ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....
Alisema
kuwa siku aliyotoka kuongea na mimi kwenye hospitali ya magereza alikutana na
msichana aliyekuwa akitusumbua katika kesi hiyo. Msichana aliyekuwa
amenisingizika kuwa nimeua wakati sijaua.
SASA ENDELEA.......
“Nilikutana naye
sokoni niliposimama kununua matunda, ndipo akaniita wakati naingia kwenye gari
niondoke zangu sokoni hapo. Kusema kweli nilikuwa sijamfahamu ila alipofika
kwangu alijitambulisha.” Alieleza wakili Mlyanyama.
“Akakuambia vipi?” Nikamuuliza huku nikikaa
makini kusikia alichomwambia wakili wangu.
“Eti kanionya niachane na kesi yako kwa sababu
hainihusu, akadai vinginevyo nitapata matatizo makubwa.”
Taarifa
hiyo ilininyong’onyeza na kunifanya niishiwe nguvu.
“Hivyi huyu mwanamke ananitafuta nini mimi?”
Nilimaka kwa machungu.
“Hata hivyo nilimwambia sitishiki na nikamtaka
ajipange kujibu maswali yangu yangu siku atakayosimama kutoa ushahidi.”
“Lakini yule ni mtu hatari sana kaka, bora
uachane tu na kesi yangu nisije nikakusababishia matatizo.” Nilimwambia wakili
Mlyanyama.
“Hapana, hayo ni maneno ya vitisho tu, ameona
hana hoja za kunikabili na huenda kashaambiwa jinsi ninavyowakaba maswali
mashahidi wengini au huwa anakuja kinyemela na kashashuhudia.”
“Kaka mimi
nimekuambia, yule msichana ni mchawi, hii kesi achana nayo tu wanihukumu
yaishe.” Nilimwambia wakili huyo.
Hata
hivyo wakili huyo alikataa katakata kuiachia njiani kesi yangu. Aliapa kuwa na
mimi bege kwa bega mpaka pale ambapo kingeeleweka. Alikuwa na kiu ya haki
kwangu mithili ya mzee Toboa katika Kiu ya Haki.
Tuliagana
na kuachana huku tukisubiri kesho yake ifike ili nipande tena kizimbani
kuendelea na kesi yangu. Nilizidi kupata wasiwasi juu ya hiyo kesi yangu. Kama
mpaka yule wakili alikuwa kapewa vitisho na yule msichana, niliwaza bila kupata
jibu ni kipi hasa alichokuwa akikitafuta msichana yule kutoka kwangu.
Kwa
kweli nilikuwa na mtihani, tena mzito. Nilitamani nikutane naye uso kwa macho kisha nimuulize kinagaubaga ni nini hasa
nilichokuwa nimemkosea ama ni kipi alichokuwa anahitaji kutoka kwangu.
Kesho
yake asubuhi tulisombwa tena na karandinga la magereza kuelekea mahakamani.
Tulipofika mahakamani mimi nilipelekwa moja kwa moja mpaka ndani kwani kesi
yangu ndiyo ilikuwa inaanzia kusikilizwa.
Jaji
alipoingia watu wote walisimama wakati sauti ya “kooort” iliposikika. Baada ya
kutoa heshima ya mahakama watu wote waliketi, kesi yangu ikaendelea.
Upande
wa mashtaka uliendelea kuleta mashahidi wake ambapo baadhi ya polisi waliokuwa
wamekuja kunikamata nyumbani siku ya tukio walisimama mmoja baada ya mwingine kutoa
ushahidi.
Wakili
wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kuwahoji. Yeye alichodai ni kwamba
anamsubiri kwa hamu shahidi ambaye alitoa taarifa za tukio hilo kwenye kituo
cha polisi. Shahidi huyo hakuwa mwingine bali ni yuleyule msichana mwenye kiinimacho.
Baada
ya polisi hao kuisha wote kutoa ushahidi, msichana huyo ambaye nilikuwa simjui
hata jina aliinuka na kwenda kwenye kizimba cha upande wa pili kutoa ushahidi
wake.
Kama
ilivyo ada, mwendesha mashtaka alimuongoza kutoa maelezo hatua kwa hatua.
“Mimi naitwa Sharifa Abdul.” Alitaja jina lake
baada ya kuulizwa na mwendesha mashtaka.
“Sharifa, hebu ieleze
mahakama ulikuwa wapi mnamo tarehe ishirini na moja mwezi wa kumi na moja mwaka
jana muda wa jioni?” Ilikuwa ni sauti ya mwendesha mashtaka bwana Charles
Ngonyani.
“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani kwangu
Majengo mapya, ndipo nilipoamua kwenda kumtembelea kaka yangu ambaye ni
marehemu Kishoka.”
“Endelea..,”
“Nilipofika alipokuwa
akiishi kaka yangu huyo nilikuta milango ipo wazi.”
“Huyo kaka yako alikuwa akiishi wapi?”
Mwendesha mashtaka aliuliza.
“Alikuwa akiishi mtaa wa Tumaini.”
“Alikuwa akiishi na nani?”
“Alikuwa amepanga na alikuwa akiishi na
mmiliki wa nyumba hiyo.”
“Ehe, ulipokuta
mlango upo wazi ulichukua uamuzi gani?”
“Kabla sijagonga nilisikia sauti ya kilio na
makelele mle ndani ambapo sauti ya mtu aliyekuwa akitoa kilio niliitambua.”
“Ilikuwa ni sauti ya nani?”
“Ilikuwa ni sauti ya kaka yangu Kishoka.”
“Uliposikia hivyo ulifanyaje?”
“Niliamua kuingia mpaka sebuleni, hata hivyo
makelele hayo yalikuwa yakitokea chumbani.”
“Chumba hicho kilikuwa ni cha nani?”
“Kilikuwa ni cha mmiliki wa nyumba hiyo.”
“Baada ya hapo ulifanyaje?”
“Baada ya kuuona hata mlango wa chumbani
haujafungwa, nilianza kwenda kwa tahadhari kubwa kuchungulia kilichokuwa kinaendelea
ndani ya chumba hicho.”
“Uliweza
kuchungulia humo ndani?”
“Ndiyo!”
“Ulipochungulia uliona nini?”
“Nilichokiona sikuamini kwa macho yangu.
Nilimuona kijana mwenye nyumba akimchinja Kishoka kama mbuzi wa sherehe
achinjwavyo huku kamfunga kamba miguuni na mikononi.”
“Ulipoona hivyo
uliamua nini?”
“Kwanza niliongopa kuongea chochote kwa
kuhofia usalama wangu. Kwa bahati nzuri nilikuwa na kamera kwenye mkoba wangu,
nikaitoa na kuanza kupiga picha.”
“Baada ya hapo afanyaje?”
“Nilitoka na kuondoka mbio kurudi nyumbani,
wakati nikiwa njiani nilipiga simu kituoni na kutoa taarifa hizo.”
“Hizo picha
ulizozipiga siku ya tukio unazo?”
“Ndiyo zimo kwenye kamera yangu hii.” Aliongea
Sharifa huku akiionyesha mahakama kamera ndogo ya digitali.
“Huyo mtu aliyefanya hayo mauaji ukimuona
unaweza ukamfahamu?”
“Bila shaka!”
“Hebu tuonyeshe kama mtu huyo yumo humu ndani
ya mahakama!”
“Ni yule pale kwenye kizimba.” Aliongea
msichana huyo huku akinisonta.
JE, WAKILI WA BRIGHTON ATAWEZA
KUMKABILI KWA MASWALI MSICHANA ALIYEMUONYA AACHANE NA HIYO KESI? NA NI MADHARA
YAPI ATAYAPATA KWA KUKAIDI ONYO LA MSICHANA HUYO? USIKOSE TOLEO LIJALO!
No comments:
Post a Comment