ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Baada ya kumwambia
hivyo jaji aliutaka upande wa mashtaka kuandaa maelezo ya mashtaka kuonyesha ni
kwanini unamuona mshtakiwa anahatia kwa mujbu wa ushahidi uliotolewa. Shauri
hilo liliahirishwa tena kwa mwezi mmoja.
*************************
SASA ENDELEA.......
Siku zilipita. Tarehe
ya kesi iliwadia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ambayo upande wa mashtaka ulitakiwa
kutoa maelezo ya uchambuzi wa kisheria ya kueleza ni kwa jinsi gani inaniona
mshtakiwa nina hatia kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa.
Tayari nilikuwa
nimeshapandishwa kizimbani. Ndipo nilipomuona mwendesha mashtaka amesimama
kisha akaanza kutoa maelezo mbele ya mahakama ya kuwa upande wa mashtaka
umeleta mashahidi walioweza kuthibitisha ya kwamba nilikuwa nimetenda kosa la
kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudia, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Akaendelea kueleza
kwamba ushahidi uliotolewa umeonyesha dhahiri kuwa nilimchinja Kishoka kwa
mikono yangu nikitumia kisu kilichokutwa karibu na mlango kama ushahidi
ulivyokuwa umeeleza.
Akaendelea kusema
kuwa licha ya mshtakiwa kudai kuwa aliyetoa taarifa za awali hakutaka
kujitokeza kituoni mara baada ya kutoa taarifa hizo, shahidi huyo ambaye
alikuwa ni mwanadada huenda aliogopa kwenda kituo cha polisi kutokana na
kuchanganyikiwa baada ya kushuhudia ndugu yake akiuawa kikatili ama kutokana na
desturi iliyojengeka miongoni mwa waafrika wengi ya kukiogopa kituo cha polisi
hata kama hawana hatia.
“Hata hivyo shahidi
huyo alifanya jambo kubwa na la maana kwa kutoa taarifa kituo cha polisi.”
Alizidi kueleza mwendesha mashtaka huyo ambaye ni bwana Charles Ngonyani.
Halikadhalika kuhusu
madai yangu ya kudai kuwa msichana huyo alikuwa ni mshirikina au jini,
mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba hayo yalikuwa ni madai yasiyokuwa ya
msingi na mantiki hivyo shahidi huyo alikuwa na haki ya kunifungulia kesi nyingine
kwa kumzushia ya kwamba ni mchawi na ni jini. Pia aliongeza kwa kusema kuwa
mahakama huwa haiamini imani potofu za kichawi kama mimi nilivyokuwa nikidai.
Hata kuhusu wakili
wangu mwendesha mashtaka alidai kuwa wakili huyo alijaribu kufanya usanii mbele
ya mahakama kwa kujifanya kashindwa kuongea kutokana na uchawi aliokuwa akisingiziwa
Sharifa ili kujenga hoja yetu, lakini ukweli ni kwamba shahidi huyo alikuwa
ameishiwa hoja za kisheria kutokana na ukweli uliokuwa umetolewa na mashahidi
wa upande wa mashtaka.
Suala la wakili wangu
kufariki dunia mwendesha mashtaka alisema kuwa hiyo ni mipango ya Mungu hivyo
asisingiziwe Sharifa.
“Hivyo kulingana na
mashahidi waliotoa ushahidi mbele ya mahakama hii tukufu, ni juu ya mahakama
kumuona mshtakiwa ana hatia ya kuua kwa kukusudia na hivyo tunaitaka imuhukumu
kifo kwa mujibu wa sheria.” Alimalizia mwendesha mashtaka na kuketi.
Niliumia sana
kumsikia mwendesha mashtaka huyo akaniona mharifu na kuiomba mahakama inihukumu
kifo wakati maskini wa Mungu nilikuwa sijatenda hiyo dhambi ya mauaji. Hata
hivyo sikuweza kumlaumu sana kwa vile wajibu wa waendesha mashtaka ni kuwaona
washtakiwa wana hatia hata kama hawajafanya makosa.
Baada ya mwendesha
mashtaka kumaliza kutoa maelezo yake, jaji Aneth Mwalukwa alinitazama na
kuniuliza,
“Na upande wako mshtakiwa unajibu nini?”
Nilighutuka
na kujikuta mapigo yangu ya moyo yakiongeza kasi. Hata hivyo sikuwa na lolote
la kuongea bali nilisema kuwa upande wa mashtaka umeniona na hatia kwa vile
mauzauza hayakuwatokea wao. Laiti kama yangewatokea hata mara moja basi
wangeamini yote niliyoyasema.
Pia
niliongeza kwa kusema kuwa mimi sijabobea sana katika mambo ya sheria hivyo
nisingeweza kutoa mapingamizi ya kishera juu ya maelezo ya upande wa mashtaka.
Nilimalizia kwa kusema kuwa ni juu ya jaji kuyapima maelezo yangu na ya upande
wa mashtaka.
Wakati
wote huo jaji alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo niliyokuwa nikiyatoa. Baada ya
kumaliza aliniambia kuwa ninawajika kujitetea kwa kosa lililokuwa linanikabili
kwani ushahidi uliokuwa umetolewa ulikuwa unaonyesha ya kwamba nimetenda kosa.
Nilianza
kujitetea palepale. Niliiambia mahakama ya kuwa sikuwa na chuki na Kishoka wala
hatukuwa katika mgogoro. Niliendelea kueleza kuwa tukio la kuuawa kwa kifo
hicho lilinisikitisha sana kwani siku hiyo asubuhi niliagana naye na nikaenda
katika mizunguko yangu.
“Ndipo
aliponipigia simu muda wa jioni akiniambia kuwa kuna mgeni wangu hapo nyumbani,
mgeni mwenyewe alikuwa ni yule aliyekuwa anatusumbua toka asubuhi akiwa
anagonga geti wakati mimi napata kifungua kinywa.”
Nilizidi
kueleza jinsi mgeni huyo ambaye kwa pale mahakamani nilikuja nikamjua jina lake
kuwa ni Sharifa. Nilieleza jinsi nilivyopokea taarifa kutoka kwa Kishoka ya
kuwa mgeni huyo alikuwa amekataa kuingia ndani na kunitaka niende hukohuko getini
nikaonane naye.
Niliendelea
kuieleza mahakama kuwa baada ya kwenda hapo getini sikukuta mtu. Kwa kirefu
kabisa nilieleza mauzauza yote aliyokuwa akinifanyia msichana huyo mpaka ile
jioni niliporudi kwangu na kumkuta Kishoka kashauawa chumbani mwangu.
“Mambo
ya ushirikina yapo na yanatokea sana katika jamii zetu hivyo mahakama isinione
kama naongea uongo.” Nilizidi kujitetea.
Mwisho
wa utetezi wangu niliitaka mahakama inione sina hatia na iniachie huru kisha
nikafunga kinywa changu.
Baada
ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga
siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.
HAYA SASA, TAREHE YA HUKUMU YA
BRIGHTON YATAJWA. JE, ITAKUWAJE? USIKOSE SEHEMU YA 32
No comments:
Post a Comment