ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA......
“Afande,
kama vipi richukue maerezo maana tayari rimeshazinduka.” Alisikika afande aliyekuwa
ameshikilia bunduki akimwambia mwenzake ambaye alikuwa kashika faili mkononi.
“Hamna tabu afande, hata mimi nilikuwa
ninalifikiria hilo kichwani mwangu.” Alijibu afande huyo.
SASA ENDELEA.......
Mara
nilimuona afande huyo aliyekuwa kashikilia faili mkononi akivuta kiti chake na
kusogea karibu kabisa na pale nilipokuwa nimelaza kichwa changu. Alifungua
faili lake huku akiwa kashikilia kalamu mkononi.
Alianza
kunihoji maswali kuhusiana na tukio zima la mauaji ya Kishoka, kila
aliponiuliza nilimjibu, kila nilipomjibu aliandika kwenye karatasi iliyopo
kwenye faili lake.
“Mnaishi wangapi
katika hiyo nyumba?” lilikuwa ni baadhi tu ya maswali niliyokumbana nayo kutoka
kwa kachero huyo. Swali hilo nililijibu kwa kusema kuwa tunaishi wawili tu
katika hiyo nyumba, yaani mimi na Kishoka.
Mara aliniuliza
uhusiano wangu na Kishoka, nami nilimjibu kuwa Kishoka ni mpangaji wangu katika
nyumba yangu niliyorithi kutoka kwa marehemu kaka yangu, kaka James ambaye
alikufa kifo cha kujiua mwenyewe kwa kujifyatulia risasi kichwani baada ya
kumuua aliyekuwa mpenzi wake pamoja na jamaa aliyemfuma akilamba asali ya
mapenzi kwa mpenzi wake huyo..
“Sasa
kwa nini umeamua kumuua Kishoka?” Askari huyo alinifyatulia swali jingine. Nami
nilimjibu bila kusita wala kujing’atang’ata kwamba mimi sijaua.
“Kama wewe hujaua, ni nani aliyemchinja
Kishoka ilhali mnaishi wawili tu katika hiyo nyumba?”
Nilijitahidi
kuwa makini sana katika maelezo yangu ili nisijikanganyekanganye halafu
nikaonekana nimeua kweli. Niliamua kumtaja muuaji, nikasema kuwa ni msichana
fulani ambaye alianza kunifanyia vioja tangu juzi nilipokutana naye ufukweni.
Nilieleza jinsi mambo yalivyokuwa kati yangu na mwanadada huyo kule ufukweni.
Nilipoulizwa
jina lake na mahali alipokuwa anaishi niliishia kusema sina nijualo juu yake.
Nilijaribu kurudia tena kutoa maelezo jinsi nilivyokutana na msichana huyo,
sikuwa namfahamu hata kidogo, lakini yeye alidai kuwa ananifahamu na kwa
kunithibitishia hilo alinitajia hadi jina langu. Hakuishia hapo tu, aliongeza
kuwa mpaka kwangu alikuwa anapajua hivyo akaniahidi atanitembelea kesho yake
asubuhi.
“Ilipofika
kesho yake asubuhi kweli alikuja?” Aliendelea kuhoji askari huyo huku
akionekana kunisikiliza kwa makini sana.
“Ndiyo alikuja lakini vilikuwa ni vioja
vitupu!”
“Uliweza kuonana naye na mkaongea nini?” Aliniuliza
afande nami nikaanza kumdadavulia vile ilivyojitokeza tangu msichana huyo
anafika pale getini, akakaribishwa na Kishoka lakini akakataa kuingia ndani.
Niliendelea
kueleza jinsi msichana huyo alivyopotea kimazingara tusimuone alikoelekea. Nilizidi
kuweka wazi kila kilichojitokeza mpaka wakati nilipokikuta kichwa cha Kishoka
kikiwa kimetenganishwa na kiwiliwili chake. Nilimalizia kwa kusema kuwa muuaji
si mimi bali ni huyo msichana ambaye kwa vyovyote vile si binadamu wa kawaida.
Askari
huyo aliyakataa katukatu maelezo yangu na kuniambia kuwa mimi ni muongo na hayo
maelezo yangu hayawezi yakanifikisha kokote, akasema jeshi la polisi haliamini
ushirikina wala mazingazi. Akanitaka nieleze ukweli ili aone ni jinsi gani
ataweza kunisaidia. Nilimwambia ukweli wangu ndiyo huo na sikuwa na maelezo
mengine zaidi ya hayo.
Afande
huyo nilimuona akifunga faili lake na kuniambia nijiandae kwenda kuozea jela.
Alichodai ni kwamba laiti kama ningeeleza ukweli basi angeweza kunisaidia.
************************
NINI HATIMA YA BRIGHTON? USIKOSE
KUFUATILIA MWENDELEZO WA HADITHI HII TAMU NA YENYE KUSISIMUA!
No comments:
Post a Comment