo zilileta msiba mkubwa ndani ya moyo wangu,
nilimuomba anipe muda wa wiki mbili kabla ya kutoa uamuzi wangu juu ya hiyo
hujuma ya tunu yangu. Vilevile nilitoa shinikizo la kwenda kupima virusi vya
ukimwi baada ya miezi mitatu.
Wakati tukisubiria
miezi mitatu ikamilike ili tuende kupima VVU, nilipokea taarifa za kifo cha
mpenzi Anna, taarifa ambazo zilionekana kuuchoma moyo wangu mkuki wenye sumu
kali.
Anna alipoteza uhai
wake baada ya majaribio ya kuitoa mimba aliyoipata siku aliyobakwa. Kabla mauti
hayajamfika aliandika ujumbe uliosisitiza kuwa ataendelea kunipenda hata huko aendako.
Anna sasa alikuwa
yupo mbele yangu, nilitaka kumnyoshea mikono nimuite japo kwa ishara. Hata
hivyo nilishindwa kutokana na kukosa nguvu katika mikono yangu.
‘Sasa Anna atajuaje kuwa nipo karibu yake,
tena nimemuona!’ Nilizidi kuchanganyikiwa huku nikiwaza vile.
Bila kutegemea nilimuona
akinisogelea, moyo wangu ulianza kufarijika kidogo kidogo. Nikaanza kujipa
matumaini ya kwamba huenda nitapata kuongea na Anna wangu.
Nilimsubiria kwa
shauku kubwa. Alinisogelea hadi akanikaribia, sasa alikuwa yupo umbali wa kama
mita tatu hivi kutoka nilipokuwa. Alizidi kutoa kilio cha kuomboleza, nikaanza
kumuonea huruma mpenzi wangu wa tangu zamani, tulikuwa tukipendana ila kifo
ndicho kilichotutenganisha.
Alifungua kinywa
chake na kuanza kunena,
“mpenzi
wangu Brighton, najua nilikukosea sana, na siyo wewe peke yako bali hata jamii
kwa ujumla. Huko tuliko tunateseka sana,
tena mimi nateseka mara mbili ya wenzangu. Kawaambie binadamu huko duniani kuwa
kuua ni dhambi kubwa mno, adhabu yake ni kali kupita maelezo.” Aliongea kwa
masikitiko makubwa huku akionekana ni jinsi gani alivyokuwa anaugua moyoni.
Nilitaka kumuuliza
swali, tatizo nilikuwa bado siwezi kuongea. Nilibaki nimemwangalia bila ya
kupepesa macho. Aliendelea kunihubiria,
“adhabu yangu imekuwa tofauti na za wengine
kwa sababu niliua mara mbili, nilikiua kiumbe kilichokuwamo tumboni mwangu
kisha na mimi nikajiua. Japokuwa uhai niliupoteza baada ya kupoteza damu nyingi
nilipotoa mimba, kitendo hicho kilinifanya nihesabike kuwa nilijiua; kosa
ambalo ni la kuua.
Usijaribu kabisa kuua
wala kujiua. Yeyote afanyaye hivyo makazi yake ni hii sehemu tuliyopo.
Brighton; kazidi kutenda mema duniani ili siku zako zitakapoisha ukapumzike kwa
amani na siyo kwa mateso kama tunavyopumzika sisi.”
Ghafla mwanga kama wa
radi ulitokea alipokuwa amesimama Anna. Ukali wa mwanga huo ulinifanya nifumbe
macho. Nilipigwa na bumbuwazi baada ya kufumbua macho kwani sikumuona Anna wala
lile kundi la wale kina mzee Mboma. Nilishangaa kujiona nipo kitandani kwangu
kwenye chumba changu. Kumbe ilikuwa ni ndoto tu.
******************
ITAENDELEA.......
No comments:
Post a Comment